• Nairobi
  • Last Updated May 9th, 2024 6:40 PM
NJENJE: Wakulima kupewa mbegu za GMO bila malipo mwaka 2023

NJENJE: Wakulima kupewa mbegu za GMO bila malipo mwaka 2023

NA WANDERI KAMAU 

WAKULIMA nchini watapata mbegu za vyakula vilivyotengenezwa kisayansi (GMOs) kuanzia mwaka ujao, Kenya inapojitayarisha kukumbatia ukulima wa vyakula hivyo.

Serikali imesema inapanga kutumia zaidi ya ekari nusu milioni kwa kilimo cha mazao hayo, katika msimu wa mvua ya masika kati ya Machi na Mei.

Kulingana na Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Utafiti kuhusu Kilimo na Ufugaji (Karlo), Dkt Eliud Kireger, shirika hilo litakuwa likitoa mbegu za mazao hayo bila malipo kwa wakulima wakati wa msimu huo.

Hilo linafuatia kuondolewa kwa marufuku ya mazao hayo nchini na Baraza la Mawaziri mapema mwezi huu wa Oktoba.

Mwelekeo huo sasa umetoa nafasi kwa mashirika makubwa ya kilimo kuagiza mazao hayo kutoka mataifa ya nje.

Uagizaji wa mazao hayo ulipigwa marufuku na serikali ya Rais Mstaafu Mwai Kibaki mnamo 2012, baada ya hofu kuibuka kuhusu athari za kiafya kwa matumizi yake kwa mwanadamu.

Dkt Kireger alisema kuwa kando na wakulima, watakuwa wakitoa mbegu za mazao hayo kwa mashirika yanayohusika katika utengenezaji na uboreshaji wa mbegu hizo.

Alisema baadhi ya mbegu zitakazoboreshwa na mashirika hayo zitauziwa wakulima.

“Kijumla, tumepanga kulima hadi ekari 500,000 kama hatua ya kwanza ya kukabili tatizo la uhaba wa chakula nchini,” akasema mkurugenzi huyo.

Hii itakuwa mara ya kwanza nchini kwa wakulima kuendesha kilimo cha mazao hayo kwa njia ya wazi.

Hapo awali, kilimo cha mazao hayo kilikuwa kikiendeshwa na mashirika ya utafiti wa kilimo kwa kiwango kidogo tu.

Mnamo Oktoba 3, Rais William Ruto aliondoa marufuku dhidi ya ukuzaji na uagizaji wa mazao hayo baada ya majaribio yaliyodumu kwa miaka kumi.

Majaribio hayo yamekuwa yakiendeshwa na wanasayansi wa masuala ya kilimo nchini.

Hata hivyo, hatua hiyo imezua ukosoaji mkubwa kutoka kwa mashirika ya kutetea haki za umma.

Katika kuondoa marufuku hiyo, Rais Ruto alisema kuwa njia ya pekee ya kukabili uhaba wa chakula nchini ni kurejesha kilimo cha mazao hayo.

  • Tags

You can share this post!

UJASIRIAMALI: Anahesabu mabunda ya noti kwa kuunda vinyago...

Kipchoge atuzwa kuwa mwanaspoti bora wa Septemba

T L