• Nairobi
  • Last Updated May 17th, 2024 8:50 AM
Mtaalamu aelezea kiini cha stroberi zako kukosa kuzaa matunda

Mtaalamu aelezea kiini cha stroberi zako kukosa kuzaa matunda

Na GRACE KARANJA

NI matunda ya rangi nyekundu ambayo yana ladha ya kipekee.

Stroberi aina ya chandler inaendelea kupata umaarufu miongoni mwa wakulima hapa nchini kwa sababu ya sifa zake za kukomaa haraka, kustahimili magonjwa na wadudu waharibifu, gharama ya kuzalisha na huchukua muda wa miezi mitatu matunda yake kukomaa.

Tunakutana na mmoja wa wakulima hawa ambaye amepitia changamoto si haba katika safari yake ya kukuza matunda haya. Peter Mwangi ni mkazi wa eneo la Mang’u. Amekuwa akijihusisha na kilimo cha aina mbalimbali cha mboga hadi pale alipoamua kuanza kukuza stroberi aina ya chandler.

“Nilifanya utafiti wangu katika mitandao ya kijamii na kuona vile wakulima wanaumiminia sifa mmea huu kwamba licha matunda yake kuwa na faida kiafya pia yanaweza kumpa mkulima mapato ya juu. Nilinunua miche lakini baada ya kupanda mimea yangu inaendelea tu kukua bado haijaanza kunipa hata tunda moja. Nimetumia zaidi ya Sh200,000 kugharimia kilimo hiki, nilihakikisha kwamba nimefuata taratibu zote zinazofaa lakini baada ya miezi saba bado sijaweza kupata hata senti, mimea inatoa maua tu,” Peter anaelezea masaibu anayokumbana nayo.

Kulingana na wataalamu, Peter ni mmoja tu kati ya wakulima wengi nchini ambao hawana ufahamu kwamba kuna aina nyingi za stroberi zinazokuzwa hapa nchini. Miongoni mwa inayokuzwa Kenya ni Chandler maarufu zaidi ya zingine, Douglas, Aiko, Pajaro, Fern, Cambridge, San Adrian miongoni mwa zingine. Aina hizi zote hukuzwa katika mazingira sawa ila tu zinatofautiana na muda wa kukomaa ilhali zingine zina matawi mengi. Hata hivyo matunda ya mimea hii ni tofauti kwa umbo, ladha, na muda wa kuharibika.

USHAURI

Vonnies Ombiro ni mtaalam wa mimea ya mazao kama vile mboga na matunda.

Kulingana naye, hakuna miche feki ila tu kuna aina tofauti za mimea ya stroberi kwani wakulima hawana ufahamu wa kutofautisha aina hizi.

Kuhusu suala la mmea kutokuwa na matunda, hii ni kwa sababu wakulima hawatilii maanani upimaji wa udongo kabla ya kufanya kilimo. Kupima udongo husaidia mkulima kujua kiwango cha asidi kilicho kwenye udongo pamoja na virutubisho. Kiwango kinachopendekezwa cha pH ni cha 5.5 na 6.5. Mkulima aelimishwe ni wakati gani mwafaka wa kuongeza virutubisho kwani utafiti unaonyesha kwamba mimea ya matunda inaweza kukua katika udongo ulio na asidi lakini hauwezi kuzaa matunda.

Ili kukuza mimea hii mvua ya mililita 1200 inahitajika la sivyo mkulima atahitaji kunyunyizia mimea yake maji mililita 25 kila wiki kwani mmea huu hauwezi kustahimili ukame. Njia moja inayopendekezwa na wataalam ni unyunyiziaji maji kwa mfumo wa matone yaani drip irrigation. Mfumo huu hufanya matunda kuwa makubwa na kuzaa zaidi hivyo kuongeza muda wa kuvuna.

Kulingana na mtaalam huyu maeneo ya Athi River, Kitengela, Sagana, Kinangop, Embu, Molo, Kiambu Kirinyaga, ni mwafaka kwa kukuza mmea wa stroberi. Hata hivyo anaeleza kwamba jua ni msaada mkubwa kwa mimea hii ya chandler.

Anaongeza kwamba kukuza mimea hii wakati wa jua hufanya matunda kuiva upesi na kuwa na rangi nyekundu iliyokolea ambayo huwavutia wateja.

Ardhi thumuni ya ekari 1/8 inatosha kuzalisha kati ya kilo 30-50 za matunda haya kwa kila wiki.Kwa sababu matunda haya huharibika kwa haraka hii ikiwa ni siku 4-5 baada ya kuvunwa, mkulima anashauriwa kutafuta soko mapema kabla ya matunda haya kukomaa.

You can share this post!

BIASHARA MASHINANI: Ubunifu wa upanzi wa maua umemzolea sifa

Dkt Ruto adokeza uwezekano wa kuungana na Raila katika...