• Nairobi
  • Last Updated May 19th, 2024 9:01 PM
MBWEMBWE: Bruno Fernandes si magoli tu pia kuunda pesa hafanyi mzaha

MBWEMBWE: Bruno Fernandes si magoli tu pia kuunda pesa hafanyi mzaha

Na CHRIS ADUNGO

BRUNO Miguel Borges Fernandes, 26, ni kiungo mvamizi raia wa Ureno ambaye kwa sasa anachezea klabu ya Manchester United ya Ligi Kuu ya Uingereza (EPL).

Akiwa mzaliwa wa eneo la Maria viungani wa jiji la Porto nchini Ureno, Fernandes alianza kupiga soka kitaaluma akivalia jezi ya kikosi cha Novara katika Ligi ya Daraja la Pili (Serie B) nchini Italia.

Aliridhisha sana na kuvutia timu ya Udinese iliyomsajili 2013 kabla yake kuhamia Sampdoria miaka mitatu baadaye.

Baada ya kupiga soka ya kulipwa nchini Italia kwa miaka mitano, Fernandes alijiunga na Sporting CP ya Ureno mnamo 2017 na kupokezwa utepe wa unahodha.

Aliongoza orodha ya wafungaji bora wa Ligi Kuu ya Ureno mnamo 2018 na 2019 huku akitawazwa Mchezaji Bora wa Mwaka katika kila moja ya misimu hiyo.

Msimu 2018-29 alifunga jumla ya mabao 33 katika mashindano yote na akaweka rekodi ya kuwa kiungo wa Ureno aliyetinga idadi kubwa zaidi ya magoli katika soka ya bara Ulaya katika msimu mmoja.

Ubora wa matokeo yake msimu huo yalimfanya kivutio cha vikosi vingi duniani.

Hata hivyo, alihiari kutua kambini mwa Man-United kwa Sh9.5 bilioni mwezi Januari 2020.

Fedha hizo zilimfanya mchezaji wa pili ghali zaidi baada ya Cristiano Ronaldo kuwahi kusajiliwa kutoka Ureno.

Aliwajibishwa na timu ya taifa ya Ureno kwa mara ya kwanza Novemba 2017 baada ya kuwa tegemeo kambini mwa chipukizi wa U-19, U-20 na U-21.

Baada ya kuwakilisha Ureno katika Kombe la Dunia 2018 nchini Urusi, Fernandes aliongoza timu yake ya taifa kutwaa kombe la UEFA Nations League 2019.

Ukwasi

Mwanzoni mwa mwaka huu, jarida la Forbes lilimweka Fernandes katika nafasi ya 31 miongoni mwa wanasoka wanaovuna hela nyingi zaidi.

Thamani ya mali yake inakadiriwa kufikia kima cha Sh4.5 bilioni.

Anakula Sh28 milioni kwa wiki na zaidi ya Sh1.3 bilioni kwa mwaka ugani Old Trafford.

Pia hutia mfukoni Sh365 milioni kama malipo ya kuwa balozi wa mauzo ya bidhaa na huduma za kampuni mbalimbali kama Nike, ndani na nje ya Ureno. Dili hizi za kibiashara humvunia zaidi ya Sh40 milioni mwishoni mwa mwezi.

Majengo

Fernandes anamiliki jumba la Sh600 milioni jijini Lisbon, Ureno. Moja kati ya majengo mengine anayojivunia nchini Ureno ni lile la Sh660 milioni analotumia kwa shughuli za kibiashara mjini Maia. Kwa sasa anaishi katika kasri la Sh560 milioni jijini Manchester, Uingereza.

Magari

Kwa mchezaji wa kiwango chake, Fernandes anamiliki magari ya haiba kubwa.

Baadhi ya michuma ya kifahari anayosukuma ni pamoja na Range Rover Evoque, Mercedes CL63, Aston Martin, Ferrari na Audi S9.

Magari haya yanakisiwa kumgharimu Fernandes kima cha Sh168 milioni.

Mapenzi na Familia

Fernandes alianza kutoka kimapenzi na kichuna raia wa Ureno, Ana Pinho, 25, mnamo 2013.

Walifunga pingu za maisha miaka miwili baadaye na wamejaliwa mtoto mmoja – Matilde aliyezaliwa mwishoni mwa 2015.

Maazimio

Ingawa Fernandes alitia saini mkataba wa miaka mitano na nusu na Man-United mwanzoni mwa mwaka 2020, matamanio ya mkewe ni kumuona kiungo huyo akivalia jezi za Juventus nchini Italia, kabla ya kuyoyomea Amerika kupiga kabumbu ya Major League Soccer (MLS).

You can share this post!

UDAKU: Melanie awachoka visura kudonadona penzi lake na...

Kafyu ya unyama