• Nairobi
  • Last Updated May 4th, 2024 10:15 PM
Ruto: Kanini Kega alitusumbua chini ya utawala wa Jubilee tukambandika ‘Kanini Koru’

Ruto: Kanini Kega alitusumbua chini ya utawala wa Jubilee tukambandika ‘Kanini Koru’

NA SAMMY WAWERU 

RAIS William Ruto amesimulia mahangaiko aliyopitishwa na aliyekuwa mbunge wa Kieni Kanini Kega, chini ya utawala wa mtangulizi wake, Uhuru Kenyatta. 

Dkt Ruto alihudumu kama Naibu wa Rais, na 2018 mpasuko wa kisiasa uliibuka hasa baada ya muafaka kati ya Rais Kenyatta (japo sasa ni mstaafu) na kiongozi wa ODM, Bw Raila Odinga, maarufu kama Handisheki.

Ruto aidha alilalamikia kutengwa katika serikali ya Jubilee, aliyohoji kushiriki kuunda.

Jumatano, Agosti 9, 2023 Rais Ruto alisema Kanini Kega, akiwa kiongozi wa wengi bungeni alipitisha muungano wa Kenya Kwanza changamoto chungu nzima.

Bw Kega, alitwaa wadhifa huo baada ya aliyekuwa mbunge wa Garissa Mjini, Adel Duale kubanduliwa na vuguvugu la Jubilee.

Bw Duale kwa sasa ndiye Waziri wa Ulinzi.

“Kanini Kega alitusumbua mpaka tukamuita Kanini Koru,” Ruto alisema akizungumza eneo la Naromoru, Nyeri.

Jumatano, Rais Ruto, naibu wake Rigathi Gachagua na baadhi ya viongozi wakuu serikali ya Kenya walikamilisha ziara ya siku tano eneo la Mlima Kenya, ambapo walizindua miradi mbalimbali ya maendeleo.

Kanini Kega, ni majina yenye asili ya Agikuyu yanayomaanisha ‘kidogo kizuri’ hivyo basi majina ya usumbufu aliyobandikwa yanamaanisha ‘kidogo kibaya’.

Kega alikuwa anaunga mkono kinara wa Azimio, Bw Odinga kuingia Ikulu katika uchaguzi mkuu wa 2022, ambaye pia alikuwa anapigwa jeki na Kenyatta.

Mbunge huyo wa Bunge la Afrika Mashariki (EALA), hata hivyo, sasa anaunga mkono utawala wa Ruto.

“Amebadilisha mawazo na sasa ni wetu. Tunafanya kazi pamoja,” Ruto akasisitiza, akidokeza kwamba alimsamehe.

Bw Kega aliwania kuhifadhi kiti chake cha ubunge 2022 kupitia chama cha Jubilee, japo alionyeshwa kivumbi na Anthony Njoroge Maina (UDA).

UDA ni chama kinachoongozwa na Dkt Ruto.

 

  • Tags

You can share this post!

Linda Njoki: Siwezi nikalia kwa sababu ya mapenzi

Hospitali 260 zafungwa kwa kutokidhi viwango

T L