• Nairobi
  • Last Updated May 13th, 2024 7:55 AM
NGILA: Teknolojia itumike kukabili uchafuzi wa mazingira

NGILA: Teknolojia itumike kukabili uchafuzi wa mazingira

Na FAUSTINE NGILA

KATIKA majukwaa mengi mitandaoni, mjadala wa mabadiliko ya tabianchi, Waafrika wamekuwa wakikosoa mabara ya Amerika, Asia na Ulaya kwa kuchangia zaidi kwa uchafuzi wa mazingira.

Wamehoji kuwa mataifa ya mabara hayo yametumia kawi chafu katika kujiendeleza kiuchumi, kisha kuongoza ajenda ya kupunguza gesi hatari duniani na kuwekea Afrika presha.

Ingawa ni kweli kuwa Afrika pia yahitaji kujiendeleza kufikia viwango vya China, kwa mfano, wakati wa kutumia kawi chafu inayotoa gesi ya kabonidiosksidi umepita.

Hata hivyo, katika juhudi za kupunguza athari za mabadiliko ya tabianchi zinafaa kuongozwa na mataifa yanayochangia pakubwa katika kuchafua mazingira.

Wakati mwingi tunaposhuhudia mafuriko katika mataifa ya Afrika katika miaka ya hivi punde, huwa ni athari za uchafuzi wa mazingira, ambapo joto kwenye bahari na nchi kavu imepanda kupita kiasi na kusababisha mvua ya mafuriko.

Yanapochafua mazingira, uchafu huo hufika hadi katika anga ya Afrika ambapo sasa theluji katika milima ya Kilimanjaro na Kenya imeyeyuka. Hata hivyo, kwa juhudi za pamoja, bila kulaumiana kuhusu nani anachafua mazingira zaidi, dunia inaweza kupunguza athari hizi ambazo zimesababisha mioto ya kiajabu kule Amerika, Ureno na Australia.

Tayari katika tafiti zangu nimeona teknolojia kadhaa ambazo zinatumiwa kupunguza madhara haya, na iwapo mataifa yote yatajitolea kuzikumbatia, basi Mkataba wa Paris wa kuhakikisha joto haipandi kwa nyuzijoto 1.5 utafaa.

Kwa mfano, kampuni ya Climeworks nchini Uswisi inatumia teknolojia za kisasa kuondoa tani 900 za kabonidioksidi kila mwaka.

Baada ya kugundua kuwa saruji inachangia pakubwa katika kuongeza joto angani, kampuni ya Amerika Solidia sasa inatumia ubunifu kuunda saruji inayoondoa asilimia 30 ya gesi ya makaa katika ujenzi.

Pia, magari ya kielektroniki yasiyotumia dizeli au petroli yanazidi kuongezeka, hali ambayo inaweza kupunguza sana uchafuzi wa mazingira kutokana na uchukuzi.

Kwa sasa kuna magari milioni tano ya kielektroniki, lakini idadi hii yafaa kuongezwa zaidi, hasa kwa kubuni sera mwafaka kuyaleta barani Afrika bila vikwazo, na kuyauza kwa bei nafuu. Mbinu nyingine itakuwa kuwapa watu intaneti ya kasi ya juu kwa bei nafuu kuwawezesha kukoma kusafiri hadi kazini, na kufanyia kazi nyumbani, hali inayopunguza idadi ya magari yanayochafua hewa barabarani.

Hii inamaanisha bei ya simu za kisasa na kompyuta pia inafaa kupunguzwa, kupitia kuondolewa kwa ushuru unaotozwa bidhaa hizo zinaponunuliwa kutoka mataifa mengine.

Gesi ya methane, ambayo hutoboa wingu linalotukinga dhidi ya miale hatari ya jua, pia yafaa kupunguzwa. Utafiti unaonyesha kuwa gesi hii hutolewa na mifugo kama ng’ombe na mbuzi. Inamaanisha binadamu wanafaa sasa kujizoesha kula vyakula vya protini kama mahaharagwe ili kulinda mazingira.

Teknolojia ya roboti za kisasa zinazosafisha hewa katika miji pia yafaa kukumbatiwa kote duniani. Nimeona jijini Kampala kampuni ya Google ikishirikiana na vijana wabunifu kuweka mpango maalum wa kusafisha hewa kwenye bodaboda. Huu ni ubunifu unaofaa kusambazwa kote ulimwenguni.

Lakini kwa haya yote kufanikiwa, mataifa yote duniani yanafaa kukubaliana kupunguza uchafuzi wa mazingira, na kuunda mkataba unaotoa adhabu kwa mataifa yanayokiuka kanuni za kuhakikisha sayari hii itakuwa pahali salama kwa vizazi vijavyo.

You can share this post!

Mwanamke auawa kwa kunyongwa Ruiru mpenzi wa kiume akiwa...

GWIJI WA WIKI: Dkt Beverlyne Asiko Ambuyo