• Nairobi
  • Last Updated May 17th, 2024 6:50 AM
Jinsi ya kuandaa katlesi za kuku

Jinsi ya kuandaa katlesi za kuku

Na MARGARET MAINA

[email protected]

Walaji : 3

Kuandaa kuku unahitaji

  • kuku kilo ½ bila ngozi na mifupa
  • juisi ya ndimu
  • chumvi
  • pilipili

Vinavyohitajika ili kuandaa katlesi

  • mafuta ya kupikia vijiko 3
  • viazi 4
  • kitunguu maji kilichokatwakatwa
  • kitunguu saumu kilichotwangwa kiasi cha kijiko 1
  • tangawizi iliyotwangwa kijiko ½
  • binzari kijiko 1
  • pilipili mbichi iliyokatwa vipande vidogovidogo
  • manjano kijiko ½
  • giligilani ya unga kijiko ½
  • poda ya curry kijiko ½
  • mayai 2; piga tia katika bakuli
  • chenga za mkate kiasi; tia katika sahani

Maelekezo

Weka mnofu wa kuku pamoja na vitu vingine katika sufuria ili uchemshe mekoni kama kawaida ili nyama iive vizuri.

Chemsha viazi kwa chumvi kiasi kisha chuja maji yote na uviponde.

Nyambue kuku kupata vipande vidogovidogo. Unaweza ukasaga pia kwa blenda ya vitu vikavu ukitaka kazi yako iwe rahisi.

Mimina mafuta ya kupikia kwenye sufuria mekoni na yakishapata moto, tia vitunguu na kaanga hadi vianze kupata rangi ya kahawia.

Tia tangawizi na saumu pamoja na maji kidogo kisha kaanga kwa dakika tatu.

Tia manjano na chumvi kiasi halafu koroga vizuri kisha tia kuku na kaanga tena kwa dakika mbili. Baada ya hapo, tia viazi vyako ulivyoponda na uchanganye vizuri.

Tia viungo vilivyobaki kisha koroga vizuri. Onja ujue kama chumvi ni ya kutosha au unatakikana kuiongeza.

Epua na acha mchanganyiko upoe.

Chota mchanganyiko wako na ufanye maduara kisha taratibu binya kwa kiganja chako na ufinye. Panga katika sahani. (Unaweza fanya shepu yoyote)

Mimina mafuta katika sufuria iliyo mekoni na mafuta yakipata moto, chovya katlesi katika mayai kisha zungusha katika chenga za mkate na tia katika mafuta moto.

Kaanga hadi zipate rangi ya kahawia pande zote mbili.

Epua katika chujio zichuje mafuta. Pakua na ufurahie.

You can share this post!

Watu wawili wauawa Lamu genge hatari likitekeleza unyama...

Okutoyi awasili Australia tayari kwa mashindano mawili ya...

T L