• Nairobi
  • Last Updated September 28th, 2023 10:25 PM
Laikipia inaweza kugeuzwa kutoka eneo kame kuwa uga wa kilimo

Laikipia inaweza kugeuzwa kutoka eneo kame kuwa uga wa kilimo

Na SAMMY WAWERU

KENYA ni miongoni mwa mataifa matatu yaliyoorodheshwa kuathirika kwa kiwango kikubwa na janga la ukame katika Upembe wa Afrika.

Tangazo hilo lilitolewa na Shirika la Chakula na Kilimo (FAO – UN). Nchi zingine ni Ethiopia na Somalia, FAO ikisisitiza inahitaji msaada wa dharura kusaidia watu milioni 1.5 wanaokabiliwa na baa la njaa.

Makali ya ukame yanapotajwa, zaidi ya kaunti 20 Kenya hazikosi kushirikishwa. Laikipia, ni mojawapo ya kaunti hizo, na baadhi ya maeneo yamejiunga na orodha ya yanayoendelea kupokea chakula cha msaada.

Licha ya makali ya kiangazi, baadhi ya wakazi wanahisi eneo hilo linaweza kukombolewa kutoka katika minyororo ya ukame endapo serikali ya kaunti na ile kuu itawekeza kwenye mifumo ya kuvuna na kuhifadhi maji.

Nanyuki, ni kati ya maeneo yanayounda Kaunti pana ya Laikipia, na ni katika eneo lilo hilo Gad Kamarei anaendeleza shughuli za kilimo. Akiwa mmiliki wa ekari mbili, hukuza mseto wa mimea, kuanzia nyanya, vitunguu na mboga.

Gad Kamarei akikagua nyanya zake kwenye kivungulio…Picha/ SAMMY WAWERU.

Amekumbatia kilimo cha mvungulio, almaarufu green house. Vilevile, mwanazaraa huyu huzalisha mazao katika eneo tambarare. Anasema, alichukua mkondo huo baada ya kufanya utafiti wa kina, uliojumuisha kutembelea wakulima waliofanikiwa Nyeri, Laikipia na Meru.

“Isitoshe, nilijituma kushiriki maonyesho ya kilimo kuvuna maarifa na ujuzi zaidi,” Kamarei adokeza. Ufumbuo huo wa macho ulikuwa baada ya majaribio kadha katika ufugaji wa kuku na ng’ombe wa maziwa.

“Awali, nilijaribu kufuga ng’ombe wa maziwa Trans Nzoia ninakotoka, ila jitihada hizo hazikuzaa matunda nilivyotarajia. Sikuwa na budi ila kuinua mikono na kusaliti amri,” aelezea, akikadiria hasara.

Kutia msumari moto kwenye kidonda kinachouguza majeraha, Kamarei pia alijaribu kilimo cha mahindi wakati ambapo viwavijeshi vilikuwa kero kuu nchini. “Wadudu hao nao hawakunipa afueni,” akumbuka.

Licha ya mahangaiko hayo, Kamarei anakiri kutulizwa na mimea anayokuza akiitaja kuwa ya thamani. “Vilevile, hulima kabichi, brokoli, koliflawa, sukuma wiki, spinachi na mboga za kienyeji,” asema. Hali kadhalika, hukuza kabichi zikiwemo zile za rangi nyekundu, maboga na matango.

Nyanya za Gad Kamarei anazokuza kwenye kivungulio eneo kame….Picha/ SAMMY WAWERU.

 

Safari ya kilimo Nanyuki, eneo ambalo ni kame, aliianza 2016. Alitangulia na sukuma wiki, spinachi, mseto wa mboga za kienyeji na maboga, kwenye ploti. “Majirani na wakazi waliridhia mazao, nami nikaona mwanya wa kilimo-biashara,” asema.

“Kufikia 2017, niliona nuru ya ufanisi katika kilimo, nikanunua ekari mbili,” Kamarei afichua. Ameboresha shamba lake kupitia uwekeza wa mifumo ya kuvuna maji inayojumuisha kisima chenye kina cha urefu wa futi 40 na tangi la kuyahifadhi, lita 10, 000.

Amewekeza pakubwa katika mfumo wa kunyunyizia mimea na mashamba maji kwa kutumia mifereji. Kijumla, anasema mifumo ya mvungulio, kuvuna na kuhifadhi maji na kuyanyunyizia mimea, imemgharimu maelfu ya pesa.

“Haijakuwa mteremko, ikizingatiwa kuwa nimelazimika kuchukua mikopo kuafikia azma yangu katika kilimo,” afafanua. Kulingana na Daniel Mwenda, mtaalamu, kilimo bora kinafanikishwa na uwepo wa maji ya kutosha na mifumo kunyunyizia mimea na mashamba maji.

“Serikali inapaswa kuwekeza katika uchimbaji na ujenzi wa visima, vidimbwi na mabwawa,” asema mdau huyo, akisisitiza baa la njaa linaloshuhudiwa nchini litakabiliwa kikamilifu katika siku za usoni kupitia uvunaji maji.

Gad Kamarei akielezea kuhusu kilimo cha nyanya kivungulioni eneo kame, Nanyuki, Kaunti ya Laikipia…Picha/ SAMMY WAWERU.

“Nchi kame kama vile Israili, hakuna tone la maji ya mvua linalopotea. Kwa sababu gani? Inathamini ukusanyaji na uvunaji maji kupitia mabwawa na vihifadhio vingine,” Mwenda aelezea.

Ni aibu kwa serikali ya Kenya kuahidi wananchi mabwawa, kisha mgao unaotengewa shughuli hiyo kufyonzwa kupitia ufisadi na ubadhirifu wa mali ya umma. Isitoshe, inasikitisha kuona viongozi na wanasiasa wakijishughulisha na kampeni kuwania viti vya kisiasa kufuatia uchaguzi mkuu mwaka huu.

Hatua ya Gad Kamarei kuonyesha ukakamavu kukomboa eneo kame, ni ya uzalendo. Mbinu anazotumia kuendeleza kilimo ni ishara kuwa zinaweza kuleta afueni katika kaunti zingine zinazokodolewa macho na hatari ya kiangazi.

Huku jitihada zake zikitambuliwa na serikali ya Kaunti ya Laikipia, ni miongoni mwa wakulima wa kipekee wanaotegemewa na hoteli na mikahawa kuisambazia mazao mabichi ya shambani. Aidha, Nanyuki ina vivutio maridadi kwa watalii.

Mkulima Gad Kamarei akionyesha nyanya alizovuna…Picha/ SAMMY WAWERU.

You can share this post!

Mifumo ya teknolojia anayotumia kuendeleza kilimo

KCSE 2021: Kaunti ya Kwale yalenga kuendeleza rekodi nzuri...

T L