• Nairobi
  • Last Updated May 4th, 2024 10:15 PM
NASAHA: Hakikisho la kufanya vizuri ndicho kichocheo kwa mwanafunzi kufanya vyema

NASAHA: Hakikisho la kufanya vizuri ndicho kichocheo kwa mwanafunzi kufanya vyema

Na HENRY MOKUA

NILIKUWA nimekamilisha wasilisho langu tayari kuondoka Nasir aliponiwahi mlangoni na kushtakia angependa kusema nami faraghani.

Akiwa amesaza siku moja tu kabla ya kuanza mtihani wake wa kitaifa, sikuwa na budi kumsikiliza. Nilikisia kwamba huenda jambo alilotaka tulizungumzie lilikuwa la dharura na labda lilihusiana moja kwa moja na mtihani aliokuwa anajiandaa kuuanza. ‘Mwalimu! Nina msongo ajabu!’ Alishtakia.

Sikuhitaji kumhoji ndipo anitajie waziwazi kiini cha msongo wake. Jamaa zake hawajaridhishwa na alama yake ya 380/500. Wanadai, asipozoa angaa alama 400, ajipange kwani hapana atakayemwajibikia baada ya hapo!

Mbona wazazi wa siku hizi tumezidi kwa jeuri! Mwingine anapoomba bila kukoma mwanawe azoe angaa alama 250/500, wewe umejaliwa mwana wa kuzoa alama 380 na bado unateta! Wamwambia nini Muumba wa mwana huyo? Akuonjeshe hali ya kuwa na mtoto asiye mwepesi masomoni ili uone tofauti au watakaje! Mungu anataja waziwazi katika Matabu Matakatifu kwamba humthamini mnyenyekevu na kumchukia mwenye kiburi! Kabla hujaniuliza swali hilo ambalo naona linakuchoma, ati itakuwaje ikiwa mwana mwenyewe ana uwezo kiasi hicho…sikiliza nikuzindue kidogo.

Shinikizo ni mojawapo ya vianzo vya kudidimia kwa wanafunzi masomoni na kuwazia kujitoa uhai kwani huhisi kwamba hawana faida kwa wazazi wao na jamii nzima ikiwa hawazoi alama uzitakazo wewe!

Nasir ni kielelezo tu cha wanafunzi na watahiniwa wengi ambao nimekumbana nao wakidai wamechoshwa na kusukumwa na wazazi wao kuzoa alama zinazozidi uwezo wao. Badala ya kuyaboresha matokeo yao, hukata tamaa na kuanza kuyawazia mengine wanayoyamudu hata yatakayoyakiuka maadili ya jamii zao. Huanza kutafuta jambo la kuyavutia makini ya wanajamii. Nimewasikia wengine wakinongónezana kwamba wapo radhi kvunja hata sheria muradi waangaziwe kwenye vyombo vya habari.

Nisikilize ewe mzazi mwenzangu…tunachohitaji ni moyo wa shukrani. Huu ndio moyo aupendao Muumba wa mwanao. Unapomshu

kuru, anahisi kwamba unatambua baraka zake za sasa kwako na anakuwa radhi kukubariki na kuibariki familia yako hata zaidi. Hebu kakome kushawishiwa na mitazamo potovu ya wanajamii ambao wanajidai wanajua kumwekea kila yeyote matazamio. Wewe ni mtu binafsi na unatofautiana na kila yeyote ulimwenguni! Mwenyezi Mungu alivyomzindua Nabii wake Yeremia kwamba alimjua kabla ya kumuumba tumboni mwa mama yake na kumteua kuwa nabii kwa mataifa ndivyo afanyavyo na watoto wa vizazi vyote. Lipo kusudi mahususi au maalum ambalo kwalo Mungu alimuumba mwanao. Usije ukaiingilia mipango ya Mungu kwa kujitakia makuu!

Nilimpongeza Nasir na kumhakikishia kwamba akiendelea na bidii yake ambayo imemtuma kuzoa alama 380/500 azipatazo, atajiunga na shule ya upili ya ndoto zake, ikiwa atalifikilia lengo la jamaa zake au la! Isitoshe, atajiunga na chuo kikuu wakati wake utakapowadia na kuisomea taaluma aliyomtengea Mungu hata kabla hajamuumba.

Alitulia kwa namna ya kupigiwa mfano na kuuachia msongo aliokuwa nao. Sina shaka atakuwa miongoni mwa wanafunzi bora katika kaunti yake na kitaifa!

Ikiwa umewahi kumsukuma mwanao kuzoa alama inayozidi uwezo wake, hii ni fursa yako ya kuchukua hatua ya kijasiri na kumwomba msamaha. Msaidie kujitahidi kadri ya uwezo wake. Anapoibuka na alama moja mbili zaidi mpongeze badala ya kumfokea. Mhakikishie kwamba umetambua jitihada yake hiyo na upo radhi kumsaidia azidi kufanya vizuri.

Utakapoukumbatia moyo wa shukrani, moyo wa kutambua na kupongeza kila jitihada ndogo, utamwona mwanao akipaa taratibu hata akakiuka ile alama ambayo umekuwa ukimsukuma aizoe.

Hata asipoizoa muradi amefanya bidii kadri ya uwezo wake, njia yake itanyooka tu. Kila la heri unapochukua hatua hii ya kijasiri!

You can share this post!

GWIJI WA WIKI: Fatma Ali Mwinyi

KINA CHA FIKRA: Daima Magufuli atakumbukwa kwa uzalendo na...