• Nairobi
  • Last Updated May 16th, 2024 8:50 PM
MWALIMU WA WIKI: Iwapo ni siri ya ufanisi tu, hii hapa

MWALIMU WA WIKI: Iwapo ni siri ya ufanisi tu, hii hapa

NA CHRIS ADUNGO

TIJA na fahari ya mwalimu yeyote ni kuona mwanafunzi aliyeingia shuleni bila kujua lolote akipiga hatua kubwa kielimu na kuanza kufahamu vyema stadi za kusikiliza, kuzungumza, kusoma na kuandika.

Zaidi ya majukumu ya kawaida ya kufundisha, mwalimu pia ana wajibu wa kutambua, kukuza na kulea vipaji vya wanafunzi wake.

Haya ni kwa mujibu wa Bw Martin Njuguna Mwaura ambaye kwa sasa ni mwalimu wa Kiswahili na mkuu wa masuala ya mitihani katika shule ya msingi ya Kanyanjara, eneo la Kikuyu, Kaunti ya Kiambu.

“Tambua uwezo wa kila mwanafunzi ndani na nje ya mazingira ya darasani. Wahimize wajitahidi zaidi katika hicho wanachokipenda kufanya na uwe tayari kuwasaidia wanapopitia changamoto mbalimbali,” anasema.

“Mwalimu bora huelekeza wanafunzi kwa utaratibu ufaao huku akiwahimiza mara kwa mara katika safari yao ya elimu,” anaeleza.

Njuguna alizaliwa na kulelewa katika eneo la Maragua, Kaunti ya Murang’a. Ndiye kitinda mimba katika familia ya watoto tisa wa Bi Monicah Njoki na marehemu mwalimu Peter Mwaura.

Alianzia safari ya elimu katika shule ya msingi ya Wairuri, Maragua (1997-2004) kabla ya kujiunga na shule ya upili ya Maragua Ridge (2005-2008) kisha Chuo cha Mafunzo ya Ualimu cha St Augustine Ishiara, Kaunti ya Embu (2009-2011).

Baada ya kuhitimu, Njuguna alianza kufundisha katika shule ya msingi ya Waminne Winners Academy, Gatundu Kaskazini, Kaunti ya Kiambu.

Alihudumu huko kwa kipindi cha mwaka mmoja kabla ya kuhamia The Trinity School, Maragua (2012-2017) kisha Rockfields Junior School, Nairobi (2019). Tume ya Huduma kwa Walimu (TSC) ilimwajiri mnamo 2019 na kumtuma katika shule ya msingi ya Kanyanjara.

Kwa mtazamo wa Njuguna, jitihada zisizokadirika pamoja na ushirikiano miongoni mwa walimu, wazazi, wahisani na wanafunzi ni nguzo na mhimili wa mafanikio katika shule ya msingi ya Kanyanjara katika mitihani ya kitaifa.

“Siri ya kufanya wanafunzi wafaulu katika somo lako ni kuwasikiliza, kuelewa changamoto zinazowakibili kisha kuwaelekeza hatua kwa hatua. Ni vyema mwalimu kuwa mvumilivu na kuwatia shime wanafunzi wasio wepesi kulimudu somo lake,” anasema.

“Matumizi bora ya Kiswahili shuleni hutegemea sana kiwango cha ujuzi wa mwalimu, kiasi cha kutangamana kwake na wanafunzi, uelewa wake wa stadi za mawasiliano na wepesi wake wa kubuni mbinu anuwai za ufundishaji,” anaeleza.

Njuguna anapania sasa kuhimiza wanafunzi wake kuchangamkia usomaji wa Taifa Leo baada ya shule ya Kanyanjara kujisajili kwa mradi wa Newspapers in Education (NiE) unaoendeshwa na Nation Media Group (NMG).

Anaungama kuwa majaribio ya mitihani katika Taifa Leo kila Jumatatu na Jumanne ni jukwaa zuri kwa watahiniwa wa KCPE kujinoa na kukadiria uwezo wao katika masomo mbalimbali.

“Shindano la Uandishi wa Insha katika gazeti hili pia ni fursa adhimu kwa wanafunzi kufanya mazoezi kwa ajili ya mitihani na kuukuza ubunifu wao. Tuzo zinazotolewa kwa washindi zinaamshia wanafunzi hamu ya kukithamini Kiswahili,” anasema.

Kubwa zaidi katika maazimio ya Njuguna ni kujiendeleza zaidi kielimu na kuwa miongoni mwa walimu na waandishi watakaobadilisha sura ya ufundishaji wa Kiswahili humu nchini.

Kwa pamoja na mkewe Bi Lucy Wanjiru, wamejaliwa mtoto wa kiume – Griffiths Curtis Peter Mwaura. Bi Wanjiru kwa sasa ni mwalimu katika eneo la Machakos.

  • Tags

You can share this post!

MAPISHI KIKWETU: Sweet and sour chicken

Utawala wa Uhuru wang’aa katika ujenzi wa barabara

T L