• Nairobi
  • Last Updated May 10th, 2024 7:50 AM
MIKIMBIO YA SIASA: Watumishi wafahamu afadhali nusu ya shari

MIKIMBIO YA SIASA: Watumishi wafahamu afadhali nusu ya shari

NA LEONARD ONYANGO

IDADI Kubwa ya maafisa wa serikali waliojiuzulu kufikia Februari 9, mwaka huu, na kujitosa katika siasa walikosa tiketi.

Mawaziri wa zamani, Sicily Kariuki (Maji) na Charles Keter ni miongoni mwa maafisa wakuu wa serikali waliojiuzulu kutoka serikalini lakini hawatakuwa debeni katika Uchaguzi Mkuu wa Agosti 9.

Bi Kariuki alijitoa kwenye kinyang’anyiro cha ugavana wa Nyandarua kwa tiketi ya Jubilee na badala yake akatangaza kumuunga Gavana wa sasa Francis Kimemia.

“Uongozi ni kujinyima. Kujiondoa katika kinyang’anyiro hakumaanishi kwamba mimi ni dhaifu. Nitatumikia watu wa Nyandarua kupitia wadhifa tofauti,” akasema.

Ni Kariuki alipokuwa akizungumza katika makao makuu ya Jubilee, Alhamisi.

Mkurugenzi wa uchaguzi wa Jubilee, Kanini Kega alisema kuwa chama hicho kiliamua kumpa tiketi Bw Kimemia ili kuongeza uwezekano wa Jubilee kuhifadhi kiti hicho katika uchaguzi mkuu ujao.

Naye Bw Keter alikubali kushindwa baada ya kupoteza kura za mchujo wa chama cha United Democratic Alliance (UDA) katika kinyang’anyiro cha ugavana wa Kericho.

Keter alikuwa wa pili kwa kura 60,342 nyuma ya Dkt Erick Mutai aliyeibuka mshindi kwa kura 126,038.

Mawaziri wengine waliojiuzulu ni Adan Mohamed (Afrika Mashariki) na John Munyes (Madini) ambao wanawania ugavana wa Mandera na Turkana mtawalia wangali katika kinyang’anyiro.

Watumishi wengine wa serikali ambao wamejipata katika baridi ya kisiasa ni Bw Kiema Kilonzo na mwana wa kinara wa Wiper Kalonzo Musyoka, Kevin Muasya.

Bw Kilonzo alikuwa balozi wa Kenya nchini Uganda hali Bw Muasya alijiuzulu kutoka wadhifa wa Bodi ya Wakurugenzi ya Mamlaka ya Utalii na kujitosa katika siasa.

Bw Muasya alikuwa mwaniaji mwenza wa ugavana wa Bw Kilonzo katika Kaunti ya Kitui lakini Bw Musyoka aliwanyima tiketi ya Wiper na kumkabidhi gavana wa zamani Julius Malombe.

Bw Kilonzo amewasilisha kesi mbele ya jopo la kuamua mizozo ya vyama vya kisiasa (PDDT) kupinga hatua ya Wiper kumpa tiketi Bw Malombe.

Aliyekuwa Waziri Msaidizi (CAS) wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) Ken Obura pia alijipata pabaya baada ya kukosa tiketi ya ODM kuwania ugavana wa Kaunti ya Kisumu.

ODM ilitoa tiketi ya moja kwa moja kwa Gavana Anyang’ Nyong’o ambaye atapeperusha bendera ya chama hicho katika Uchaguzi Mkuu ujao.Bw Obura analenga kuwania kiti hicho kama mgombea wa kujitegemea.

Inspekta Jenerali wa Polisi wa zamani na Naibu Waziri wa Utalii Joseph Boinett pia hatakuwa debeni baada ya kubwagwa katika kura za mchujo za chama wa UDA.

Bw Boinett aliyekuwa akiwania ugavana wa Elgeyo Marakwet alibwagwa na Bw Wesley Rotich.

Alhamisi, Bw Boinett aliahidi kutowania kiti hicho kama mgombea wa kujitegemea baada ya kukutana na Naibu wa Rais William Ruto mtaani Karen, Nairobi.

Naibu Rais Ruto amekuwa akikutana na wawaniaji waliokosa tiketi na kuwasihi kutowania kama wagombea huru kwa kuhofia kugawanya kura na kutoa mwanya kwa wapinzani ‘kupitia katikati’.

Ruto amekuwa akiwaahidi waliokosa tiketi katika mchujo nyadhifa serikalini iwapo atashinda urais na kuteuliwa katika Bunge la Afrika Mashariki (EALA).

Aliyekuwa mbunge wa Starehe Charles Njagua, almaarufu Jaguar, wiki iliyopita alidai kuwa aliahidiwa na Dkt Ruto ubunge EALA iwapo atakubali kuunga mkono mbunge wa EALA Simon Mbugua ambaye atapeperusha tiketi ya UDA katika eneobunge hilo.

Bw Jaguar, hata hivyo, ameshikilia kuwa atatetea kiti chake kama mwaniaji wa kujitegemea licha ya ahadi ya ubunge wa EALA.

Dkt Ruto pia anadaiwa kumsihi aliyekuwa Katibu wa Wizara ya Madini John Mosonik kuachana na mpango wake wa kutaka kuwania ugavana wa Bomet kama mwaniaji wa kujitegemea kutokana na hofu ya UDA kupoteza kiti hicho.

Bw Mosonik aliyejiuzulu wadhifa serikalini na kujitosa katika siasa, aliambulia patupu katika mchujo wa UDA baada ya kubwagwa na Gavana Hillary Barchok.

Iwapo Bw Mosonik atawania kama mgombea huru, huenda akagawa kura na kutoa mwanya kwa gavana wa zamani Isaac Ruto wa Chama cha Mashinani (CCM) kuibuka mshindi.

Aliyekuwa Balozi wa Kenya nchini China Sarah Serem ambaye alijiuzulu kujaribu bahati katika ugavana wa Uasin Gishu pia alijipata katika baridi ya kisiasa baada ya kupoteza katika mchujo wa UDA.

  • Tags

You can share this post!

TAHARIRI: Kibaki awe kioo cha wawaniaji wa urais

Norwich City washushwa daraja katika EPL

T L