• Nairobi
  • Last Updated April 27th, 2024 11:15 AM
DINI: Neema itakufuata unapopanda mbegu maishani mwako na hata kwa wengine

DINI: Neema itakufuata unapopanda mbegu maishani mwako na hata kwa wengine

Na PADRE FAUSTIN KAMUGISHA

UNAPOJAALIWA kuwa na vitu jua kwamba vimetokana na neema.

Neema ni mtego na unapoweka vitu katika nafasi yake, vitakuweka katika nafasi yako.

Kama una watu ni neema, unapowaweka katika nafasi zao, watakuweka katika nafasi yako.

Liwezekanalo ni neema lifanye leo. Leo ni mtego. Wamepanda mbegu ya neno ‘kesho’ na haijachipuka (Methali ya Arabia).

Mungu hatoi chochote kwa wale ambao wanakunja mikono yao daima. Chochote ni neema, Chochote ni mtego. Chochote bila chochote hupati chochote. Kuwa na macho ni neema yatumie kuona.

Mtu anaweza kuwa na macho, asione. Penye miti hakuna wajenzi. Neema ni mtego. Miti ni mtego.

Biblia yasema, “Kwa hiyo umezungukwa na mitego” (Ayubu 22:10).

Kama umezungukwa na neema. Umezungukwa na mitego. Kama umezungukwa na baraka umezungukwa na mitego. Kama umezungukwa na watu, umezungukwa na mitego.

Kama umezungukwa na fursa, umezungukwa na mitego. Kama umezungukwa na raslimali. Umezungukwa na mitego. Unaloweza kufanya ni mtego.

Mfuasi alienda kwenya hema la mwalimu wake wa kisufi amepanda ngamia.

Alishuka kutoka kwa ngamia na kwenda moja kwa moja kwenye hema na kuinama na kusema, “Imani yangu kwa Mungu ni kubwa, nimemwacha ngamia wangu nje hakufungwa, nikijua kuwa Mungu atalinda maslahi ya wale wampendao.”

Mwalimu wake alimwambia, “Wewe mpumbavu nenda umfunge ngamia. Mungu hawezi kusumbuliwa kukufanyia yale ambayo una uwezo wa kuyafanya kikamilifu.”

Kuwa na kichwa cha kufikiri ni mtego. Umiza kichwa kufatuta majibu ya maswali. Umiza kichwa kutegua vitendawili vya maisha.

Nilipokuwa Kidato cha Nne nilimtembelea mwalimu mkuu wangu ofisini saa mbili usiku. Huyu alikuwa mkuu wa seminari ndogo.

Baada ya kuniruhusu kuingia ofisini aliniambia, “Faustin naomba nifungulie dirisha mbu wanimalize.”

Niliona suala hili kuwa ni mtego sikufungua. Niliumiza kichwa. Siku nyingine mwalimu mkuu huyo ambaye alikuwa ni padre alikutana na baba mzazi wangu, na kumuuliza “Faustin akipiga chafya, unasema nini?”

Baba alisema, “Nasema kuwa uwe padre.” Baba aliwekewa mtego. Aliutegua. Mzazi anaweza kuwaambia watoto, “Natoka nje mkitaka pita kwenye lango mtoke nje majirani waseme nilizaa wazururaji.”

Mtu ni mtego. Tunasoma hivi katika Biblia, “Yesu akawaambia, Nabii hakosi heshima, isipokuwa katika nchi yake mwenyewe, na kwa jamaa zake, na nyumbani mwake.” (Marko 6:4).

Huko Nazareth Yesu alikosa heshima. Walimuona anachota maji, anachanja kuni. Hawakumpa heshima yake. Mtu anayeitwa Potenteni kijijini alipozaliwa utashangaa wanamuita Kapoti.

Hata akiisha kuwa mtu mkubwa bado kijijini wanamuita kapoti. Mtu ni mtego. Astahiliye heshima, mpe heshima. Kuna hata wanandoa ambao wakiishazoena wanachukuliana poa.

Joana alimuuliza mume wake Kerry, “Kwa nini kila mara ninapoimba unapitisha kichwa dirishani na kutazama nje? Bwana Kerry alijibu, “Nataka majirani wajue anayeimba vibaya si mimi.”

Bwana Kerry hakuweza kupongeza juhudi za mke wake za kuimba na hakuweza kumsifu.

Alimchukulia poa.Yesu aliheshimika sana Yerusalemu kwa vile akiwa na umri wa miaka kumi na miwili aliwaajabisha walimu hekaluni akiuliza maswali ya nguvu.

Yesu aliheshimika sana Kana alipobadili maji kuwa divai. Lakini Nazareti Yesu alikuwa Yesu. Nukta! Watu wa Nazareti walimchukulia poa. Hawakumthamini.

“Yeyote aliyekujua ukiwa mtoto mdogo hatakuheshimu ukiwa mkubwa.”

Ni methali ya Kiarabu.

Mtu akizoea kitu au mtu mwishowe haoni uzuri wake na umuhimu wake.

Mazoea huzaa upofu. Watu wa Nazareti walimzoea Yesu wakawa vipofu wa kutoona nguvu yake na uwezo wake.

Mwanamke anapoolewa huimbiwa nyimbo nzuri baada ya miaka kadhaa shemeji, mama mkwe na wifi kumzoea wanamgeuka, humtukana, humsengenya na kumpigia kelele.

Katika mazingira hayo mwanamke huyo hununua kanga au leso yenye maneno, “Leo Vigelele, Kesho Kelele.” Mazoea huleta kelele.

William James alibainisha, “Kanuni ya kina ya maumbile ya binadamu ni hamu ya kupongezwa.’ Mwenzi wako wa ndoa mwambie: “Asante” kila mara akifanya jambo zuri. Unapompongeza, mtazame na tabasamu. Msifie mwenzi wako mbele ya watu wengine.

You can share this post!

Akiri kuua mkewe kwa kuambiwa hajiwezi chumbani

Jinsi ya kuandaa makange ya kuku

T L