• Nairobi
  • Last Updated May 17th, 2024 12:48 PM
Mogotio yapata ofisi ya usajili kwa mara ya kwanza

Mogotio yapata ofisi ya usajili kwa mara ya kwanza

NA MERCY KOSKEI

KAUNTI ndogo ya Mogotio, Baringo imepata afisi mpya ya usajili wa raia.

Ufunguzi wa kituo hicho cha kusajili watoto wanaozaliwa na visa vya vifo, imeletea wakazi wa Mogotio afueni ikizingatiwa kuwa ni cha kwanza katika eneo hilo.

Kinakadiriwa kitasaidia zaidi ya watu 90,000 kutoka wadi tatu za Kisanana, Mogotio na Emining ambao wamekuwa wakisafiri kilomita nyingi kupata stakabadhi na vyeti muhimu vya kuzaliwa na kuandikisha vifo.

Husafiri hadi Eldama Ravine, Kabarnet na Nakuru mjini kusaka huduma.

Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, Katibu katika Wizara ya Uhamiaji na Huduma za Raia Balozi Julius Bitok alikiri kuwa wakazi wamekuwa na matatizo ya kujiandikisha kutokana na gharama kubwa za usafiri na muda.

Akiongoza hafla ya kuzindua rasmi afisi hiyo, Bw Bitok alifichua kwamba eneobunge la Mogotio ni asilimia 60 pekee ya watu waliopata cheti cha kuzaliwa, huku waliofariki asilimia 27 jamii zao zikipata vyeti vya vifo.

Afisa huyo aidha alihimiza machifu kuhamasisha wakazi kujitokeza kwa wingi kupata vyeti hivyo muhimu.

“Mbunge wa Mogotio aliwasilisha malalamishi yenu katika afisi yangu, kufuatia changamoto zinazowakumba kupata vyeti vya kuzaliwa na kuandikisha visa vya vifo.

“Uzinduzi wa kituo hiki ni ishara kuwa serikali imejitolea kuhakikisha huduma zinaletwa karibu na wananchi,” alisema Balozi huyo.

“Tunalenga kuhakikisha kila mtu anapata chetu cha kuzaliwa, na walioaga jamaa zao wapate cha kifo. Hati hizi ni muhimu katika maisha ya mtu. Wakazi 1000 wa kwanza watakaofika kujisajili watapata huduma bila gharama yoyote,” aliahidi.

Balozi Julius Bitok, Katibu katika Wizara ya Uhamiaji na Huduma za Raia akizindua afisi mpya ya usajili wa raia Mogotio, Kaunti ya Mogotio. PICHA / MERCY KOSKEI

Katibu huyo alielezea kwamba kituo hicho kipya ni cha tatu kufunguliwa katika Kaunti ya Baringo.

Kituo cha kwanza kilifunguliwa mwaka wa 1971 mjini Kabarnet, nacho cha pili 1994 Eldama Ravine na kuidhinishwa na Rais Mstaafu Marehemu Daniel Arap Moi.

Bw Bitok aliwataka wazazi kutumia mwanya huo kutafutia watoto wao cheti cha kuzaliwa, ikizingatiwa kuwa Wizara ya Elimu imeweka sheria lazima kila mwanafunzi anayejiunga na chekechea awe na cheti hicho muhimu.

Akifurahia kufunguliwa kwa ofisi hiyo, mbunge wa Mogotio Reuben Kiborek alielezea jinsi wapiga kura wake wamekuwa wakihangaika kupata huduma hizo muhimu.

“Hii ni ishara kuwa hata mgao wa fedha za karo itakuwa rahisi kupata, na kusaidia kuboresha elimu eneo hili,” Bw Kiborek akasema.

Alisema afisi hiyo itawapa wakazi Mogotio nafasi za ajira, akidokeza kwamba tayari vijana wawili wameshapata kazi.

Balozi Julius Bitok, Katibu katika Wizara ya Uhamiaji na Huduma za Raia (katikati) akizindua afisi mpya ya usajili wa raia Mogotio, Kaunti ya Mogotio. PICHA / MERCY KOSKEI

Bw Richard Kimaru, mkazi, alishindwa kuficha furaha na tabasamu yake akikumbuka mahangaiko ambayo wenyeji wamepitia kusaka vyeti vya kuzaliwa na vya waliofariki.

“Ni afueni, kwani tulikuwa tunasafiri zaidi ya kilomita 80 na kukadiria gharama isiyopungua Sh1, 000,” alisema.

Naye Bw Daudi Chepkurgor mkazi wa Kisanana alisikitika kuwa watoto wengi wamelazimika kuacha shule, kwa sababu ya ukosefu wa cheti cha kuzaliwa kujiandikisha kufanya mtihani wa kitaifa darasa la nane (KCPE.

“Tunafurahi kwamba huduma sasa ziko karibu nasi, hata sisi wazee tutapata zetu. Wazazi kwa sasa hatuna kisingizio cha kutokuwa na vyeti vya watoto wetu,” Chepkurgor alisema.

“Asilimia 50 ya wazee Mogotio hawana cheti cha kuzaliwa, lakini sasa wana matumaini kukipata.”

[email protected]

  • Tags

You can share this post!

Ngono: Sasa mapadre, maaskofu kuadhibiwa

Vyakula vya Iftar vinavyoenziwa Lamu

T L