• Nairobi
  • Last Updated May 4th, 2024 8:46 PM
NGILA: Ajabu ya Wakenya kuzidi kujipeleka kichinjioni mitandaoni

NGILA: Ajabu ya Wakenya kuzidi kujipeleka kichinjioni mitandaoni

Na FAUSTINE NGILA

SIWAELEWI kabisa Wakenya. Iweje uporwe jana, leo na kesho na bado uko tayari kuwapa hela matapeli waliozoea kukunyang’anya?

Nilipouliza swali kwenye Facebook kuhusu aina na idadi ya apu za kidijitali zinazowapora Wakenya hela, nilipata majibu ya kushtua.

Kuna baadhi ya wananchi ambao baada ya kukubali hadaa ya kuwekeza hela zao kwenye majukwaa ambayo hatimaye hutoweka na hela hizo, bado wanasaka programu nyingine kupunjwa hela walizobaki nazo.

Yashangaza sana kuwa licha ya hali mbaya ya kiuchumi, wananchi wanatumia hela walizoweka kwa akiba kujaribu bahati katika uwekezaji ovyo.

Kisa na maana? Wanataka vya bwerere, maelfu ya pesa bila kutoa jasho.

Hawataki kuwekeza kwenye biashara halali ambapo wanalipia kodi na umeme, wanapendezwa na wezi wa mitandaoni wanaowadanganya kuwa wakitoa Sh5,000 watapata Sh10,000 baada ya wiki moja.

Progamu ya hivi majuzi imwekuwa Amazon Web Worker, ambayo ilitimua mbio na mamilioni ya Wakenya wenye mapato ya chini waliokopa hela za kuwekeza humo kwenye programu za dijitali.

Katika tafiti zangu, nimegundua kuwa kuna zaidi ya programu 30 ambazo zimeiba hela za wananchi bila kujali kwani tayari zinajua wateja wake wanaelewa biashara nzima ni uhuni.

Wengi wamesema kuwa wanaojiunga wa kwanza hunufaika pakubwa; ila pia wao wamejipata bila chochote baada ya apu hizi kuondoa hela zote, zikafunga akaunti na hata kung’oa apu kutoka kwenye Google Playstore.

Ingawa ni kweli janga la corona limeangusha riziki za watu wengi, kuwekeza kwa majukwaa chwara kama hayo ni upumbavu wa hali ya juu usio na suluhu.

Iweje mtu na akili yake timamu, kwa kuongozwa na tamaa ya kuwa tajiri chini ya mwezi mmoja anadaganywa kuwa akiwekeza Sh3,000 atakuwa akipata Sh1,000 kila siku na anakubali!

Kisha anaamua kuwekeza Sh9,000 ndipo apate Sh3,000 kila siku kisha baada ya siku nne anaona kuwa akaunti yake imezimwa.

Kwenye Facebook, wengi wamesema kuwa baada ya kuporwa hadi hata Sh100,000 wametimuliwa na malandilodi kwenye nyumba zao huku watoto wao wakikosa karo.

Licha ya serikali kuwaonya Wakenya dhidi ya walaghai kama hao, Wakenya hawaambiliki hawasemezeki; wanaendelea tu kufukuzia hela za kirahisi wakijua fika kuwa maelfu yao yanaweza kutokomea gizani.

Je, ungependa sasa serikali ikusaidie vipi iwapo wewe mwenyewe unajipeleka kichinjioni licha ya kuona wenzako wakitundikwa msalabani?

Hilo litumike kama funzo kuwa hakuna pesa zozote zijazo kwa urahisi; sharti utolee jasho pato lako hata kama ni dogo.

Ni muhimu kuridhika na kidogo unachotolea jasho kuliko kuhadaiwa kuwa utapata maelfu bila kusumbuka kisha ghafla unapoteza hata kidogo ulichokuwa nacho.

You can share this post!

KAMAU: BBI: Kimya cha makanisa kwa hakika chatamausha

AKILIMALI: Alipoteza vyote katika ghasia za 1992 ila sasa...