• Nairobi
  • Last Updated May 2nd, 2024 8:55 PM
MUTUA: Polisi wazingatie sheria na waepuke mauaji ya kiholela

MUTUA: Polisi wazingatie sheria na waepuke mauaji ya kiholela

Na DOUGLAS MUTUA

INASIKITISHA kuwa huenda enzi ya serikali kuwaua raia bila kufuata utaratibu rasmi wa sheria imerejea nchini Kenya.

Inanipa hofu mno kwani nilikuweko kikosi cha polisi kilichoitwa Kwekwe kilipodaiwa kuwatesa na kuwaua walioshukiwa kuwa wanachama wa kundi haramu la Mungiki.

Haikuwa raha kamwe kurauka na kukumbana na vichwa vilivyotenganishwa na viwiliwili au miili iliyojaa madonda ya risasi.

Ilikuwa kawaida kwa miili kupatikana maeneo kusikoishi watu. Iliyonata akilini mwangu ni picha ya mifupa ya miguu iliyookotwa eneo la Kitengela huku ikiwa bado na viatu.

Sasa siku hazipiti nyingi bila habari za mauaji sampuli hiyo kugonga vichwa vya habari. Cha leo ni kisa ambapo vijana wawili wanadaiwa kuuawa na maafisa wa serikali na miili yao kutupwa ndani ya Mto Chania, kijijini Rubiru, eneobunge la Gatanga, Kaunti ya Murang’a.

Nicholas Maithya, 20, na Asman John Kamau, 18, waliuawa yapata wiki mbili zilizopita.

Walioshuhudia wanasema vijana hao walifungwa pingu mikononi, wakateswa kisha wakatupwa mtoni humo ambamo maji yalijaa pomoni.

Kosa lao? Eti walikataa kuwaonyesha maafisa hao kunakopikiwa pombe haramu ya chang’aa!

Inadaiwa afisa mmoja alichukua jiwe akampiga kijana mmoja kwenye kisogo, akaanguka mtoni na kumvuta mwenzake waliyefungwa pingu pamoja.

Badala ya maafisa hao kuwaokoa mahabusu wao, walikiona hicho kama kioja cha kuchekwa, wakajiendea zao na kukaa kimya hadi wananchi waliporipoti kisa chenyewe.

Nalifahamu vizuri tu eneo hilo, sikwambii kuna watu ambao wamepika pombe hiyo haramu kwa miaka zaidi ya 30.

Miezi kadhaa iliyopita mtu amekatwa shingo na kutupwa msituni kwa madai aliwasaliti kwa polisi watu wanaoifanya biashara hiyo.

Ikiwa kuna watu wa kushikwa na kushtakiwa, basi ni hao waliokita mizizi kwenye biashara hiyo hivi kwamba miongoni mwa gharama zao ni hongo za machifu.

Inaaminika kuna juhudi za kuharibu ithibati ya uhalifu huo; polisi wanalaumiwa kwa kutoa pingu kwenye mwili wa mmoja wa wahanga wa uhalifu wao ulipopatikana ukielea mtoni.

Mauaji ya Maithya na Kamau yalitokea huku nchi ikiwa bado imeduwazwa na mauaji ya wanaume wanne waliotekwa eneo la Kitengela Aprili 19.

Miili ya Jack Anyango, 37, Elijah Obuong, 35, Benjamin Imbayi, 30, na Brian Odour, 36, ilipatikana kwenye mito na misitu mbalimbali ndani ya majimbo ya Murang’a na Kiambu.

Ingawa bado haijajulikana iwapo waliowateka ni polisi, miili yao ilikuwa na alama zilizoonyesha walifungwa pingu kabla ya kuuawa kinyama.

Na mauaji yao yalitokea huku majimbo matano yakiwa yamefungwa kutokana na janga la corona, hivyo miili yao ilivyopatikana nje ya kulikofungwa bado ni kitendawili.

Tusisahau wakili wa haki za binadamu, Bw Willie Kimani, wateja wake na dereva wa teksi walivyouawa kinyama na polisi eneo la Mavoko mnamo 2016.

Katika taifa lolote linalotawaliwa kisheria, washukiwa hukamatwa na kupawa fursa ya kujitetea mahakamani na kuadhibiwa wakipatwa na hatia.

Ni mchakato mzima ambapo mchunguzi, mkuu wa mashtaka, hakimu na anayeadhibu hasa huwa watu tofauti. Polisi wanapojitwika majukumu hayo yote ni hatari kubwa.

[email protected]

You can share this post!

Kila bandari Kenya kuwa na mkurugenzi wake mkuu

KAMAU: Serikali isiwasaliti wanafunzi kwa kuwanyima mikopo