• Nairobi
  • Last Updated May 3rd, 2024 10:50 AM
Mifumo ya teknolojia anayotumia kuendeleza kilimo

Mifumo ya teknolojia anayotumia kuendeleza kilimo

Na SAMMY WAWERU

ENEO la Juja, Thika Super Highway ni lenye shughuli chungu nzima, kuanzia za kibiashara, masomo na uchukuzi na usafiri.

Ni katika mtaa huo, tunakutana na Miriam Karuitha, ambaye ni mkulima. Hafanyi bora kilimo, ila kilimo bora. Karuitha, ni mwanazaraa wa mimea ya thamani, kama vile pilipili mboga za rangi tofauti.

Maarufu kama hoho, kwa ushirikiano na mume wake, alianza kilimo cha zao hilo baada ya kuhangaishwa na soko la mboga. “Mboga ni nzuri japo zinapaswa kulenga msimu bora. Mazao yakilingana na msimu ambao zimefurika sokoni, bei huwa duni,” asema.

Anafichua, awali alikuwa akikuza sukuma wiki, spinachi, mboga za kienyeji kama vile mnavu maarufu kama managu, mchicha – terere, na sagaa. Aidha, Karuitha hulima pilipili mboga za rangi ya; manjano, nyekundu na za kijani.

Miriam Karuitha akionyesha mtambo wa teknolojia ya kisasa, maarufu kama Automated Irrigation Controller, anaotumia kunyunyizia mimea maji kivungulioni…Picha/SAMMY WAWERU

Kulingana na Peter Kang’acha, mkulima hodari wa pilipili mboga Kaunti ya Murang’a, zao hilo huwaniwa sokoni kwa sababu ya rangi yake. “Mbali na virutubisho vyake kiafya, wateja wengi wanaridhia hoho kwa sababu ya rangi yake maridadi,” Kang’acha aelezea, akisema ametambua siri ya pilipili mboga ni kukuza zile za rangi.

Karuitha, ambaye ana Shada ya Uzamili katika kozi ya Molecular Biology & Bioinformatics aliingilia kilimo cha hoho 2019. “Mazao ya thamani yana ushindani mkuu sokoni,” asema. Amekumbatia kilimo cha mvungulio, maarufu kama green house.

Ana vivungulio viwili, ambavyo vimewagharimu maelfu ya pesa kuwekeza. Kivungulio cha kwanza, kina kipimo cha mita 9 kwa 5.5, kilichogharimu Sh215, 000. Cha pili, chenye ukubwa wa mita 25 kwa 10, nacho kina dhamani zaidi ya Sh700, 000.

Kilimo cha mvungulio kinasifiwa kusaidia kudhibiti kero ya usambaaji wa magonjwa na wadudu kwa mimea. “Manufaa yake ni tele, yakilinganishwa na ukuzaji wa mimea eneo tambarare, ambalo upepo huchangia msambao wa wadudu na magonjwa,” afafanua Caroline Murage, mtaalamu.

Mkulima Miriam Karuitha amekumbatia matumizi ya malighafi asilia kukuza pilipili mboga za rangi tofauti…Picha/ SAMMY WAWERU

Kabla kuingia kwenye kivungulio, langoni Karuitha ameweka maji yaliyotibiwa na dawa kuua viini vinavyosababisha magonjwa. “Haturuhusu yeyote yule kuingia ndani ya vivungulio. Kwa anayeruhusiwa, lazima makanyagio yake ya viatu yaloweshwe kwenye maji kuua vijidudu vinavyosambaza magonjwa,” aelezea.

Isitoshe, anayeingia sharti avalie aproni. Magonjwa yanayoibukia vivungulioni, Karuitha amekumbatia mfumo wa kisasa katika kilimo, maarufu kama Hydroponic System, kuyakabili. Aidha, ni mbinu isiyotumia udongo kupanda mimea, na badala yake kutumia malighafi asili kama vile; Pumice na maganda ya mpunga – mchele.

Malighafi hayo yametengenezewa mfano wa vitanda, vilivyoinuliwa juu kiasi kwa minajili ya upanzi. Hukuza miche kwa kutumia coco peat na peat moss. Mfumo wa hydroponic unasaidia kupunguza athari za magonjwa haswa yanayosababishwa na udongo na pia yanayosalia udongoni.

Unasifiwa kusaidia kufanikisha uzalishaji wa mazao bila kutumia fatalaiza na dawa zenye kemikali. Hata ingawa si asilimia mia kwa mia kukabiliana na wadudu na magonjwa, dawa hupuliziwa haja inapoibuka. “Umesaidia kwa kiasi kikubwa kupunguza gharama ya kilimo,” Karuitha asema.

Miriam Karuitha akielezea kuhusu mfumo wa kunyunyizia mimea na mashamba maji kwa kutumia mifereji…Picha/SAMMY WAWERU

Mkulima huyo vilevile amekumbatia matumizi ya mkojo wa sungura, pilipili hoho (zile kali), majani ya mmea asilia aina ya akapulko, kupambana na changamoto za wadudu na magonjwa. “Hupondaponda mimea hiyo na kuichanganya na mkojo wa sungura, mchanganyiko huo tunauweka kwenye mashina ya mimea,” aelezea.

Vitanda vinavyopandwa pilipili mboga, vimesindikwa mifereji ya kunyunyizia mimea maji. Imeunganishwa na mtambo wa teknolojia ya kisasa – Automated Irrigation Controller, uliosetiwa kuachilia lita 150 ya maji kila baada ya saa moja. Mtambo huo huhudumu kati ya saa mbili asubuhi hadi saa kumi alasiri, Karuitha akiuridhia kusaidia kupunguza gharama ya maji.

Ni kutokana na teknolojia hiyo ya kisasa, Karuitha hakosi kuwa na mazao. Kando na hoho, vilevile hukuza nyanya.

Baadhi ya malighafi ambayo Miriam Karuitha hutumia kuendeleza kilimo ili kukabiliana na kero ya magonjwa na wadudu…Picha/ SAMMY WAWERU

You can share this post!

Ngirici kuwania ugavana kama mwaniaji huru

Laikipia inaweza kugeuzwa kutoka eneo kame kuwa uga wa...

T L