• Nairobi
  • Last Updated May 4th, 2024 7:12 PM
TAHARIRI: Kibaki awe kioo cha wawaniaji wa urais

TAHARIRI: Kibaki awe kioo cha wawaniaji wa urais

NA MHARIRI

MAZISHI ya Rais Mstaafu Mwai Kibaki nyumbani kwake Othaya, Kaunti ya Nyeri, Jumamosi yalikuwa kilele cha maisha ya rais huyo ambaye amesifiwa kitaifa na kimataifa kwa uongozi wake mahiri uliopelekea nchi hii kuonekana kwenye ramani ya Afrika na ulimwengu kwa jumla.

Rais Mstaafu Kibaki, ambaye alifariki Aprili 21, amesifiwa kama mtu aliyependa uaminifu na mchapakazi wa aina yake.

Aliamini katika kuwatumikia wananchi bila ya kuwa na kundi la wasaidizi wa karibu na wafuasi waliomzunguka wakifuja mali ya umma.

Ajabu ni kwamba hata kabla ya kuzikwa, Hospitali ya Kitaifa ya Kenyatta iliyoko Othaya ilibadilishwa jina na kuitwa Hospitali ya Mwai Kibaki kufuatia mashauriano na familia yake na maafisa wa serikali.

Pia kumekuwa na wito wa kutaka barabara kuu ya Thika ya urefu wa kilomita 45 ipewe jina lake. Angalipinga hili kama angalikuwa hai.

Kibaki aliingia madarakani wakati ambapo viongozi wa Afrika waliweka picha zao kwenye sarafu za kitaifa.

Alikubali tu kutambulishwa kwa sarafu ya Sh40 kwa ukumbusho na hakuna zaidi ya hapo.

Hali kadhalika, sarafu hiyo haijapata umaarufu zaidi nchini kwani haipatikani sana.

Alistawisha uchumi wa Kenya, huku biashara zikiwa zimeshamiri na benki zikistawi.

Kwa hakika, alisimamia mpango wa mageuzi ambao uliinua uchumi kutoka chini ya asilimia 0.6 ya ukuaji wa Pato la Taifa hadi takriban asilimia saba.

Bila shaka, kulikuwa na changamoto kama vile kashfa za ufisadi na machafuko baada ya uchaguzi wa 2007, lakini mema aliyofanyia nchi yalizidi mabaya.

Moja ya mafanikio yake makubwa ilikuwa mpango wa elimu ya msingi bila malipo, ambao umenufaisha mamilioni ya watoto.

Urithi wake tajiri unapaswa kutumika kama msukumo wa kukuza zaidi elimu na kuinua uchumi.

You can share this post!

Wanasiasa wasifu marehemu Kibaki

MIKIMBIO YA SIASA: Watumishi wafahamu afadhali nusu ya shari

T L