• Nairobi
  • Last Updated May 17th, 2024 12:48 PM
VYAMA: Chama cha Kiswahili katika shule ya msingi ya Kinderworld Academy

VYAMA: Chama cha Kiswahili katika shule ya msingi ya Kinderworld Academy

NA CHRIS ADUNGO

CHAMA cha Kiswahili katika shule ya msingi ya Kinderworld Academy iliyoko South C jijini Nairobi, hushughulikia mahitaji ya wanafunzi wenye ari ya kuzamia uanahabari na fani nyingine zinazofungamana na lugha.

Chama kilichoasisiwa na Bw Daniel Mwai mnamo 2014, kilipata mwamko mpya 2017 chini ya ulezi wa mwalimu Nicholas Kilonzo.

Kufikia sasa, chama kinajivunia zaidi ya wanachama sitini ambao ni wanafunzi kuanzia gredi ya nne hadi darasa la saba.

Viongozi wa chama ni Hassan Mohamed (Mwenyekiti), Mohamed Salat (Naibu Mwenyekiti), Salim Ahmed (Katibu) na Suhaib Abdikarim (Mhazini). Wao hushirikiana kwa karibu na wawakilishi wa madarasa kuratibu shughuli za chama.

Mbali na kuzamia masuala ya utafiti, wanachama hukusanya habari za matukio mbalimbali shuleni, kuzihariri na kuziwasilisha gwarideni kwa Kiswahili.

Malengo mengine ya chama ni kupiga jeki shughuli za Idara ya Lugha ili kuboresha matokeo ya mitihani; na kuwapa wanafunzi majukwaa mwafaka zaidi ya kukuza na kulea vipaji vyao katika sanaa mbalimbali – ulumbi, uimbaji, utunzi wa mashairi na uandishi wa hadithi.

Wanachama hukutana kila Ijumaa kuanzia saa nane mchana hadi saa kumi alasiri ili kuratibu mijadala mbalimbali na kutathmini maendeleo na mwelekeo wa chama.

Vikao hivi pia huwapa wanafunzi fursa za kushughulikia masuala ya kiakademia kwa kuzamia mada zinazowatatiza.

Shughuli zote za chama zinakusudia kukuza Kiswahili, kuwatia wanafunzi mshawasha wa kuthamini masomo ya lugha na kuimarisha viwango vya ufundishaji na ujifunzaji wa stadi kuu za kusikiliza, kuzungumza, kusoma na kuandika.

Kauli mbiu ya chama ni ‘Kiswahili umoja wetu, Kiswahili utamaduni wetu’.

Zaidi ya Bw Kilonzo, walimu wengine wanaosukuma gurudumu la Kiswahili ni Bw Patrick, Bw Edwin, Bw Fredrick, Bw Jibril, Bi Mildred, Bw Wandera na Bi Margaret.

  • Tags

You can share this post!

NGUVU ZA HOJA: Serikali ichukue hatua kuupa urasmi wa...

GWIJI WA WIKI: Ryan Mwenda

T L