• Nairobi
  • Last Updated May 8th, 2024 5:20 PM
Mwanamke auawa kwa kunyongwa Ruiru mpenzi wa kiume akiwa mshukiwa

Mwanamke auawa kwa kunyongwa Ruiru mpenzi wa kiume akiwa mshukiwa

Na LAWRENCE ONGARO

HOFU ilitanda katika kijiji cha Kambi Moto mjini Ruiru, Kaunti ya Kiambu baada ya mwanamke kwa kunyongwa, mshukiwa akiwa ni mpenzi wake wa kiume.

Majirani walisema uvundo mkali ulishuhudiwa kwa siku mbili mfululizo baada ya kuvutiwa na nzi waliotoka ndani ya nyumba ya mshukiwa wa mauaji.

Kamanda mkuu wa polisi kaunti ndogo ya Ruiru, Bw Phineas Ringera alisema majirani ndio waliogundua uvundo kwenye nyumba hiyo na baadaye wakapiga ripoti kwa kituo cha polisi cha Ruiru.

Alisema majirani walidai ya kwamba mshukiwa aliishi na maiti nyumbani kwa siku mbili mfululizo kabla ya wao kugundua maiti hiyo.

Ilidaiwa wawili hao waliishi pamoja kama wapenzi lakini walitofautiana kutokana na maswala ya mapenzi.

Alisema mshukiwa huyo alimnyonga marehemu halafu akamfunika ndani ya karatasi kubwa ya nailoni huku akimficha mvunguni mwa kitanda.

Alizidi kueleza ya kwamba kwa wiki chache zilizopita visa vya watu kuuana vimezidi Juja na Ruiru, huku ikionekana ni shida nyingi za kijamii.

Polisi waliondoa mwili huo chumbani na kuupeleka katika chumba cha kuhifadhi maiti cha General Kago katika hospitali ya Thika Level 5.

Mshukiwa ataendelea kuhojiwa huku akingojea kufikishwa katika mahakama ya Ruiru kujibu mashtaka ya mauaji.

Bi Zaitun Wanjiru ambaye ni jirani wa mshukiwa aliwashauri wasichana kuwa makini wanapofanya mahusiano na wanaume marafiki wao.

“Ningetaka kuwashauri wasichana kuwa makini wakiwa na wanaume,” alisema Bi Wanjiru.

Naye Bi Mary Kibathi aliwashauri wapenzi wanaoishi pamoja kuheshimiana na iwapo hawaelewani ni vyema kuachana kwa amani.

Tukio hilo limeacha wakazi wengi wa Ruiru na mshangao huku wakiendelea kutafakari na kujiuliza maswala mengi kuhusu vifo vya kila mara.

You can share this post!

WASONGA: Uteuzi wa makamishna wapya wa IEBC uwe na uwazi

NGILA: Teknolojia itumike kukabili uchafuzi wa mazingira