• Nairobi
  • Last Updated May 9th, 2024 8:50 AM
UMBEA: Penzi lina ladha ya kipekee, utamu, uchachu, uchungu na hata ukakasi kidogo

UMBEA: Penzi lina ladha ya kipekee, utamu, uchachu, uchungu na hata ukakasi kidogo

Na SIZARINA HAMISI

MAISHA ni kitendawili wakati mwingine.

Kwani unaweza kukutana na mtu anatembea barabarani lakini akili na mawazo yake yako mahali pengine. Na chanzo kikubwa kwa wengi ni mapenzi.

Hivi karibuni katika pilika pilika zangu nilizungumza na kaka ambaye katika umri wake unaozidi miaka 30, bado anajiuliza mapenzi yana maana gani hasa katika maisha ya mtu. Kwani kila anapojaribu kupenda, hapendwi. Akijaribu kutongoza, inashindikana. Amejaribu kuelewa hili penzi, lakini ameshindwa kabisa.

Nikatumia fursa ya kuzungumza naye na kumpa ufafanuzi wa hili suala la mapenzi.

Kawaida, penzi lina ladha ya kipekee.

Kuna mchanganyiko wa utamu, uchachu, uchungu na hata ukakasi kidogo. Hivyo unapopenda usitarajie utamu pekee kuna ladha zote ndani yake.

Pia usidanganywe na wajanja wa mjini, penzi halina dawa. Ni ujuzi, kuelewana, kutambuana na kugawana hisia baina yenu.

Penzi pia linahusisha kubembeleza, kubembelezwa na kuheshimiwa.

Wapo wengi wanaoshindwa kuelewa tofauti ya penzi na kuchangamsha mwili. Penzi halihusiani kabisa na kufanya ngono.

Hivyo kama unataka kupenda kwa dhati si lazima mrushane roho na kutafunana uroda. Ingawa kuchangamsha mwili ni muhimu, lazima upime kiwango na muda ambao mnaamua kufurahishana. Isiwe kila mkikutana hakuna mazungumzo ni kurushana kitandani na kuanza shughuli.

Pia penzi halilazimishwi hata siku moja. Kama hupendwi, ni hivyo huwezi kumlazimisha mwenzio akupende.

Hivyo ni jambo la busara ujiondoe mapema kwenye uhusiano ukiona hakuna dalili za penzi kati yenu. Kama unampigia simu mwenzio na majibu ni ya mkato ama ni mteja, anza kujitayarisha kwani uhusiano wenu hauelekei pazuri.

Kwa wenzangu wanaoamua kwenda kukoleza kwa mganga. Yaani wanalipa pesa na kwenda safari ndefu kwa nia moja pekee ya kumdhibiti mwanaume! Dada, kama hii ndio tabia yako, nakuhakikishia unapoteza pesa na muda wako, kwani penzi halipaliliwi kwa mganga hata siku moja.

Penzi lahitaji malezi, upendo, maelewano, kubembeleza na kuelewana na mwenzio na hata kusamehe wakati mwingine.

Hili penzi ni hisia zenye nguvu za ajabu kati ya mwanaume na mwanamke. Hisia hizi hazijalishi umaridadi, umevaa nini, sura yako ikoje, utajiri, umri, elimu na kama unaishi kijijini, mjini, hapa nchini ama ng’ambo.

Ukivamiwa na hisia hizi zinaweza zikufanye ushindwe kufanya shughuli zako za kawaida ambazo unazifanya kila siku. Kwani kichwani mwako kunakuwa na mawazo ya umpendaye kwa muda mrefu. Zinaweza kubadili tabia yako, hasa unapofanikiwa kuwa na yule umpendaye.

Na unapofanikiwa kumpata umpendaye, raha ya ajabu huingia moyoni. Kila umwonapo unajisikia kumgusa, kuzungumza naye ama hata kwenda naye faragha umbusu kidogo.

Ni rahisi sana kumjua mtu asiyekupenda, yule anayejifanya anakupenda na yule anayetaka kukuonja na kukutupa.

Kwa akina kaka, ukiona msichana anakuzungusha, kila mkipanga miadi hatokei ama ana sababu nyingi au akujibu maneno makali, ujue hujaingia moyoni mwake. Na ukiendelea kulazimisha ni mawili, ataamua akutumie kwa vyovyote atakavyoweza ama akueleze ukweli kuwa hakutaki.

Hivyo usilazimishe, acha mambo yaende taratibu kama penzi lipo litajitokeza.

Kuna wale dada zangu walioamua kuolewa na wanaume bila ya kuwapenda kwa sababu moja ama nyingine. Najua wanaishi kwenye ndoa zao kama wafungwa. Hawafurahii unyumba na waume zao, hawana uhuru wa kujieleza na na wa kufanya mambo wayapendayo.

Kuna wale walioamua kuolewa sababu ya pesa. Anaingia kwenye ndoa akijua kabisa hampendi mwanaume, lakini sababu ana tamaa ya maisha ya hali ya juu, anajitosa ndani ya ndoa na kuwa mateka wa moyo wake.

Ingawa jambo hili ni gumu na linawashinda kabisa wanawake na wanaume wengine, wapo wanaofanikiwa kuwapenda wenzao baada ya kuishi kwenye ndoa kwa muda.

Muhimu, usijisahau hata kama unapendwa. Palilia mapenzi yenu kila inapowezekana, kwani pia yanaweza kuchuja na kuchakaa kama hayatunzwi.

[email protected]

You can share this post!

Ruto aahirisha kikao cha wawaniaji wa Bonde la Ufa

Kananu kuapishwa kumrithi Mike Sonko

T L