• Nairobi
  • Last Updated May 4th, 2024 7:12 PM
Ruto ahimiza wakulima kugeukia Mungu kupata mazao tele   

Ruto ahimiza wakulima kugeukia Mungu kupata mazao tele  

NA SAMMY WAWERU

RAIS William Ruto amewapa wakulima changamoto, akiwahimiza ‘kukabidhi’ jitihada na bidii zao kwa Mwenyezi Mungu ili kunogesha mazao.  

Akisifia serikali yake kama inayoongozwa na viongozi wanaomcha Mungu, kiongozi wa nchi amesisitizia haja ya wakulima kuwa karibu na Mola.

Kwa kupalilia ushirikiano wa karibu na Muumba wa mbingu na nchi, Dkt Ruto amesema watashuhudia mazao chungu nzima.

“Huwezi ukafanikiwa kama mkulima ikiwa hujaelekeza bidii na jitihada zako kwa Mungu,” Rais akasema.

Dkt Ruto alitoa kauli hiyo mnamo Jumapili, Agosti 13, 2023 akizungumza katika Kanisa la Faith Evangelistic Ministry, Karen, Jijini Nairobi.

Rais aidha alitaja mazao kibao ya mahindi yanayotarajiwa mwaka huu, kama mfano kwa wakulima kufuatia imani yake kwa Mwenyezi Mungu.

“Tangu tutwae uongozi, tumekuwa tukiomba Mungu atusaidie kuangazia uhaba wa chakula Kenya na njaa. Na mwaka huu, 2023 tumeshuhudia mvua kubwa, ikilanganishwa na ya misimu ya awali – miaka mitano iliyopita,” Rais akafafanua.

Kuoa mke mcha Mungu

Isitoshe, alitaja mpango wa Ruzuku ya Mbolea kama mojawapo ya ajenda alizofanikiwa kuafikia kufuatia imani yake.

Dkt Ruto, aidha, amekuwa akionyesha na kudhihirisha ukristiano wake na kuthamini dini.

Rais pia ameoa mke mcha Mungu, Bi Rachael Ruto, ambaye ameonekana mara kadhaa akiongoza taifa katika maombi.

Naibu wa Rais pia, Rigathi Gachagua amenukuliwa mara kadha hadharani akisisitiza kwamba yeye ni mcha Mungu.

Mke wa Bw Gachagua, Dorcas Gachagua ni pasta.

Wakati akihudumu kama Naibu Rais, chini ya utawala wa serikali ya Jubilee, iliyoongozwa na Rais Uhuru Kenyatta ambaye kwa sasa ni mstaafu, kinara wa upinzani Raila Odinga na viongozi wenza walikuwa wakikosoa ukarimu wa Dkt Ruto hasa katika michango na harambee ya mara kwa mara kanisani.

Akimkosoa, Bw Odinga alitaka Ruto kufichua kiwango cha utajiri wake na kiini.

Rais Ruto amekuwa akitoa michango ya mamilioni ya pesa makanisani, akisisitiza kwamba hajutiii hatua hiyo kwa kile Mungu amemfanyia – Kummiminia baraka.

Kabla kujiunga na ulingo wa siasa, Ruto alikuwa mfugaji hodari wa kuku katika Kaunti ya Uasin-Gishu, anakotoka.

Amekuwa akisema ufanisi wake maishani, kiasi cha kuwa Rais wa Kenya, unatokana na msingi wake dhabiti kanisani na kumcha Mungu.

  • Tags

You can share this post!

Msaidizi wa mbunge wa Maragua alirogwa katika sakata ya...

Ahadi feki za Ruto kuhusu mahindi 

T L