• Nairobi
  • Last Updated May 1st, 2024 10:08 PM
BIASHARA MASHINANI: Ubunifu wa upanzi wa maua umemzolea sifa

BIASHARA MASHINANI: Ubunifu wa upanzi wa maua umemzolea sifa

Na PATRICK KILAVUKA

UBUNIFU wa mpanzi wa maua na miche kwenye kivuli (Indoor planting) Michael Ndichu Kimani wa kuunda masanduku ya kupanda na kukuzia maua na miche umekuwa njia mbadala ya kuhifadhi mazingira na kumchumia riziki ya kila siku.

Isitoshe, umewapa waraibu na wapenzi wa upanzi huo, njia ya kufanya ukuzaji maua na miche baada ya kutolewa kivulini mbali na kutoa suluhisho la kuboresha mazingira wanamokaa kwa kuyapandia maua na miche kulingana na ukubwa wa nyumba au varanda.

Anatengeneza masanduku hayo kwenye barabara ya Mwanzia 16, mzunguko wa Peponi.

Mpanzi huyu anasema alikuwa anapanda maua na miche kwenye mikebe, vikapu na nyungu lakini akawazia wateja wake wanaotaka kuyapanda ndani ya nyumba almaarufu (Indoor planting) ili watimize lengo la kutunza mazingira yao.

Kubuniwa kwa masanduku hayo kulingana na ukubwa, kumewawezesha wapenzi wa miche na maua kupata fursa ya kuyapanda kwa wingi.

Pia, mkulima huyo anasema upanzi huu, utaboresha ukuzaji maua na miti ya kila aina kwani miche ya kichaka (shrubs) itaweza hata kupandwa kulingana na ukubwa wa sehemu ya nyumba ndani au kwenye varanda kuboresha hewa safi kwenye makazi.

Bei ya masanduku baada ya kukamilika, huwa kati Sh20,000 na Sh 40,000 kulingana na ukubwa wake.

Anasema huyaunda baada ya kuihifadhi mbao vyema kuikinga dhidi ya uharibifu wowote. Isitoshe, kuepuka kugusana na maji, huweka ndani karatasi ya nailoni kwanza ndiposa aongezee mchanga na mbolea ya asili tayari kwa upanzi.

Pia, huacha nafasi baina ya mbao kupitisha maji ya kunyunyizia na hewa wakati inakua. Kwa kuwa wateja wanazidi kuyatambua, ameanza kuuza mawili hivi kwa mwezi na biashara inanawiri.

Changamoto kuu ya masanduku haya ni bei ghali ya mbao na uhifadhi wake.

Aina ya miche na maua akuzayo Michael Ndichu. Mbali na kuongezea umaridadi, mbinu hii inatunza mazingira. Picha/ Patrick Kilavuka

Anasema ari na mapenzi yake katika kilimo hiki imempelekea kuyakuza maua na miche ambayo ina uwezo wa kudhibiti jua kwa asilimia 75 na kuyawezesha kustahimili mazingira ya ndani akitumia kivuli maalum cha karatasi ya plastiki.

Alianza kazi hii mwaka 2001.Wakati huo, alikuwa anafanya kazi ya kutunza miche na maua kwenye maboma. Hata hivyo, alikuwa na ari ya kutunza mazingira.

Anasema alikuwa anaipanda miti na maua bomani mwao na kuitunza.

Isitoshe, ari hiyo ilimsukuma kujiunga kundi la Green Belt Movement ambalo lilikuwa linaongozwa na mwanamazingira maarufu marehemu Wangari Maathai.

Kimani alianza upanzi na mtaji wa Sh20,000 ambao alipewa kama mkopo na mmoja wa wateja aliokuwa akiwatunzia maua na miche bomani. Alinunua nyungu, vikapu na mikebe ya plastiki kwani wakati huo alikuwa ameanza kukuza maua na nyasi ya kufunika ardhi kama China, Lantana, Abutinia, Central dinia, Gazinia ambayo ilikuwa inachukua mwezi hadi miwili kukua na kuiuza Sh30-50.

Baada ya kumaliza ulipaji wa mkopo wa kwanza, alipewa mwingine wa Sh50,000 na akapiga jeki kazi.

Kuimarisha upanzi wake, alinunua vikapu na vyungu vyingine vikubwa na kuanza kukuza miche inayokua kama kichaka ambayo alianza kuiuza Sh300-1000 kwa kutegemea aina yake na ukubwa.

Mfano, ile inayosafisha hewa Peace Lily na Ferns aliiuza Sh500 na nyingine kama Vicers, Agronema, Bamboo minture akaiuza kati Sh1000-3000. Aina ya maua kama Orchids na Arthurium huuza Sh2,500 kwa kila kikapu, mikebe au nyungu.

Katika kufuatilia ukuzaji wa miche na maua, mpanzi huyu anayo kadi ambayo anampatia mteja kuhakikisha anaendelea kufuatilia ukuzaji unaostahili. Ana kampuni yake ya kutunza na kuhifadhi mazingira ya Beyond Beauty Landscapers.

Kadi humuelekeza mteja kuhusu wakati wa kuweka mbolea, kunyunyuzia na mchanga.

Ana wateja wa hapa nchini na ughaibuni kwani hutumia mtandao kuangazia kazi.

Mpanzi huyu tajriba yake imemwezesha hata kufunza wanafunzi wa NITA( National Industrial Trainning Authority) mafunzo kuhusu upanzi wa miche na maua kwenye nasari na kutunza mazingira.

Ana kampuni yake ya kutunza na kuhifadhi mazingira ya Beyond Beaty Landscapers.

You can share this post!

KILIMO NA MAZAO: Pato la nduma kwake si kubwa lakini...

Mtaalamu aelezea kiini cha stroberi zako kukosa kuzaa...