• Nairobi
  • Last Updated May 6th, 2024 1:13 PM
WASONGA: Malumbano makali kati ya vigogo wa Nasa, Raila hayafai

WASONGA: Malumbano makali kati ya vigogo wa Nasa, Raila hayafai

Na CHARLES WASONGA

MALUMBANO yanayoendelea miongoni mwa waliokuwa vinara wa muungano wa upinzani, NASA, kuhusu nani anafaa kuidhinisha nani katika kinyang’anyiro cha urais 2022 hayafai, kwani yanaweza kuchochea uhasama miongoni mwa wafuasi.

Malumbano hayo hayana mantiki yoyote kwa sababu, kimsingi, Wakenya ndio wana usemi na uwezo wa kuamua mgombea urais ambaye anafaa kuwa Rais wao wa tano baada ya Rais Uhuru Kenyatta kustaafu Agosti 2022.

Kwa hivyo, haikuwa na maana kwa kiongozi wa Amani National Congress (ANC) Musalia Mudavadi na wenzake Kalonzo Musyoka (Wiper) na Moses Wetang’ula kudai juzi kuwa kiongozi wa ODM Raila Odinga anapaswa kuunga mkono mmoja wao aingie Ikulu 2022.

Wakiendesha kampeni katika maeneo bunge ya Matungu na Kabuchai, watatu hao walidai kuwa wamemuunga mkono Bw Odinga kwa jumla ya miaka 30 na sasa ni wakati wake “kurudisha mkono” kwa kuunga mgombeaji urais wa muungano wao ambao hawajamtaja.

Waziri huyo mkuu wa zamani aliwajibu kwa kubainisha wazi kwamba hataunga mkono yeyote miongoni mwa watatu hao kwa sababu walimtelekeza alipojiapisha kama Rais wa Wananchi mnamo Januari 30, 2018 katika uwanja wa Uhuru Park, Nairobi.

Inadaiwa kuwa kulikuwa na mkataba wa maelewano (MOU) miongoni mwa vinara wa NASA kuelekea uchaguzi mkuu wa 2017 kwamba Bw Odinga angeongoza mwa miaka mitano kisha ampishe Bw Musyoka mwaka wa 2022. Hii ni endapo NASA ingeshinda katika uchaguzi huo.

Nadhani MOU hiyo sasa haina maana kwa sababu Bw Odinga hakufaulu kuingia Ikulu 2017.

Kwa hivyo, Mabw Mudavadi, Musyoka na Wetang’ula hawafai kurejesha suala hilo katika kampeni zao za urais kuelekea uchaguzi mkuu ujao.

Kile watatu hao wanafaa kufanya, kwa haraka, ni kutaja mgombeaji wa urais wa muungano wao unaojulikana kama “Sacred Alliance.”

Kisha waanzishe kampeni kabambe kote nchini kuuza sera zao kwa wananchi na kuelezea kwani ni mgombeaji wao anafaa kupewa nafasi ya kuingia Ikulu na wala sio Naibu Rais William Ruto, Bw Odinga au wagombeaji wengine watakaochipuza.

Tayari Bw Odinga ametangaza kuwa chama chake kitabuni muungano na mrengo wa Jubilee unaoongozwa na Rais Kenyatta.

Kando na hayo, juzi alikutana na Gavana wa Makueni Kivutha Kibwana na aliyekuwa Katibu Mkuu wa Shirika la Umoja wa Mataifa kuhusu Biashara na Maendeleo (UNCTAD) Mukhisa Kituyi, ishara kwamba anapania kuwashirikisha katika muungano huo.

Wito wangu kwa Mabw Mudavadi, Musyoka na Wetang’ula ni kwamba watumie muda wao mwingi kujiandaa kwa uchaguzi mkuu wa 2022 na wakome kurushiana cheche na Bw Odinga na Dkt Ruto. Watakuwa wakichochea uhasama nchini na hivyo kuyeyusha sifa zao za kuwa “wanasiasa wangwana.”

You can share this post!

Wito serikali isiingize nchi kwa madeni zaidi

NGILA: Vijana msilaze bongo, mamilioni yawasubiri!