• Nairobi
  • Last Updated April 28th, 2024 4:55 PM
Mkuki kwa Raila, kwa Ruto mchungu

Mkuki kwa Raila, kwa Ruto mchungu

NA CHARLES WASONGA

VUTA nikuvute inayoendelea kati ya serikali na mrengo wa Kenya Kwanza kuhusiana na madai ya kutumika kwa machifu kufanikisha ushindi wa mwaniaji wa urais wa Azimio la Umoja-One Kenya, Bw Raila Odinga, inaashiria umuhimu wa maafisa hao katika siasa.

Hii ni licha ya kwamba, kimsingi, wajibu wa maafisa hawa wa utawala ni kudumisha usalama katika ngazi za mashinani na hawapaswi kuegemea mrengo wowote wa kisiasa.

Katika siku za hivi karibuni, Naibu Rais William Ruto ambaye ni mgombea urais kwa tikiti ya chama cha UDA, alidai kuwa serikali inawatumia maafisa wa serikali kufanikisha ushindi wa Bw Odinga katika uchaguzi mkuu wa Jumanne.

Akiongea katika mikutano ya kampeni sehemu mbalimbali nchini, Dkt Ruto alidai kuwa na habari kwamba kuna njama ya kuwatumia machifu na manaibu wao kuwakodi watu watakaozua fujo katika vituo vya kupigia kura katika ngome zake ili kuwazuia raia kujitokeza kushiriki shughuli hiyo.

“Tunajua kuwa mikutano ya usiku inafanyika hasa katika ngome zetu ambapo machifu wanalazimishwa kuwasajili hadi watu 30 kwa ajili ya kuvuruga uchaguzi katika kila kituo cha kupigia kura. Mipango hii yote inaendeshwa kwa amri ya Fred Matiang’i, Karanja Kibicho na rais mwenyewe anafahamu njama hii,” akasema alipoongoza kampeni za Kenya Kwanza mjini Nakuru.

Mgombea-mwenza wa Dkt Ruto, Rigathi Gachagua pia ameendeleza madai hayo akisema maafisa hao wa utawala pia wanatumiwa kuwezesha wizi wa kura ili kufanikisha ushindi wa Bw Odinga.

Lakini Dkt Matiang’i aliye waziri wa Usalama, amekana madai hayo akisema wamekuwa wakifanya mikutano na machifu na maafisa wengine wa utawala kupanga taratibu za kazi ya kudumisha usalama katika ngazi za mashinani kipindi hiki cha uchaguzi.

“Inasikitisha kuwa wanasiasa wanadai kuwa tunakutana na machifu na manaibu wao kwa lengo la kuingilia uchaguzi. Mikutano ambayo maafisa katika wizara yangu wamekuwa wakiendeleza na machifu sehemu mbalimbali nchini huwa ni ya kujadili masuala ya kiusalama wakati huu wa uchaguzi. Machifu na manaibu wao ndio macho na masikio yetu katika maeneo ya mashinani wanakohudu na itakuwa vigumu kwa serikali kudumisha usalama bila kushirikiana nao,” Dkt Matiang’i akasema.

Aliyekuwa mkuu wa mkoa wa Nyanza na Nairobi, Joseph Kaguthi anasema maafisa wa utawala wa mkoa, hasa machifu, ni kiungo muhimu zaidi katika uchaguzi mkuu. Hii ni kutokana na wajibu mkubwa walionao katika ushirikishaji na usimamizi wa shughuli za usalama.

“Malumbano yanayoendelea kuhusu nafasi ya machifu na manaibu wao katika uchaguzi mkuu ujao si kitu kigeni. Yamekuwepo hata katika chaguzi zilizopita kwa sababu wao ndio husimamia usalama katika ngazi za kata na kata-ndogo,” anasema kwenye mahojiano ya kipekee.

Kuhusu madai kuwa maafisa hawa wanaweza kutumika kuendeleza ajenda za kisiasa, Bw Kaguthi ambaye alistaafu mnamo 2008, anasema hivi: “Siwezi kukubali kuwa maafisa hawa hutumika kisiasa au hawatumiki kisiasa. Kile ambacho unapaswa kufahamu ni kuwa hawa ni maafisa wanaotumikia serikali ambayo inaongozwa na Rais na naibu wake ambao, kimsingi, ni wanasiasa”.

“Kwa mfano, ilidaiwa kuwa sisi ambao tulihudumu katika enzi za utawala wa hayati Daniel Moi, tulikuwa tunatumika kufanyia kampeni chama tawala, nyakati hizo, Kanu. Hii ni kwa sababu ilikuwa vigumu kutofautisha kati ya sera za serikali na mipango ya chama tawala,” Bw Kaguthi anaeleza.

Kwa upande wake, mchanganuzi wa masuala ya uongozi Barasa Nyukuri anasema kuwa kwa msingi wa majukumu yao kama maafisa waliotwikwa wajibu wa kuvumisha sera za serikali na kusimamia usalama katika ngazi za mashinani, machifu ni kiungo muhimu zaidi katika ulingo wa siasa za uchaguzi wa urais.

“Naibu Rais, Dkt Ruto anafahamu fika jambo hilo kwa sababu yeye na Rais Kenyatta walisaidiwa pakubwa maafisa hao wa utawala kuelekea chaguzi za 2013 na 2017. Hii ndiyo maana nyakati hizo, Bw Odinga na wandani wake ndio waliokuwa wakilalamikia mwenendo huu wa machifu kutumika katika kampeni za mrengo wa serikali,” anasema Bw Nyukuri.

Itakumbukwa kuwa Julai 22, 2017, wakiendesha kampeni katika kaunti ya Makueni, Rais Kenyatta na Dkt Ruto, walitishia kuwapiga kalamu machifu katika Kaunti ya Makueni ambao walionekana kuunga mkono mrengo wa upinzani, NASA.

Nyakati hizo, Waziri Matiang’i, ambaye sasa anashutumiwa kuwatumia machifu kumpigia debe Bw Odinga, alikuwa akitetewa vikali na Dkt Ruto.

Katika hali inayoshadidia tamathali kuwa “mkuki kwa nguruwe kwa mwanadamu mchungu”, Alhamisi, Dkt Ruto aliungama kuwa 2017, ilikuwa makosa kwake na Rais kuwatumia machifu na maafisa wengine wa serikali kuwapigia debe katika jitihada zao za kuchaguliwa tena.

“Ninasikia wengine wakisema kuwa tulitumia machifu 2017, hiyo ni kweli na ilikuwa ni makosa. Wakati huu hamna haja ya kurudia kosa ambalo lilifanyika wakati ule mwingine. Wakati huu, tunafaa kuzingatia taratibu zilizowekwa katika sheria kwa kutowatumia machifu kuvuruga uchaguzi au kuiba kura,” Dkt Ruto akasema kwenye kikao na wanahabari katika makazi yake rasmi katika mtaa wa Karen, Nairobi.

  • Tags

You can share this post!

SOKOMOKO WIKI HII: Wajackoyah na mdogowe walivyopigwa na...

Uaminifu wa Mutua kwa Ruto wayumba

T L