• Nairobi
  • Last Updated May 2nd, 2024 8:55 PM
Ngono: Sasa mapadre, maaskofu kuadhibiwa

Ngono: Sasa mapadre, maaskofu kuadhibiwa

NA MASHIRIKA

VATICAN CITY, VATICAN

VIONGOZI wa Kanisa Katoliki sasa watawajibikia wenyewe makosa ya dhuluma za kingono yatakayofanyika katika maeneo wanakosimamia.

Hii ni baada ya Papa Francis kuifanyia mageuzi sheria ya 2019 ya kukabiliana na dhuluma za kimapenzi katika kanisa hilo.

Kwa mujibu wa barua iliyotumwa moja kwa moja na kiongozi huyo, Papa alisema kuwa kuna uwezekano watu wazima pia wakawa waathiriwa wa vitendo hivyo, vinavyoendeshwa na baadhi ya mapadre. Sheria ya awali iliwatambua watoto kama waathiriwa pekee wa maovu hayo.

“Sheria mpya inasema kuwa viongozi wanaohudumu katika maeneo yanayotambulika na kanisa watawajibikia makosa yanayofanyika katika maeneo hayo,” yakasema makao makuu ya Vatican kwenye taarifa.

Sheria hiyo mpya itaanza kutekelezwa Aprili 30.

“Sheria hiyo haijumuishi tu dhuluma dhidi ya watoto pekee, bali inaangazia kutowajibika kwa viongozi wanaoongoza maeneo hayo,” ikaongeza Vatican.

Hilo linajiri huku Papa Francis akikubali hatua ya kujiuzulu ya Askofu Franz-Joseph Bode wa Osnabruek, nchini Ujerumani, aliyekubali kuwa alikosea pakubwa kuhusu jinsi alishughulikia vitendo vya dhuluma za kingono katika dayosisi yake.

Bode, 72, amekuwa akielekezewa shinikizo kali tangu Septemba mwaka uliopita, baada ya ripoti moja iliyotolewa na Chuo Kikuu cha Osnabruek kumlaumu kwa kutoshughulikia dhuluma za kingono dhidi ya watoto katika dayosisi yake.

“Nimekuwa nikisikitishwa sana na waliohusika na taasisi kuliko waathiriwa. Sikufanya vizuri. Nilifanya maamuzi yasiyofaa,” akasema Bode.

Askofu huyo, aliyehudumu katika dayosisi hiyo tangu 1995, “ameomba msamaha” kwa waathiriwa.

Licha ya kukataa miito ya kujiuzulu kwa viongozi waliohusishwa na maovu mengine hapo awali nchini Ujerumani, Vatican ilithibitisha Jumamosi kuwa Papa Francis amekubali “hatua ya askofu huyo kujiuzulu”.

Kwa mujibu wa utafiti wa chuo hicho mnamo 2018, jumla ya watoto 3, 677 walidhulumiwa kingono na viongozi wa kidini wa kanisa hilo kati ya 1946 na 2014.

Tangu alipoanza kuhudumu kama kiongozi wa kanisa hilo mnamo 2013, moja ya changamoto kuu ambayo Papa Francis amekuwa akikabiliwa nayo ni kukabili dhuluma za kingono miongoni mwa mapadre dhidi ya watoto, hasa katika nchi za Ujerumani, Ireland na Amerika.

Awali, hali haikumwendea vizuri sana, baada ya tume moja ya kuwalinda watoto kudharauliwa mbali mapadre wawili waliojiuzulu walipohusishwa na vitendo hivyo. Mnamo 2018, Papa alikabiliwa na wakati mgumu baada ya kumtetea padre mmoja kutoka Chile, aliyetuhumiwa kushiriki katika vitendo hivyo.

Hilo ndilo lilimfanya kubuni tume maalum ya kuwalinda watoto.

Mnamo 2019, aliandaa kikao nadra, ambapo waathiriwa wa vitendo hivyo walieleza madhila waliyokuwa wamepitia. Baada ya kikao hicho, papa aliapa kufanya kila awezalo kukabiliana na viongozi watakaobainika kuhusika.

Kanisa lilifanya mabadiliko makubwa katika sheria na taratibu zake, zilizowapa waathiriwa uhuru wa kuripoti visa vyovyote kama hivyo kwa mahakama maalum za kanisa.

  • Tags

You can share this post!

Serikali yafuta leseni za kampuni 26

Mogotio yapata ofisi ya usajili kwa mara ya kwanza

T L