• Nairobi
  • Last Updated May 2nd, 2024 4:10 PM
KAMAU: Serikali isiwasaliti wanafunzi kwa kuwanyima mikopo

KAMAU: Serikali isiwasaliti wanafunzi kwa kuwanyima mikopo

Na WANDERI KAMAU

WANAFUNZI wengi ambao hujiunga na taasisi za elimu ya juu kama vile vyuo vikuu huwa wanatoka katika familia maskini.

Vijijini wanakotoka, huwa wanaonekana kama “wakombozi” na “mashujaa” wanaostahili kuenziwa pakubwa, kwa kuhimili changamoto nyingi ambazo watoto wanaosomea maeneo ya mashambani hukumbwa nazo.

Ni wazi kuwa kama nchi nyingi zenye chumi za kadri, Kenya inakumbwa na changamoto za kifedha, mojawapo ya sababu kuu zikiwa kiwango kikubwa cha madeni inayodaiwa na mataifa ya nje na mashirika mengine ya kifedha.

Licha ya changamoto hizo, serikali imekuwa ikijizatiti pakubwa kufadhili sekta muhimu kama vile elimu.

Miongoni mwa masuala muhimu ambayo imekuwa ikitekeleza ni utoaji wa mikopo kwa wanafunzi wa vyuo vikuu na vyuo anuwai, ili kuwawezesha kulipa karo na kugharamia mahitaji yao ya msingi.

Mikopo hiyo huwa inatolewa kupitia Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu (HELB).

Kwa wanafunzi wanaotoka katika familia maskini, mikopo huwa kama “mkombozi” wao wanapojiunga na taasisi hizo.

Sababu ni kuwa wengi huenda kusoma bila usaidizi wowote kutoka kwa familia zao. Wengine hufanyiwa michango midogo midogo angaa kuwawezesha kupata pesa za matumizi ya kila siku kwa muda.

Ni hali za kawaida tulizoshuhudia vijijini mwetu.

Hata hivyo, inasikitisha kuwa licha ya kufahamu uhalisia huo, serikali imetangaza huenda zaidi ya wanafunzi 95,000 katika vyuo vikuu wakakosa kupata mikopo hiyo mwaka huu kutokana na changamoto za kifedha zinazoikumba.

Kulingana na Wizara ya Fedha, ufadhili unaopewa vyuo vikuu umepungua kutoka Sh109.3 bilioni mwaka uliopita hadi Sh99.9 bilioni katika mwaka wa kifedha wa 2021/2022.

Upungufu huo wa kifedha ndio unatarajiwa kuathiri taasisi muhimu kama vile HELB.

Bila shaka, huu si mwelekeo wa kuridhisha hata kidogo.

Ni hali ya kuatua moyo, ikizingatiwa kuwa hata wakati wa utawala wa Kanu, ilikuwa nadra sana kwa serikali kupunguza ufadhili kwa sekta ya elimu licha ya changamoto za kifedha zilizokuwa zikiikumba nchi.

Ikizingatiwa mojawapo ya ahadi ya serikali ya Jubilee ilikuwa kupanua sekta ya elimu ili kuwiana na mwelekeo wa kisasa duniani, hili si jambo la kuridhisha hata kidogo.

Badala yake, ni pigo kubwa kwa wanafunzi wachanga, hasa wanaotegemea mikopo hiyo kugharamia mahitaji ya msingi vyuoni mwao.

Ombi kuu kwa serikali ni kutathmini upya hatua hiyo, kwani ikiwa itaitekeleza, basi itakuwa imekisaliti kizazi cha sasa.

[email protected]

You can share this post!

MUTUA: Polisi wazingatie sheria na waepuke mauaji ya...

TAHARIRI: Ni bora michezo kurejea shuleni