• Nairobi
  • Last Updated May 2nd, 2024 12:09 PM
Watu wawili wauawa Lamu genge hatari likitekeleza unyama vijijini

Watu wawili wauawa Lamu genge hatari likitekeleza unyama vijijini

NA KALUME KAZUNGU

WATU wawili wameuawa kwa kupigwa risasi na pia kukatwa kwa mapanga na majangili waliovamia vijiji vya Juhudi, Marafa na Ukumbi katika tarafa ya Mpeketoni, Kaunti ya Lamu, Jumapili jioni.

Wahalifu hao pia waliteketeza nyumba kadhaa.

Kulingana na walioshuhudia uvamizi huo, genge la wahalifu waliokuwa wamejihami kwa silaha hatari, ikiwemo bunduki na mapanga, walifika vijijini mwao majira ya saa kumi na moja na nusu jioni ya Jumapili, hivyo kuwafanya wakazi kujitoma msituni kwa usalama wao.

Katika harakati hizo, wazee wawili walipigwa risasi na kuuawa na kisha kukatwa vidole na mikono na wavamizi hao ambao baadaye walitorokea msituni.

Wahalifu hao pia wanaripotiwa kuiba vyakula na kuharibu televisheni na vifaa vingine vya nyumbani na hata kuchoma nyumba kabla ya kutorokea msituni.

Maafisa wa usalama walifika mar moja kwenye eneo la shambulio,ambapo makabiliano makali ya risasi yalizuka kabla ya kuwatokomeza majangili hao msituni.

Afisa wa utawala wa maeneo husika aliyezungumza na Taifa Leo na kudinda kutaja jina lake alisema hali ya taharuki imetanda kwa sasa kwenye vijiji vya Juhudi, Marafa, Ukumbi, Salama na viungani mwake, hivyo kuwasukuma wakazi kutorokea kwenye maeneo ya Majembeni na Kibaoni.

“Baada ya wazee wawili kuuawa na wavamizi, wakazi hapa hawakulala. Walitoroka hadi katika miji ya Majembeni na Kibaoni ambako walilala huko. Wengi wana wasiwasi wa kulengwa na kumalizwa na wahalifu. Serikali ifanye jambo,” akasema afisa huyo.

Jumatatu, maandamano ya wakazi wenye ghadhabu yalishuhudiwa kwenye miji ya Kibaoni na Majembeni kuishinikiza serikali kuhakikisha usalama wa wananchi unadhibitiwa.

Taifa Leo ilishuhudia waandamanaji wakichoma magurudumu na hata kuziba barabara kwa mawe, hivyo kutatiza shughuli za usafiri.

Ililazimu maafisa wa polisi kupelekwa kwenye maeneo hayo ya Kibaoni na Majembeni na kuwatawanya waandamanaji na kuruhusu shughuli za usafiri kuendelea.

“Sisi tutaendelea kuandamana hadi pale serikali itakapomaliza hawa wahalifu. Leo kuna wazee wameuawa kinyama. Juzi kuna wengine pia waliuawa. Tutaendelea kushuhudia maafa haya hadi lini? Tumechoka,” akasema Bw Simon Mwangi.

Mauaji ya watu wawili eneo la Juhudi na Marafa, Jumapili jioni pia imechangia wanafunzi kukosa kufika shuleni kuendelea na masomo.

Jumatatu, shule ya msingi ya Juhudi haikuwa na mwanafunzi hata mmoja kwani wazazi walikuwa wameroka vijijini na watoto wao na kulala mjini Kibaoni.

Katika mahojiano na Taifa Leo kwa njia ya simu, Mshirikishi wa Usalama, Ukanda wa Pwani, John Elungata alithibitisha mauaji ya watu wawili Lamu lakini akasisitiza kuwa usalama umedhibitiwa vilivyo.

“Ni kweli watu wawili waliuawa kwenye uvamizi eneo la Juhudi. Waliuawa wakijaribu kutoroka wahalifu. Hata hivyo walinda usalama wamegundua mwanya uliokuwepo na ambao wahalifu wamekuwa wakitumia kushambulia vijiji vya Lamu. Maafisa wa polisi na wanajeshi wamesambazwa maeneo hayo na hakutashuhudiwa mauaji au uvamizi tena kama ilivyokuwa ikishuhudiwa,” akasema Bw Elungata.

Mauaji hayo yanajiri saa chache tu baada ya Bw Elungata kuandaa kikao na wakuu wa usalama Lamu, viongozi na machifu Jumapili.

Mauaji ya Jumapili pia yanajiri siku chache baada ya watu wengine 11, wakiwemo maafisa wa polisi wa GSU kuuawa kwenye uvamizi katika kipindi cha juma moja lililopita.

You can share this post!

TAHARIRI: Kuhubiri chuki ya kisiasa tishio kwa taifa kabla...

Jinsi ya kuandaa katlesi za kuku

T L