• Nairobi
  • Last Updated May 4th, 2024 5:07 PM
SHINA LA UHAI: H. pylori: Bakteria hatari wanaotesa mamilioni ya Wakenya

SHINA LA UHAI: H. pylori: Bakteria hatari wanaotesa mamilioni ya Wakenya

Na LEONARD ONYANGO

JE, umekuwa ukihangaishwa na maumivu makali tumboni kwa kipindi kirefu na kuhisi kushiba hata bila kula, kuna uwezekano mkubwa kwamba unasumbuliwa na ugonjwa wa Helicobacter pylori, al-maarufu H.pylori.

Bakteria hao wanapoingia tumboni, hushambulia ‘ukuta’ wa tumbo ambao huilinda dhidi ya kuharibiwa na asidi (nyongo) inayotumika kusaga chakula tumboni.Bakteria hao hatari hufanya tumbo kuwa na asidi nyingi hivyo kusababisha vidonda tumboni (ulcers), kuwasha kwa ‘ukuta’ wa tumbo na kansa ya tumbo (gastric cancer).

Mnamo 2015, wataalamu wa afya kutoka nchi mbalimbali duniani waliafikiana kwamba kuangamiza H.pyroli kutasaidia pakubwa katika kupunguza visa vya kansa ya tumbo ulimwenguni.

Kansa ya tumbo huchangia asilimia 6.3 ya vifo 32,000 vinavyotokana na saratani kila mwaka humu nchini.

Hiyo inamaanisha kuwa huua takribani watu 2,000 humu nchini kila mwaka.

Kati ya visa vipya 47,800 vya kansa ambavyo hubainika hospitalini kila mwaka nchini Kenya, kansa ya tumbo huwa asilimia 4.4, kwa mujibu wa takwimu za wizara ya Afya.

Kansa hii ilisababisha vifo vya 769 000 kote duniani, kulingana na Shirika la Afya Duniani (WHO).

Mnamo 2019, watu 1,058,327 walitibiwa H. pylori humu nchini, kulingana na takwimu za wizara ya Afya.

Kevin Ochola, mkazi wa mtaa wa Kibra jijini Nairobi, anasema kwamba amekuwa akisumbuliwa na ugonjwa huo tangu 2019.

“Baada ya kuhisi maumivu tumboni kwa takribani mwezi mmoja, niliamua kwenda hospitalini lakini ugonjwa haukupatikana. Nilipewa dawa za kutuliza maumivu lakini sikupata nafuu. Januari 2020, nilirudi hospitalini ikabainika kwamba nilikuwa na H. pylori. Nilipewa tembe za kumeza kwa siku 15 na nilipopimwa tena bakteria hao walikuwa wametoweka,” anaeleza.

Mapema mwaka huu 2021, Bw Ochola alianza kuumwa na tumbo tena. Maumivu yalizidi mwezi uliopita na alipoenda kupimwa, ilibainika kwamba anasumbuliwa na H. pylori.

Naye, Alice Kariuki anasema kuwa alisumbuliwa na tumbo kwa miezi kadhaa mwaka jana hadi pale alipopimwa na kupatikana na bakteria hao.

“Nilipewa dawa nyingi na nilinunua kwa bei ghali. Nilimeza dawa chache tu maumivu yakaisha na ninashukuru Mungu nilipona,” anasema.

Dkt Christopher Opio, mtaalamu wa afya ya tumbo katika Hospitali ya Aga Khan, Nairobi, anasema kuwa H.pylori huenezwa kwa kula chakula ambacho hakijasafishwa vyema na kunywa maji machafu.

Anasema kinyesi au matapishi ya mwathiriwa yanaweza kusababisha mtu kupata baketria hao.

Kulingana na Dkt Opio, wapenzi au wanandoa wanapopigana busu mdomoni na mate yao kukutana, wanajitia katika hatari ya kuambukizana H.pylori ikiwa mmoja wao atakuwa na bakteria hao.

“Hiyo ndiyo maana mwanaume akipatikana na H.pylori ni vyema mke wake pia apimwe ili tuthibitishe ikiwa ana bakteria hao au la. Mke akiwa na bakteria hao bila kupewa dawa, itakuwa kazi bure kutibu mumewe,” anasema Dkt Opio.

Dalili nyingine za ugonjwa huo ni kuhisi tumbo ‘kuchomeka’, kichefuchefu, kukosa hamu ya kula na tumbo kufura.

Wataalamu wanaonya kuwa mtu anapohisi ugumu wa kumeza chakula au kukojoa na kutoa kinyesi cha rangi nyeusi, anafaa kukimbia hospitalini haraka kwani hizo ni dalili kwamba ugonjwa huo umefikia pabaya.

Utafiti uliofanywa mnamo 2015 humu nchini, ulibaini kwamba takribani asilimia 67 ya Wakenya wanaugua H.pyroli.

Dkt Opio anasema kuwa japo mamilioni ya Wakenya wana bakteria hao, ni baadhi tu ambao huwa na dalili kama vile maumivu ya tumbo, kichefuchefu, kufura kwa tumbo kati ya nyinginezo.

Dkt Kimang’a Nyerere, mtaalamu wa viini na mhadhiri katika Chuo Kikuu cha Kilimo na Teknolojia cha Jomo Kenyatta (JKUAT), anasema kuwa idadi kubwa ya Wakenya wanaokunywa maji machafu wako katika hatari ya kupatwa na H.pylori.

“Mnamo 2016, mimi na wenzangu tulitafiti uwepo wa H.pylori katika mito mitatu jijini Nairobi – mto Nairobi, Ngong na Mathare. Tulibaini kwamba kulikuwa na bakteria hao kwenye maji ya mito hiyo. Asilimia 90 ya watu wanaoishi karibu na mito hiyo tuliowapima, walipatikana na bakteria hao,” anasema Dkt Nyerere.

Anatabiri kwamba idadi ya visa vya H.pylori jijini Nairobi itaongezeka zaidi katika miaka ijayo.

“Hii ni kwa sababu idadi ya watu, haswa katika mitaa ya mabanda inaendelea kuongezeka. Ikiwa hatua mwafaka hazitachukuliwa kuboresha mazingira, hali itakuwa mbaya zaidi katika siku za usoni,” anasema.

Dkt Nyerere anaonya kwamba baadhi ya wagonjwa hawamalizi dawa walizopewa na daktari hivyo bakteria hao hawaishi tumboni.

“Usipomaliza dawa, kuna hatari ya kuambukizwa tena. Kutomaliza dawa si tatizo la Kenya pekee bali ni changamoto ambayo imeripotiwa kote duniani. Kutomaliza tiba kunamaanisha kwamba bakteria hao wanazoeana na dawa hivyo hazitakusaidia wakijitokeza tena,” anaeleza.

Matibabu

Dkt John Kiiru wa Taasisi ya Utafiti wa Matibabu nchini (Kemri), anasema kuwa si bakteria wote wa H.pylori ni hatari.

“Baadhi ya bakteria hao wanaishi tumboni bila kusababisha madhara yoyote. Mara nyingi watu wanaoenda hospitalini wakipimwa kinyesi na kupatikana na ugonjwa huu, wanapewa tembe za kukabiliana na bakteria hao. Lakini baada ya kumaliza dawa maumivu yakiendelea tu, inamaanisha kuwa huenda mgonjwa anasumbuliwa na maradhi mengine na wala si H.pylori,” anasema.

Anasema kuwa vifaa vilivyoidhinishwa kupima bakteria hao nchini Kenya, havina uwezo wa kubaini ikiwa bakteria hao wana madhara au la.

“Wataalamu wa Kemri walifanya utafiti katika hospitali za Nairobi na wakabaini kwamba kati ya wagonjwa 100 waliokuwa wanatibiwa H.pylori ni watano tu ndio walikuwa na bakteria hatari.

Hiyo inamaana kwamba wengine walikuwa na magonjwa mengine lakini wakapatiwa dawa ya H.pylori kwa sababu bakteria hao walipatikana kwenye kinyesi chao,” anaeleza.

H.pylori hutibiwa kwa kutumia viua vijasumu (antibiotics) na tembe za kupunguza asidi tumboni (antacids).

Mgonjwa hutakiwa kumeza tembe hizo kwa kati ya siku 10 na 15.

Japo vipimo na dawa za H.pylori katika hospitali za umma hutolewa bila malipo, ni ghali katika hospitali za kibinafsi.

Kwa mfano, katika hospitali ya Aga Khan, kipimo hugharimu Sh6, 000 na dawa pia zinagharimu kiasi sawa na hicho.

Kujilinda dhidi ya H pylori

Dkt Nyerere anasema kuwa usafi ni njia mojawapo ya kuepuka ugonjwa wa H.pylori“Kunawa mikono baada ya kutoka chooni na kabla ya kula ni muhimu katika kuzuia maambukizi. Epuka kula vyakula ambavyo hali yake ya usafi inatiliwa shaka na kunywa maji machafu. Kula vyakula ambavyo vimepikwa vyema,” anashauri Dkt Nyerere.

You can share this post!

Mali fiche yafichuka

Niliwaomba PSG waniachilie ili niyoyomee Real Madrid...