• Nairobi
  • Last Updated May 4th, 2024 8:55 AM
Polisi wakanusha kujua aliko mwanamume aliyetoweka Lamu familia ikiwanyooshea kidole cha lawama

Polisi wakanusha kujua aliko mwanamume aliyetoweka Lamu familia ikiwanyooshea kidole cha lawama

Na KALUME KAZUNGU

POLISI katika Kaunti ya Lamu wamekana kujua kuhusu mwanamume aliyetoweka wiki mbili zilizopita, huku familia yake ikisisitiza alichukuliwa na maafisa wa polisi.

Familia ya Taimur Kariuki Hussein, 39, imedai hajaonekana tangu maafisa wa polisi wa kitengo cha kukabiliana na ugaidi (ATPU) walipoagizwa na mahakama kumwachilia huru.

Alikuwa amekamatwa wakati alipokuwa akielekea Lamu Juni 11 akafikishwa mahakamani Juni 14.

Mamake Taimur, Bi Zeinab Hussein, anasema ilipofika Juni 18, mashtaka aliyokabiliwa nayo, ikiwemo kuhusika na visa vinavyolingana na ugaidi na kukataa kukamatwa na polisi yalitupiliwa mbali, ambapo mahakama iliamrisha polisi wa ATPU kumwachilia.

Mamake Taimur, Bi Zeinab Hussein. Ameiomba serikali na idara ya usalama kusaidia familia yake kujua aliko mwanawe, Taimu, awe hai au akiwa amekufa. Picha/ Kalume Kazungu

Maafisa hao hata hivyo waliiomba mahakama kuwaruhusu kumfikisha Taimur kwenye kitengo cha APTU jijini Nairobi kwa uchunguzi zaidi.

Kulingana na Bi Hussein, alifikishwa tena kwenye mahakama ya Kahawa jijini Nairobi, Juni 21, ambapo polisi waliomba muda zaidi wa kumchunguza.

Juni 28, ambayo ndiyo iliyokuwa mara ya mwisho ya kuonekana kwa Taimur, familia yake inasema maafisa wa ATPU walimrudisha jamaa huyo kwenye mahakama hiyo hiyo ya Kahawa, ambapo kwa mara nyingine iliamriwa kumwachilia huru bila masharti yoyote.

Hata hivyo Taimur alitakiwa kutia sahihi ya kuachiliwa, shughuli ambayo iilifaa kufanyika kwenye kituo cha ATPU, hivyo walinda usalama wakaagiza familia kupitia kituoni ATPU baadaye ili kumchukua jamaa wao.

Bi Hussein anasema alishangaa pale alipofika kituoni tarehe hiyo hiyo hiyo ya Juni 28 na kuarifiwa kwamba kijana wake tayari alikuwa ameachiliwa karibu dakika 30 zilizopita.

“Nilishangaa kwa nini maafisa wa ATPU wanadai walimuachilia bila ya sisi wanafamilia kuwepo. Isitoshe, simu yake walibaki nayo. Walitarajia Taimur angezungumzaje nasi ili kumchukua Nairobi alikokuwa? Sijamuona wala kusikia kutoka kwa kijana wangu. Ninashuku walinda usalama wanajua aliko mwanangu na ninawaomba kutujulisha alipo, iwe yuko hai au amekufa. Tutaridhika kwa kila jambo,” akasema Bi Hussein.

Hata hivyo, Kamishna wa Kaunti ya Lamu, Bw Irungu Macharia na Mshirikishi wa Usalama Ukanda wa Pwani, John Elungata, walishikilia kuwa hawana taarifa zozote kuhusiana na tukio hilo.

“Sina habari kuhusu tukio hilo. Sijui,” akasema Bw Elungata.

Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Haki Africa, Bw Hussein Khalid, alimuomba Waziri wa Usalama, Dkt Fred Matiang’i kuingilia kati na kuhakikisha haki imepatikana kwa familia ya Bw Taimur na nyingine nyingi ambazo zinahangaika kuwatafuta waliko wapendwa wao.

Bw Khalid alisema visa vya watu kupotezwa wakiwa mikononi mwa walinda usalama vimeongezeka Pwani siku za hivi karibuni.

“Wanavyofanya walinda usalama wetu, kuwashika watu na kisha kuwapoteza badala ya kuwalinda ni makosa. Wanakiuka haki za binadamu na hatutakubali. Dkt Matiang’i aingilie kati kuhakikisha familia ambazo watu wao wamepotezwa zinapata haki,” akasema.

You can share this post!

Jinsi tunavyoweza kuimarisha umiliki wa vipande vya ardhi,...

GWIJI WA WIKI: Neema Salome Sulubu