• Nairobi
  • Last Updated May 17th, 2024 9:50 AM
Mradi wa Rais Mstaafu Uhuru Kenyatta wakwama Mukuru

Mradi wa Rais Mstaafu Uhuru Kenyatta wakwama Mukuru

NA SAMMY KIMATU

WAKAZI na waathiriwa katika tarafa ya South B ambao walipoteza nyumba, kazi na mali ili kupisha ujenzi wa barabara katika mpango wa Ajenda Nne Kuu za serikali ya Rais Mstaafu Uhuru Kenyatta, wanataka maelezo baada ya mradi kukwama.

Kwa mujibu wa mkuu wa tarafa ya South B, Bw Michael Aswani Were, mradi wa ujenzi wa barabara katika mitaa ya Mukuru ulikuwa ukamilike kabla ya Disemba 2022.

Hata hivyo, Taifa Leo imebaini kwamba hali ni tofauti mashinani.

Kwa mfano, kivukio cha wanaotembea kwa miguu kilikuwa cha kwanza kijengwe kuunganisha mtaa wa Kayaba na mtaa wa Hazina Novemba Mwaka jana na bado hakipo.

Mwathiriwa, Bw Urbanus Ngila Mwau aliye kadhalika mlemavu aliyemiliki kioski mtaani Kayaba alikuwa na matumaini ya kurudi kazini baada ya kukamilika kwa barabara ya Kayaba/Hazina lakini bado anasononeka.

Shughuli ya ubomoaji ikiendelea. PICHA | SAMMY KIMATU

“Tunakaribia mwaka mmoja tangu tubomoe nyumba, miradi ya vyoo, kliniki, bucha, saluni na vibanda vingine vya biashara ili kupisha ujenzi wa mradi wa rais. Leo hakuna chochote kinachoendelea na hatma ya barabara zilizonuiwa kujengwa mitaani haijulikani,” Bi Veronicah Njambi akaambia Taifa Leo.

Aidha, Taifa Leo ilibaini kwamba tingatinga zilizohusika katika ujenzi wa barabara husika zimesimamishwa karibu na kambi ya chifu ya Hazina bila kufanya kazi kwa wiki kadhaa.

Kando na hayo, barabara ya Kayaba/Hazina iliyonuiwa kupungua msongamano wa magari katika barabara kuu na iliyo kitovu cha Eneo la Viwandani ya Entreprise ingali bado kumalizika.

Taswira na hali ilivyo mashinani ni kwamba mwanakandarasi alimwaga mchanga juu ya mawe ambao siku hizi umeleta kero ya vumbi punde magari na pikipiki zivurumishapo vumbi zikitembea.

Fauka ya hayo, wakazi wa Mukuru walikuwa wengi wa matumaini baada ya kuambiwa mradi wa ujenzi wa nyumba za kudumu za gharama ya chini katika mtaa wa mabanda wa Mukuru-Mariguini utawafaa.

Tingatinga likivunja jengo lisilohitajika katika mtaa wa mabanda wa Mukuru-Hazina ulioko South B, kaunti ndogo ya Starehe jijini Nairobi kupisha ujenzi wa mradi wa barabara na nyumba nafuu chini ya mpango wa Ajenda Nne Kuu za serikali ya Rais Uhuru Kenyatta (ambaye sasa ni mstaafu). Mradi huo ulikwama. PICHA | SAMMY KIMATU

Kumbe wapi!. Baada ya watu kujiondolea nyumba na vibanda katika eneo lililopimwa litumike kwa ujenzi wa barabara tingatinga lilionekana siku moja na tangu wakati huo, kila kitu kimesimama.

Dhihirisho ni katika mtaa wa mabanda wa Mukuru-Fuata Nyayo, Mtaa wa mabanda wa Mukuru-Mariguini sawia na mtaa wa mabanda Mukuru-Commercial.

Naibu kamishna wa kaunti ndogo ya Starehe, Bw Jacob Ouma aliambia Taifa Leo kwamba atafuatilia suala la mradi huo kwa makini.

Hata hivyo, alieleza kwamba wakati huu kuna serikali ya mpito hivyo wananchi wasubiri serikali itoe mwelekeo kuhusu mradi huo.

“Mradi uliendeshwa chini ya serikali ya Rais Mstaafu Uhuru Kenyatta. Sasa uongozi ni wa Dkt William Ruto. Wananchi wasubiri serikali itapeana mwelekeo kwani serikali ni endelevu na kuna mpito wa uongozi unaoendelea. Kuweni na subira. Nitatoa taarifa kamili kwa wananchi na vyombo vya habari baadaye,” Bw Ouma akasema.

  • Tags

You can share this post!

Raila ashuka bei ngomeni mwake

GWIJI WA WIKI: Annette Odusi

T L