• Nairobi
  • Last Updated May 2nd, 2024 8:55 PM
NGILA: Vijana msilaze bongo, mamilioni yawasubiri!

NGILA: Vijana msilaze bongo, mamilioni yawasubiri!

Na FAUSTINE NGILA

SI wakati wote wa kulia na kushinda ukilalamika jinsi ambavyo uchumi umekuathiri, jinsi ambavyo kampuni zimetimua wafanyakazi, jinsi ambavyo ufisadi umekuzuia kupata ajira na jinsi ambavyo sera hasi za serikali zimekufungia kuanzisha biashara.

Kama Mkenya, una nafasi ya kuonyesha si wananchi wenzako tu bali bali pia ulimwengu mzima jinsi unavyoweza kutumia nafasi ndogo uliyo nayo kuunda suluhu kwa mamia ya matatizo.

Nasema hivi kwa kuwa vijana wengi wamejificha kwenye kisingizio cha jinsi uchumi umepata pigo kutokana na janga la corona. Wasichojua ni kuwa katika lindi hilo la changamoto, ndipo kuna nafasi.

Binafsi, wiki iliyopita nilikutana na kundi la vijana katika vyuo vikuu vya humu nchini ambao wamejitokeza kutatua shida ya ukosefu wa mfumo wa kuwapa wateja bei mbalimbali katika maduka tofauti.

Nikiwahoji vijana hao ambao wameunda mfumo kwa jina ‘Bei ya Ukweli’, nilipata mfano mwingine wa jinsi unavyoweza kutumia akili zako kwa manufaa ya jamii, na kujiajiri huku ukifungua nafasi za kazi kwa mamia ya wenzako.

Mfumo wao, tofauti na asasi za serikali ambazo zimewaacha Wakenya kupunjwa na wanafanyabiashara walafi, unawalinda raia dhidi ya kulipa maradufu kwa baadhi ya bidhaa zinazouzwa. Unawasaidia kujua ni wapi kuna bei nafuu.

Mahojiano zaidi yalifichua kuwa, mradi wao huo haukuhitaji hata fedha zozote kama mtaji. Walianza tu kukusanya bei za bidhaa tofauti katika maduka mbalimbali na kuchanganua data hiyo kisha kuiweka katika mitandao ya kijamii ya Twitter, Facebook na Instagram.

Juhudi zao zilitambuliwa na wafadhili na sasa wana mamilioni ya pesa kutokana na ubunifu wao huo, huku wafuasi wao mitandaoni nao wakisema kuwa wako tayari kulipa Sh50 kwa kila ripoti. Kwa wafuasi 100,000 kati ya 500,000 wanaolipa, hizo ni hela ngapi?

Mbona umekaa tu kuisubiri serikali, wazazi, marafiki au mashirika yasiyo ya kijamii kukupa ajira? Wengine wanalia kuwa kampuni wanazofanyia kazi haziwalipi mshahara wa maana. Nani amekukataza kuanzisha mradi usio wa hela nyingi kutatua matatizo tuliyo nayo kwa jamii?

Nimetembea katika kaunti nyingi humu nchini na kugundua kuwa vijana wengi wanataka vitu vya bwerere, rahisi tu bila kutoa jasho. Huo ni uzembe.

Jitokeze. Fanya utafiti wako polepole. Tambua huduma ambazo zimekuwa ghali au hazipo kabisa na zinahitajika kwa wingi na wananchi. Kisha fikiria suluhu tosha kukabiliana na kisiki hicho. Kwa chini ya miezi sita, utakuwa na pesa zako za maana, na utasaidia pakubwa kupunguza ukosefu wa kazi nchini.

Usiwe tu mtu wa kusaidiwa wakati wote. Pia wewe, onyesha ulimwengu kuwa Mola alikujalia akili ya kufikiria mambo muhimu yanayoweza kusaidia wengine.

Usiwape wazazi na marafiki presha ukiwauliza kila siku ni lini watakutafutia kazi, huo ni ubaradhuli. Jiamini mwenyewe, tumia ulicho nacho kuanza, wafadhili wakishaona kazi yako watakupiga jeki.

Naomba nikupe siri. Kuna mamilioni ya pesa yanayosubiri kufadhili miradi ya kidijitali yenye uwezo mkuu. Kwa sasa yanamilikiwa na kampuni, mashirika na hata watu binafsi, lakini katika muda wa miezi michache ijayo, yanaweza kuwa yako.

You can share this post!

WASONGA: Malumbano makali kati ya vigogo wa Nasa, Raila...

Walioenda kulipa mahari walimwa faini