• Nairobi
  • Last Updated May 17th, 2024 12:48 PM
NGUVU ZA HOJA: Serikali ichukue hatua kuupa urasmi wa Kiswahili maana

NGUVU ZA HOJA: Serikali ichukue hatua kuupa urasmi wa Kiswahili maana

NA PROF JOHN KOBIA

KATIBA ya Kenya ya 2010 katika ibara ya 7 sehemu ya 3 inaweka wazi kuwa lugha rasmi za Jamhuri ya Kenya ni Kiswahili na Kiingereza.

Mpaka sasa urasmi wa Kiswahili umebaki tu kwenye tamko la Katiba.

Serikali ya Kenya ina wajibu wa kikatiba kuhakikisha kuwa Kiswahili kinapewa urasmi unaostahili.

Serikali inapaswa kufanya juhudi za kimaksudi ili kuimarisha urasmi wa Kiswahili katika nyanja zote za kiserikali.

Mojawapo ya juhudi hizi ni kubuniwa kwa Baraza la Kiswahili la Kenya. Hili ni jukumu la serikali kupitia Wizara ya Utamaduni.

Wasomi na wakereketwa wa Kiswahili wamekuwa wakishinikiza uundwaji wa baraza la Kiswahili kwa miaka mingi.

Kwa upande wake, serikali imekuwa ikitoa ahadi zisizo na kikomo kuhusu kuundwa kwa baraza la Kiswahili. Bado kuna matumaini. Tusife moyo.

Tunatarajia serikali ya awamu ya tano itashughulikia suala la kuundwa kwa Baraza la Kiswahili la Kenya kwa dharura, uzito na umuhimu unaostahili.

Baraza litakuwa na jukumu muhimu katika kufanikisha tafsiri na ukalimani. Hivi karibuni, Wakenya watakuwa wakifuatilia kwa makini kesi ya uchaguzi iliyowasilishwa katika mahakama ya upeo nchini. Lugha itakayotumiwa katika mahakama hiyo ni Kiingereza. Bila ukalimani, huenda Wakenya wengi wasielewe yatakayoendelea katika mahakama hiyo.

Tunahitaji vitendo zaidi kuliko maneno kuhusu uundwaji wa Baraza la Kiswahili. Wakereketwa wa Kiswahili wanahitaji kubuni mbinu mpya za kushughulikia suala hili.

Tunapongeza uongozi wa Bunge la Kitaifa kwa hatua ya kimaksudi kwamba Kanuni za Kudumu za Bunge la Taifa zilitafsiriwa kwa Kiswahili.

Ili lugha ya Kiswahili iwe lugha rasmi ya kweli; sheria, miswada na nyaraka zote za kiserikali zinapaswa kutafsiriwa kwa Kiswahili.

  • Tags

You can share this post!

VALENTINE OBARA: Pwani bado haijathamini wanawake kama...

VYAMA: Chama cha Kiswahili katika shule ya msingi ya...

T L