• Nairobi
  • Last Updated May 18th, 2024 11:39 AM
KAMAU: BBI: Kimya cha makanisa kwa hakika chatamausha

KAMAU: BBI: Kimya cha makanisa kwa hakika chatamausha

Na WANDERI KAMAU

KUNA wakati ambapo kanisa nchini lilikuwa mtetezi mkuu wa mwananchi.

Wakati huo, viongozi wa makanisa walionekana kama ‘wateule’ wa Mungu.

Waliitikisa serikali kutokana na ujasiri wao. Hawakutishwa na yeyote.

Hawakuwaona wanasiasa kama chemchemi ya kujipa utajiri au njia fupi ya kujifaidisha.

Ninazungumzia miaka ya themanini na tisini. Ninawarejelea viongozi kama marehemu maaskofu Alexander Muge, Henry Okullu, Ndingi Mwana a’Nzeki, David Gitari kati ya wengine.

Kwa kuwa waliongozwa na thamani ya uzalendo wa nchi, walifanya kila wawezalo kuyakabili maovu yote ya kiutawala yaliyokuwepo, hasa chini ya utawala dhalimu wa chama cha Kanu.

Vifo vya baadhi yao vilikuwa kama kafara kwa harakati zao za kukemea uongozi mbaya wa Kanu na ukatili ambao serikali ilikuwa ikiendesha dhidi ya wananchi.

Kwa mfano, Askofu Muge anadaiwa kuuawa na vikosi vya serikali kwa kumkosoa marehemu Daniel arap Moi kutokana na matamshi yake kuwa wakazi wa eneo la Pokot walikuwa wakikumbwa na baa la njaa.

Inaelezwa serikali iliona “kumwondoa” kama njia ifaayo zaidi ya kumyamazisha ili kutoendelea “kuwachochea wananchi” dhidi yake.

Upeo wa udhalimu wa utawala wa Kanu dhidi ya viongozi wa makanisa ulidhihirika Julai 7, 1990, wakati polisi waliponaswa kwenye video wakimpiga Askofu Mstaafu Timothy Njoya wa kanisa la PCEA kama mbwa, kwa kushiriki kwenye maandamano ya kushinikiza uwepo wa vyama vingi vya kisiasa.

Kwenye video hiyo ya kutamausha, Dkt Njoya anasikika akipiga kamsa, akiwarai polisi kumwacha.

Ingawa baadaye alitangaza kuwasamehe polisi hao, Dkt Njoya ni miongoni tu mwa viongozi ambao walishiriki kikamilifu kwenye harakati za ukombozi wa kisiasa nchini.

Hata hivyo, inasikitisha kuwa licha yao kuweka msingi thabiti kama huo katika utetezi wa haki na maslahi ya wananchi, viongozi wengi wa makanisa wamebaki kimya nchi inapoendelea kukumbwa na migogoro ya kiutawala.

Mfano mzuri ni utata uliopo nchini, kufuatia uamuzi wa Mahakama Kuu kutangaza mchakato wa Mpango wa Maridhiano (BBI) kuwa haramu na ulioendeshwa kinyume cha sheria.

Licha ya uamuzi huo kutishia kuzua migawanyiko ya kisiasa miongoni mwa raia na viongozi, makankisa yamebaki kimya.

Ni viongozi wa Kiislamu pekee ambao wamekuwa wakijitokeza kutoa misimamo na kauli zao mara kwa mara kwa masuala yanayowahusu kwenye mpango huo.

Taasisi muhimu kama vile Baraza la Kitaifa la Makanisa Kenya (NCCK) na Kongamano la Kitaifa la Maaskofu wa Kanisa Katoliki (KCCB) zimebaki kimya.

Mnamo Jumatatu, viongozi kadhaa waliodai kuiwakilisha NCCK walijitokeza na “kueleza msimamo wao” kuhusu BBI.

Kwenye taarifa yao, walijitolea kuwa “wapatanishi” kati ya serikali na Idara ya Mahakama ili kuondoa mkwamo huo.

Hata hivyo, kile walichosahau ni kuwa mzozo uliopo ni wa kisiasa na kikatiba, hivyo itayalazimu mashirika yoye ya kidini kujitokeza kueleza misimamo yao waziwazi badala ya kutapatapa bila mielekeo yao kubainika.

Ili kuendelea kudhihirisha umuhimu wake katika jamii kama ilivyokuwa awali, lazima makanisa yavunje kimya chao na kuchangia kwenye usuluhishaji wa utata uliopo kuhusu BBI.

[email protected]

You can share this post!

TAHARIRI: Koome aonyeshe hapokei maagizo

NGILA: Ajabu ya Wakenya kuzidi kujipeleka kichinjioni...