• Nairobi
  • Last Updated May 17th, 2024 2:31 PM
MITAMBO: Mashine ya kisasa inayosaga nyasi za mifugo na kuchanganya na nafaka kwa pamoja

MITAMBO: Mashine ya kisasa inayosaga nyasi za mifugo na kuchanganya na nafaka kwa pamoja

NA SAMMY WAWERU

BEI ya chakula cha mifugo cha madukani ingali ghali, licha ya serikali kutangaza mikakati kuishusha.

Mikakati hiyo inajumuisha kuondoa kwa muda ada na ushuru unaotozwa malighafi kukitengeneza na ya chakula chenyewe.

Aidha, Kenya huagiza kutoka nje asilimia 80 ya malighafi, Muungano wa Watengenezaji Chakula cha Mifugo Nchini (Akefema) ukisema mfumko huo wa bei umechangiwa na ushuru wa juu.

“Baadhi ya wakulima wamelazimika kuacha shughuli za ufugaji, kwa sababu ya gharama ya juu inayochochewa na bei ya chakula cha mifugo,” asema Martin Kinoti, Katibu Mkuu Akefema.

Kulingana na afisa huyo, chini ya kipindi cha muda wa miaka miwili viwanda 37 vya kuunda malisho vimefungwa.

Shayiri, mahindi, soya, alizeti, ngano na mbegu za pamba ni kati ya malighafi yanayotumika kukiunda.

Wakulima na wafugaji wamekuwa wakihimizwa kukumbatia mifumo kujitengenezea, ili kushusha gharama.

Hatua hiyo inashirikisha matumizi ya mashine za kusaga.

Kampuni ya Trapp, yenye makao yake makuu Brazil, inaendelea kujituma kuletea wafugaji suluhisho.

Imezindua mashine ya kisasa, inayosaga nyasi, majani ikiyachanganya na malighafi kama vile nafaka kwa pamoja na wakati mmoja.

Wakulima na wafugaji wakati wa Maonyesho ya Kimataifa ya Agritech Africa, KICC jijini Nairobi, Nelson Omwalo kutoka Ubalozi wa Brazil hapa nchini akiwajuza kuhusu mashine iliyoboreshwa ya Chaff Cutter. PICHA | SAMMY WAWERU

Multipurpose Chaff Cutter, imeboreshwa na ina vichujio ambavyo mfugaji hubadilisha saizi ya malisho anayotaka kwa kutumia swichi.

“Mbali na kuwa mashine ya kukatakata nyasi au majani, husaga nyasi za mabingobingo na aina yoyote ile pamoja na nafaka ikichanganya kwa wakati mmoja,” asema Nelson Omwalo, afisa kutoka Ubalozi wa Brazil hapa nchini.

Mfano, ikiwa mfugaji analenga kusaga na kusindika chakula cha ng’ombe wa maziwa au kuku, Omwalo anasema, anabofya swichi ambayo ni ya moja kwa moja kulingana na saizi ya ‘punje’ anazotaka.

Isitoshe, inafanikisha uwiano wa kiwango cha chakula kwa mujibu wa vigezo faafu.

Mashine hiyo ikiwa na injini yenye nguvu za 7Hp, inatumia mafuta ya petroli.

Aidha, ina tangi linalositiri lita mbili za mafuta, Omwalo akidokeza kwamba tayari mashine zenyewe zimetua humu nchini kuletea wafugaji afueni.

“Zinapatikana katika duka la Fyeka Ventures, moja ikigharimu Sh75,000,” aelezea afisa huyo.

Brazil ni tajika ulimwenguni katika utengenezaji na usambazaji wa vifaa na mashine za kilimo na ufugaji, ikiwa imekumbatia mifumo na teknolojia za kisasa.

Ubalozi wa taifa hilo ulikuwa miongoni mwa waonyeshaji wa vifaa, mashine na mitambo ya ufugaji ng’ombe, kuku na mbinu za kisasa kuendeleza kilimo na ufugaji, walioshiriki Maonyesho ya Kimataifa ya Agritech Africa.

Maonyesho hayo ya makala ya saba, yaliandaliwa katika jumba la mikutano ya kimataifa la Kenyatta (KICC) jijini Nairobi.

Aidha, yalihudhuriwa na kampuni na mashirika kutoka nje na ndani ya nchi.

  • Tags

You can share this post!

West Ham wajinasia maarifa ya beki Flynn Downes kutoka...

KeNHA kuunda barabara ya Sh5.5 bilioni Thika

T L