• Nairobi
  • Last Updated May 17th, 2024 5:50 AM
MWALIMU WA WIKI: Mwalimu mlezi wa vipaji vya watoto

MWALIMU WA WIKI: Mwalimu mlezi wa vipaji vya watoto

NA CHRIS ADUNGO

KUFAULU kwa mwanafunzi shuleni hutegemea mtazamo wake kwa mwalimu na masomo yote anayofundishwa darasani.

Kwa kuwa uwezo wa wanafunzi kumudu masomo hutofautiana, mwalimu anastahili kuelewa kiwango cha kila mmoja na kubuni mbinu za ufundishaji zitakazomwezesha kufikia malengo ya kila kipindi.

Mwalimu Allan Wanjala Mukhwana katika shule ya Teresia’s Academy Gilgil, anashikilia kuwa mbinu rahisi zaidi ya kuamsha ari ya kuthaminiwa kwa masomo miongoni mwa wanafunzi ni kuwaaminisha kwamba hakuna lisilowekezana.

“Mwanafunzi asiye mwepesi wa kuelewa masomo darasani huvunjika moyo kwa urahisi iwapo mwalimu atamlinganisha na wenzake walio na uwezo wa kuelewa mambo haraka,” anatanguliza.

“Mwalimu bora huwa karibu na wanafunzi wake na hutia azma ya kufahamu changamoto wanazozipitia wakiwa shuleni na nyumbani. Anapaswa kuelekeza wanafunzi kwa utaratibu unaofaa na kuwahimiza wajitahidi masomoni,” anasisitiza.

Allan alizaliwa mnamo Mei 11, 1992 katika eneo la Tongaren, Kaunti ya Bungoma. Ndiye wa pili katika familia ya watoto watano wa Bi Monicah Naliaka Simiyu na marehemu Bw Joseph Wafula Mukhwana.

Alisomea katika shule za msingi za Sikhendu, Trans Nzoia (1997-1999), Rising Star Academy, Bungoma (2000-2003), Sunrise Academy, Trans Nzoia (2004) na All Saints Academy Kitale, Trans Nzoia (2005-2007).

Alijiunga baadaye na shule ya upili ya Chesamisi Boys, Bungoma (2008-2011) kabla ya kusomea shahada ya ualimu (Historia/Kiswahili) katika Chuo Kikuu cha Moi kati ya 2012 na 2015.

Kabla ya kuhitimu, Allan alishiriki mazoezi ya kufundisha katika shule ya Havard mjini Eldoret (2014).

Nafasi hiyo ilimpa jukwaa mwafaka la kuzima kiu ya ualimu na akaamsha ari ya kuthaminiwa kwa somo la Kiswahili miongoni mwa wanafunzi.

Alipata mafunzo ya nyanjani katika shule ya Kabuyefwe Girls, Trans Nzoia (2015) na akaajiriwa katika shule ya Muungano, Trans Nzoia mnamo 2016.

Alihudumu huko kwa miaka sita kabla ya kuhamia Teresia’s Academy Gilgil mnamo Januari 2022. Mbali na Kiswahili, anafundisha pia somo la Dini na P.E.

“Pamoja na kutumia vifaa vya kidijitali ambavyo husisimua wanafunzi, matumizi ya video, michoro na picha za rangi ni namna nyingine ya kufanya masomo kuvutia.”

“Kuhusisha wanafunzi moja kwa moja katika masomo yanayohitaji ubunifu wa kiteknolojia huwapa fursa ya kufanya mambo kwa kujiamini zaidi. Mawanda ya fikira zao hupanuka, uelewa wao huimarika na huanza kuona vitu wanavyofundishwa vikiwa vya kawaida mno,” anaeleza.

Kwa mujibu wa Allan, mwanafunzi akipata umilisi ufaao, atakuwa wa manufaa katika jamii ya sasa inayoshuhudia mabadiliko ya kasi katika takriban nyanja zote.

“Kutokana na imani hii, ipo haja kwa mwalimu kukumbatia matumizi ya mbinu za ufundishaji zitakazompa mwanafunzi nafasi murua ya kushiriki shughuli za ujifunzaji kikamilifu. Matumizi ya vifaa vya kidijitali yatachochea ubongo wa mwanafunzi uanze kufanya kazi,” anashauri.

Kubwa zaidi katika maazimio ya Allan ni kujiendeleza kitaaluma huku akipania kuweka hai ndoto za kuwa profesa wa Kiswahili na mhadhiri wa chuo kikuu.

Analenga pia kuzamia masuala ya uandishi wa fasihi ili kuendeleza kipaji cha utunzi wa kazi bunilizi ambacho anaamini kilianza kujikuza ndani yake tangu utotoni.

  • Tags

You can share this post!

Kampuni yazindua vitafunio vilivyosindikwa kwa nyama ya kuku

Juve Queens: Klabu yenye uwezo mkubwa wa kuinua talanta

T L