• Nairobi
  • Last Updated May 9th, 2024 5:50 AM
UJASIRIAMALI: Anahesabu mabunda ya noti kwa kuunda vinyago vya kipekee

UJASIRIAMALI: Anahesabu mabunda ya noti kwa kuunda vinyago vya kipekee

NA CHARLES ONGADI

KATIKA kituo cha kibiashara cha Mtwapa, Kaunti ya Kilifi kwenye barabara kuu ya Mombasa kuelekea Malindi, kuna vinyago vya aina yake, vinavyovutia macho ya wengi.

Hapa, Damasio Alberto Ntumuke,55, ambaye ni raia wa Msumbiji yuko kwenye mishemishe katika karakana yake akichonga vinyago.

Ni viti vilivyochongwa kwa ustadi mkubwa mfano wa makalio ya mwanamke mrembo na ambavyo vimevutia wapita njia hasa watalii wanaozuru mji wa Mtwapa.

“Nilipozuru mji wa Mtwapa kwa mara ya kwanza mwaka wa 1992 nilifurahishwa jinsi akina dada hapa walivyowavutia mno watalii kutoka ughaibuni wanaozuru mji huu. Nikapiga bongo jinsi ninavyoweza kujipatia riziki kutokana na urembo wa akina dada hawa pasina kujihusisha moja kwa moja nao ndipo nikafikia uamuzi wa kuchonga viti hivi maalum ,” aeleza Ntumuke wakati wa mahojiano na Akilimali majuzi.

Kulingana na Ntumuke, alijifunza uchongaji vinyago kutoka kwa baba yake akiwa na umri wa miaka 11 pekee. Baba yake alikuwa fundi stadi wa kuchonga aina mbali mbali za vinyago zikiwemo barakoa zinazotumika wakati wa kucheza ngoma za kitamaduni za Wamakonde.

Mara baada ya kufungua karakana yake pembezoni mwa barabara hiyo mkabala na hoteli ya Casuarina, wateja wengi walianza kumiminika kuona aina hizi za viti.

Ntumuke anaiambia Akilimali kwamba anauza kiti kimoja kwa kati ya Ksh350,000 hadi Ksh400,000 kulingana na msimu.

“Mara nyingi wateja wangu ni wazungu ama wafanyibiashara wenye hoteli kubwa za kitalii hapa Pwani na hata baadhi ya wananchi wa kawaida wanaopendezwa na viti hivi,” asimulia Ntumuke.

Mbali na kuchonga viti hivi vya kuvutia pia Ntumuke, anachonga vinyago vya aina tofauti ya wanyama na hata shanga.

Humchukua takriban mwezi mmoja kuchonga kiti kimoja.

Aidha, anakiri kupata miti spesheli ya kutumia kuchonga aina hizi za viti ndio changamoto kuu inayomkabili katika kazi yake.

“Ili kupata kiti cha kudumu na kuvutia, hutumia miti aina ya Mvule ama Mwarubaine ambayo ni nadra kupatikana,” asema fundi huyu stadi.

Aghalabu Ntumuke anasema hupata miti hiyo kutoka nchi jirani ya Tanzania na maeneo mengine nchini jambo analosema humgharimu kiasi kikubwa cha hela.

Hata hivyo, Ntumuke anafichua mbali na biashara yake ya viti hivi maalum na shanga pia, anajipatia hela kutoka kwa wageni wanaozuru mji wa Mtwapa kwa kupiga picha na viti hivi.

Kwa wapita njia wanaotaka kupiga picha na vinyago hivi hutoza Ksh100 pekee ambapo msimu mzuri anaweza kuvuna Ksh2,000 ama Ksh3,000 na hasa kunapokuwa na semina za kitaifa katika kaunti za Mombasa na Kilifi.

Katika hatua ya kurudisha mkono kwa jamii, Ntumuke amekuwa akiwafundisha vijana namna ya kuchonga aina mbali mbali ya vinyago vya kuvutia katika karakana yake.

Anawashauri vijana kuwa wabunifu kwa kufikiria njia ya kujipatia riziki bila kutumia njia ya mkato.

“Vijana wajiajiri badala ya kutegemea kazi ya kuajiriwa ambazo ni nadra kupata kutokana na idadi kubwa ya vijana wanaomaliza masomo yao kila mwaka,” anasema.

  • Tags

You can share this post!

MITAMBO: Mashini kusaidia kilimo endelevu kulinda mazingira

NJENJE: Wakulima kupewa mbegu za GMO bila malipo mwaka 2023

T L