• Nairobi
  • Last Updated May 17th, 2024 10:50 AM
MWALIMU WA WIKI: Mwalimu stadi, mbunifu kazini

MWALIMU WA WIKI: Mwalimu stadi, mbunifu kazini

NA CHRIS ADUNGO

MWALIMU anapaswa kuwa na ufahamu mpana unaozidi ule wa wanafunzi wake. Ikitokea kwamba mwanafunzi anajua zaidi ya mwalimu wake, basi mwalimu huwa na ulazima wa kufanya utafiti wa kina katika somo analofundisha.

Mbali na kuwa mnyumbufu wakati wa kuandaa vipindi vya somo lake na mbunifu katika uwasilishaji wa kile anachokifundisha, mwalimu bora anastahili pia kuwa na ujuzi wa kutumia nyenzo mbalimbali za ufundishaji na kuelewa masuala yote muhimu yanayohusiana na mtaala.

Haya ni kwa mujibu wa Bi Gloria Lumiri ambaye sasa anafundisha katika shule ya msingi ya Holy Cross St James Dandora, Kaunti ya Nairobi.

“Mwalimu anastahili kuwa nadhifu na mwenye nidhamu. Awe mchangamfu, ajitume ipasavyo na atambue mahitaji ya wanafunzi wake. Awaelekeze kwa utaratibu unaofaa, awashajiishe na kuwatia moyo hata wasipofaulu vyema masomoni jinsi anavyotarajia,” anasema.

Gloria alilelewa katika eneo la Kapsabet, Kaunti ya Nandi.

Ndiye wa nne kuzaliwa katika familia ya watoto saba wa Bw Timothy Lumiri na marehemu Bi Wilfridah Lumiri.

Alianza safari ya elimu katika shule ya msingi ya Chepsonoi iliyoko Nandi (1999-2006) kabla ya kujiunga na shule ya upili ya Tigoi Girls, Kaunti ya Vihiga (2007-2010).

Japo matamanio yake yalikuwa kusomea udaktari, alihiari kujiunga na Chuo cha Mafunzo ya Ualimu cha Eregi katika Kaunti ya Kakamega (2011-2013).

Haja ya kujiendeleza kitaaluma ilimpa msukumo wa kujiunga na Chuo Kikuu cha Mount Kenya (MKU) kusomea shahada ya ualimu (Kiswahili/Dini) kuanzia mwaka wa 2020.

Zaidi ya Bi Kidiga na Bw Shivayanga waliompokeza malezi bora ya kiakademia shuleni Chepsonoi, mwingine aliyemwamshia hamu ya kuchapukia Kiswahili ni Bw Mirikau aliyemfundisha katika chuo cha Eregi.

“Walimu walikuwa watu wa kustahiwa sana katika jamii. Walikuwa wamepiga hatua kubwa kimaendeleo na walitegemewa mno kwa ushauri wa kila aina vijijini,” anasema.

Baada ya kuhitimu ualimu mnamo Agosti 2013, Gloria alipata kazi ya kufundisha katika shule ya msingi ya By Faith Junior jijini Nairobi.

Alihudumu huko hadi Disemba 2017 na akaamsha ari ya kuthaminiwa kwa Kiswahili miongoni mwa wanafunzi.

Amekuwa akifundisha Kiswahili pamoja na masomo ya Zaraa, Muziki na Kompyuta shuleni Holy Cross St James Dandora tangu Januari 2019.

Akijivunia tajriba ya miaka katika taaluma ya ualimu, Gloria anakiri kuwa mtaala wa umilisi (CBC) una nafasi kubwa ya kukuza na kulea vipaji vya wanafunzi kwa kuwa unaegemea zaidi uwezo wao katika fani mahsusi.

“Ni mpango unaoadilisha wanafunzi, kuwajengea msingi wa kukumbatia tamaduni za jamii mbalimbali na kuwachochea kutambua umuhimu wa kuwajibika na kujitegemea,” anaeleza.

Kwa mujibu wa Gloria, mwanafunzi akipata umilisi ufaao, atakuwa wa manufaa katika jamii ya sasa inayoshuhudia mabadiliko ya kasi katika takriban nyanja zote.

“Kutokana na imani hii, ipo haja kwa mwalimu kukumbatia matumizi ya mbinu zitakazompa mwanafunzi nafasi murua ya kutononoa vipaji vyake na majukwaa mwafaka ya kuchochea ubongo wake kufanya kazi,” anashauri.

“Pania kutambua vipaji vya wanafunzi wako huku ukiwahimiza pia wajitahidi masomoni kadri ya uwezo wao,” anaeleza mwalimu huyu ambaye pia ni msusi stadi.

  • Tags

You can share this post!

Wakenya kujua rais mpya

Macho yote yaelekezwa Bomas Wakenya wakisubiri kwa hamu...

T L