• Nairobi
  • Last Updated May 10th, 2024 7:50 AM
BAHARI YA MAPENZI: Ndoa ya njoo tuishi au ya kanisani?

BAHARI YA MAPENZI: Ndoa ya njoo tuishi au ya kanisani?

SIZARINA HAMISI na DKT CHARLES OBENE

IMEKUWA jambo la kawaida kupata mwanaume anaishi na mwanamke bila ndoa, tena kwa muda mrefu.

Limekuwa mazoea kupata wapenzi wakiishi miaka kadha bila ya kuwepo makubaliano yoyote kisheria, kidini ama kimila.

Hivi karibuni dada mmoja aliniandikia barua pepe ndefu akinisimulia yaliyomkuta. Huyu dada aliishi na mwanaume kwa miaka minne, wakashirikiana kununua vifaa muhimu vya nyumbani na hata kufanikiwa kununua ploti wakiwa pamoja.

Lakini miezi michache iliyopita, yule mwanaume akamwambia arudi kwanza kwao, ili aweze kujipanga masuala ya ndoa naye.

Bila hiyana, dada akabeba sanduku lake la nguo na kurudi kwao akingoja mpenzi wake ajipange kwenda rasmi kwao na hatimaye kuanza utaratibu wa ndoa. Lakini kilichofuata, ni mpenziwe kufunga ndoa kanisani na mwanamke mwingine na hata kuhama ile nyumba waliyokuwa wakiishi pamoja.

Uchungu, hasira na hofu vilimtawala na ilichukua muda kuweza kurudi hali yake ya kawaida, kwani hakuwa na jinsi yoyote ya kuweza kumzuia mwenzake ama kudai vile ambavyo alinunua pamoja na mpenziwe.

Ukweli ni kwamba idadi kubwa ya ndoa za njoo tuishi, huwa zinaishia kuwa hivyo ama hata kuvunjika. Ni nadra kupata wanaoishi pamoja kwa muda mrefu hatimaye wakifunga ndoa.

Mara nyingi mwanaume anayekuambia njoo tuishi, basi uelewe nia yake ya kufunga nawe ndoa huenda ikawa ni kidogo sana ama hamna kabisa. Kwanini asikuoe kabla ya kuanza kuishi? Wapo wengine husingizia gharama, lakini ndoa sio sherehe ama shamrashamra, ni lengo na madhumuni hakika ya kuishi na kujenga maisha pamoja.

Mwanaume anapoanza kuishi na mwanamke anakosa sababu ya kufunga ndoa kwa sababu kila kitu ambacho kingemfanya kuoa anakipata tena bure au kwa bei rahisi. Lakini sio bure tu, tena kwa unyenyekevu. Wanaume ambao huishi na wanawake kwa namna hiyo wanajua kuwa, kama wakifunga ndoa na mwanamke, basi anakuwa na kiburi lakini mwanamke anayebembelezea ndoa, anakuwa na heshima na hunyenyekea ili asiachwe.

Jambo la msingi ni kwamba huyo sio mume ama mke wako, bali ni kimada mnayeishi pamoja. Anaweza kukuacha wakati wowote na hutakuwa na la kufanya ama hatua ya kuchukua kisheria. Kwa maana nyingine ni kwamba utaratibu wa njoo tuishi unarahisisha hata pale unapotaka kuachana ama kumuacha mwenzako,

Sheria ya ndoa ya Kenya, kifungu namba 4 cha 2014 inatambua aina nne pekee za ndoa, ndoa ya kiserikali, ndoa ya Kikristo, ndoa ya kimila na ndoa ya Kiislam. Kwa maana hiyo muungano wowote baina ya mwanamke na mwanaume ambao haujasajiliwa kulingana na sheria ya ndoa ya Kenya, haumaanishi kwamba ni ndoa.

Kwa hiyo, dada na hata kaka unapoamua kuishi na mwenzako bila kuchukua hatua ya kuhalalisha muunganiko wenu, utambue kwamba lolote litakapotokea utabaki peke yako na shughuli ya kupata haki yako kama itabidi, itakuwa yenye vurumai.

[email protected]

BINTI mmoja aliwatumia wazazi wake ujumbe kwenye simu uliosoma, “msinitafute maana nimekwishaolewa na mume niliyemchagua?”

Angalikuwa mwanao huyu, ungefanya nini? Ungehisi vipi kama mzazi kupokea dhoruba kama hii? Ijapo timia wakati wa janadume kuoa ama janajike kuolewa, sharti khanga za siri kuvuliwa, mambo yakawekwa wazi tena peupe. Raha ya ndoa kama ngoma za kitamaduni, ni mrindimo!

Hakuna siri wala cha siri kwenye ndoa. Hili litue na kukolea akilini mwa wachumba wanaotaka ama wanaodhamiria kuasisi familia. Ninasema “kutaka” na “kudhamiria” nikijua tosha kwamba sio wote wanaotaka wana dhamira. Isitoshe, ndoa ndio asili fasili ya familia nayo familia thabiti ndio kiini na msingi wa jamii thabiti. Hatuna budi kuwa watu wema wanaotaka tena wanaodhamiria mema. Dhamira ni sehemu ya ndoa thabiti.

Mjadala umekuwepo, upo na bado utakuwepo juu ya suala tata la “ndoa ya kanisani” ama “njoo tuanze maisha?”. Haidhuru! Lazima tuyaweke wazi mambo yanayostahili kudhihiri maishani mwa watu wenye hadhi wanaojua maana na hadhi ya ndoa. Achana na mahambe wanaoolewa na kuoa kama kuku kondeni mwa majirani. Ajabu ni kwamba hata jogoo hujizatiti kujitambulisha nyumbani kwa tembe! Mambo ya ndoa ni wajibu wa familia na jamii nzima. Hii ni kwa sababu ndoa ndio asili ya jamii!

“Ndoa ya kanisani” ama “njoo tuanze maisha?” Hili ndilo suala tata tunalojaribu kulitatua leo. Tunaliona kama jambo la kiutu kutia nyayo zetu majini ili kuchanganua kwa kina na kuzungumzia kwa uwazi suala tata la “ndoa halisi” katika jamii.

Isitoshe, tunalo jukumu la kimsingi kuelekeza jamii katika masuala yanayoleta uthabiti ndani mwa familia angalau kuchangia ukuaji na ukomavu wa wanandoa na wanadamu kwa jumla.

Katika asasi za ndoa, misimamo ya watu inatofautiana hali kadhalika kukinzana mno. Kuumeni, kuna kundi la waja wanaoshikilia msimamo kwamba ndoa sharti kusukwa kwa kamba na kuelekezwa kwa mujibu wa sheria za dini na mila za jamii. Kwa mujibu wa wangwana hawa, ndoa sio ndoa pasipo baraka ya wazee na dua za maabadani.

Kuukeni, kundi la pili linashikilia msimamo kwamba ndoa ni makubaliano na uamuzi wa wawili wanaopendana! Kundi hili linakataa katakata shinikizo za kuwahushisha wazazi na wakuu wa kidini katika shughuli na mambo ya ndoa zao.

Hekima daima hutukumbusha kuwatii, kuwasikiliza na kuwaheshimu wazazi ili nasi tujijenge kwa zao baraka. Ni kosa kubwa tena ufidhuli wa hali ya juu janadume na janajike kujitoza chumbani kama mke na mume pasipo kutaka radhi na dua za wazazi. Hivyo ni kusema kwamba hizi ndoa za “njoo tuanze maisha” hazina nafasi katika jamii staarabu!

Na ifahamike kwamba ndoa sio vifaabebe kupakatwa, kupakatana, kuchupia kisha kuchepuka kama wanadamu wendao msalani. Ndoa thabiti inajengwa kwa misingi ya hekima, imani, ufahamu, uelewa na dua za wazazi na jamaa kwa jumla. Wanandoa wanastahili mwongozo na mwelekeo wa watu waliokwisha kujijua na ndoa kuijulia. Katika ndoa hakuna cha siri wala sirisiri watu kuzikana kama jongoo mchangani!

[email protected]

  • Tags

You can share this post!

Wadudu waharibifu wavamia mashamba ya mahindi Gatundu...

Mioto shuleni: Rai wizara ibuni kamati maalum

T L