• Nairobi
  • Last Updated May 12th, 2024 5:17 PM
Koome na idara yake kuwa na kibarua kikubwa mwaka ujao

Koome na idara yake kuwa na kibarua kikubwa mwaka ujao

Na RICHARD MUNGUTI

TUNAPOBAKISHA siku 11 kuumaliza mwaka wa 2021, macho yote ya Wakenya yanaelekezwa katika tukio kuu la mwaka ujao – Uchaguzi Mkuu.

Kama ilivyokuwa miaka ya 2013 na 2017, punde baada ya uchaguzi huo Agosti 9, shughuli nyingi zitatarajiwa kuonekana katika mahakama. Idara hiyo ya utekelezaji wa haki na sheria itakubaliana na mafuriko ya kesi za watakaohisi kuibiwa kura.

Ili kuzikabili, Jaji Mkuu Martha Koome atabuni kamati maalum ya majaji watakaoweka mikakati jinsi ya kusikiza na kuamua kesi zitakazotokana na zoezi hili.Kamati hii ya majaji wa mahakama ya rufaa na mahakama kuu itapanga jinsi ya kukabili kesi zitakazotokana na uchaguzi.

Kesi zitakazosababishia idara ya mahakama tumbojoto ni za urais, useneta ugavana, ubunge na udiwani (MCA).Nyingi ya kesi hizi zitamalizikia Mahakama ya Juu chini ya urais wa Jaji Koome.Kabla ya kesi hizi kuwasilishwa kortini, kamati ya tume huru ya uchaguzi na mipaka (IEBC) ya kushughulikia mizozo ya uteuzi ya wawaniaji viti itazishughulikia.

RIDHISHWA

Wale ambao hawatakuwa wameridhishwa na maamuzi ya kamati hii ya IEBC watawasilisha kesi zao kwa jopo la kutatua mizozo ya uteuzi katika vyama vya kisiasa mbali mbali (PPDRT).Wanasiasa watapepetana mbele ya PPDRT kisha vumbi litulizwe na uchaguzi kufanyika kisha warejelee malumbano katika mahakama kuu.

Gurudumu la uchaguzi likishika kasi wawaniaji wa viti watakaoshindwa katika zoezi hili ndio watakaofululiza hadi mahakamani.Mahakama ya Juu itaamua kesi ya kura ya urais peke yake kisha itoe uamuzi ikiwa uchaguzi wa urais utarudiwa au la.

Majaji wa Mahakama kuu kote nchini wanajiandaa kumenyana na kesi zitakazowasilishwa na wawaniaji wa viti vya ubunge, useneta, ugavana na udiwani.Katika muda wa miezi sita kuanzia Septemba 2022 mahakama kuu itakuwa na kivumbi na kindumbwe ndumbwe kikuu cha kesi kutokana na uchaguzi mkuu.

Kesi nyingi zitatokana na wale watakaomenyana kutoka mirengo ya kisiasa ya mibabe wa kisiasa Raila Odinga na William Ruto.Kesi chache zinatarajiwa kutoka kwa vyama vidogo vya kisiasa.Kesi ya kupinga matokeo ya uchaguzi ya urais itasikizwa na Jaji Koome, naibu wake (DCJ) Philomena Mwilu na Majaji Mohamed Ibrahim, Smokin Wanjala, Njoki Ndung’u, Isaac Lenaola na William Ouko.

Jaji Koome ambaye ndiye mwanamke wa kwanza kuteuliwa Jaji Mkuu nchini anakabiliwa na kibarua kigumu cha kuamusa kesi ya kupinga matokeo ya urais.Uamuzi atakaotoa ndio utamwidhinisha ikiwa anaweza kudhibiti idara ya mahakama au la.Macho yote na masikio yote yatakuwa kwake Jaji Koome kuona ikiwa atachukua mwelekeo uliochukuliwa na Jaji mkuu mstaafu David Maraga.

Jaji Maraga hakuharibu wakati kesi ya kupinga matokeo ya uchaguzi wa urais 2017.Mara moja aliufyatua na kuupasua ushindi wa Rais Uhuru Kenyatta 2017 na kuamuru uchaguzi wa urais urudiwe.Uamuzi huo wa 2017 uliopokea kwa hisia mbali mbali.

Wakenya wengi waliusifu na wachache wakaukemea.Hata hivyo uamuzi huu uliipatia umaarufu kote ulimwenguni idara ya Mahakama ya Kenya.Ukakamavu wake ulishabikiwa na majaji na mahakimu wakapasha misuli ya sheria na kutoa maamuzi ya kufana.

Akihojiwa na jopo la makamishna wa tume ya idara ya mahakama kabla ya kuteuliwa kuwa Jaji Mkuu, Jaji Koome alisukumwa mno atoboe siri ikiwa atafuata mkondo wa Jaji Maraga au la kuhusu suala la uchaguzi wa urais kesi itakapowasilishwa mbele yake.

USHAHIDI

Akiwajibu makamishna wa jopo la JSC , Jaji Koome aliewaeleza ataiamua kesi hiyo kulingana na ushahidi utakaowasilishwa.Swala lingine ambalo limekatalia katika meza ya Jaji Koome ni ile ya kutoapishwa kwa majaji sita na Rais Uhuru Kenyatta.Majaji hao sita walikuwa miongoni mwa majaji 40 waliohojiwa na JSC 2019 na majina yao kuwasilishwa kwa Rais wateuliwe.

KATAA KUAPISHA

Rais Kenyatta alikataa kuwaapisha huku akidai alipokea habari kwamba baadhi yao wameshiriki ufisadi.Majaji 34 kati ya hao 40 waliapishwa lakini sita -Joel Ngugi, Weldon Korir, Aggrey Muchelule, George Odunga, Evans Makori na Judith Omange – bado wanasubiri kuapishwa.

Majaji Ngugi, Korir, Muchelule na Odunga walikuwa wameteuliwa kuwa majaji wa mahakama ya rufaa.Makori na Omange waliteuliwa kuwa majaji wa mahakama kuu.Tangu uamuzi huo wa 2017 idara ya mahakama ilipata mwamko mpya.

Kuhusu suala hili la kutoapishwa kwa majaji , mnamo Oktoba Majaji George Ndulu, James Wakiaga na Roselyn Aburili walimwamuru Rais Kenyatta awaapishe la sivyo Jaji Koome ajitwike jukumu na kuwaapisha.Madai ya majaji hawa sita ni kwamba hawakueleza makosa yaliyosababisha Rais Kenyatta akatae kuwaapisha wajitetee.Kesi hii ingali katika mahakama ya rufaa ikisubiri kuamuliwa.

Mwanasheria mkuu alikata rufaa Rais Kenyatta kushurutishwa kuwaapisha.Maamuzi yanayotolewa na mahakama sasa ni tofauti na hapo awali tangu 2017.Maamuzi mbali mbali yanayokinzana na maagizo ya wakuu serikali siyo mageni tangu 2017.

Uamuzi huo wa 2017 wa Jaji Maraga na Mahakama ya Juu ulifanya idara ya mahakama kusimama imara kama fito.Sasa wakenya wanamtazamia Jaji Koome kuendeleza mkondo huo idara ya mahakama aliouweka Jaji Maraga.Alipokuwa akistaafu Jaji Maraga aliwaachia majaji ushauri huu, “Mimi nimestaafu.Naondoka na kuwaacha mwendeleze idara ya mahakama.

Msipozingatia sheria na kuisimamia katiba nchi hii itatumbukia kwenye shida historia itawahukumu vikali.”Kwa kuitikia wito wa Jaji Maranga majajaji watano wa mahakama kuu walisimamisha kura ya maoni iliyokuwa imepigiwa upatu na mchakato wa BBI.

Mahakama ya rufaa pia ilifuata mkondo na kusimamisha reggae kwa kusema zoezi hili la BBI lililenga kufanyia marekebisho katiba kinyume cha sheria.Kesi hii ya BBI bado ingali katika meza ya Jaji Koome.Wakenya wako na matarajio kuona ikiwa reggae itarudishwa au la.

Rais Kenyatta alisema wakati wa hotuba yake wakati wa sikuu kuu ya Jamhuri alisema “siku moja BBI itarejelewa.”Mwanasheria mkuu aliwasilisha rufaa kupinga uamuzi wa mahakama ya rufaa kutupilia mbali mchakato wa BBI.Kesi hii ya BBI ni mojawapo ya kesi kuu zaidi mahakamaya Juu inatazamiwa kuamua 2022.

You can share this post!

Maaskofu wahimiza serikali ikarabati daraja la mto Enziu

Balozi asifu uhusiano mwema wa Kenya na Japan

T L