• Nairobi
  • Last Updated May 17th, 2024 8:50 AM
PAUKWA: Bahati ajuta kuomba mama yake msamaha

PAUKWA: Bahati ajuta kuomba mama yake msamaha

NA ENOCK NYARIKI

WANAWAKE waliosimama karibu na Bi Cheusi walimwona akipaparika kwa wasiwasi wakamtahadharisha: “Mama, usicheze na ndimi za moto! Wewe ungali mwanamke mchanga na mrembo. Mungu atakujalia watoto wengi mfano wa mchanga wa bahari!’’

Hatua aliyoichukua Bi Cheusi ilionyesha bayana kwamba maneno yale yalitua kwenye sikio lililotiwa komango.

Kufumba na kufumbua, alilinyakua shuka la mmoja wa wanawake waliosimama kando yake akajitupia kichwani likateremkia mabegani.

Mbio za wenzake za kumzuia asijitose kwenye moto ambao uliroroma kwa ghadhabu zilikuwa bure yao!

Wingu la moto lilimmeza Cheusi. Nyuma, wenzake waliachwa wamefungua vinywa kwa mshangao. Kibanda cha maskini mwanamke yule si kikubwa kitu! Alisunzasunza akapafikia alipokuwa amemlaza mtoto. Mungu ni mkuu! Alimnyakua kwa kasi, akamrushia lile shuka alilokuwa amejitandia na kumkumbatia kifuani jinsi kuku anavyowakumbatia vifaranga chini ya mbawa zake.

Alipotoka nje, moto ulikuwa umemramba barabara! Nywele na ngozi vilitafunwa na moto. Hewa ilimwia chache akaanguka chini na kuzimia. Baadhi ya wanawake walikichukua kitoto Bahati wakaanza kukirairai na wengine wakambeba mama ya mtoto ili kumkimbiza hospitalini.

Hivyo ndivyo Bi Cheusi alivyoambulia lile kovu la usoni lililomtia mwanawe soni asipende kunasibishwa naye.

Bahati alilia hata zaidi alipogundua chanzo cha sura ya kutisha ya mama yake. Alijiona mtovu wa hisani.“Nisamehe mama!’’.

Bi Cheusi alimkumbatia mwanawe ambaye alitiririkwa na machozi kifua tele akayaacha machozi yenyewe yamloe kifuani pia.

  • Tags

You can share this post!

Juve Queens: Klabu yenye uwezo mkubwa wa kuinua talanta

Hofu huenda ukame ukaathiri uchaguzi

T L