• Nairobi
  • Last Updated May 18th, 2024 3:46 PM
Niliwaomba PSG waniachilie ili niyoyomee Real Madrid – Kylian Mbappe

Niliwaomba PSG waniachilie ili niyoyomee Real Madrid – Kylian Mbappe

Na MASHIRIKA

FOWADI matata raia wa Ufaransa, Kylian Mbappe, amekiri kwamba aliwasilisha ombi la kuagana na Paris Saint-Germain (PSG) mwishoni mwa msimu uliopita wa 2020-21 baada ya Real Madrid kufichua azma ya kuwania huduma zake.

Ingawa hivyo, ameshikilia kwamba anafurahia maisha yake jijini Paris na kubwa zaidi katika maazimio yake kwa sasa ni kumakinikia majukumu yake kambini mwa PSG.

Ofa mbili za Sh21 bilioni na Sh23 bilioni zilizotolewa na Real kwa ajili ya maarifa ya Mbappe, 22, mnamo Julai na Agosti 2021 zilikataliwa na PSG.

Katika mahojiano yake na wanahabari wa RMC Sport nchini Ufaransa mnamo Oktoba 4, 2021, Mbappe alifichua kwamba alipania sana kuondoka uwanjani Parc des Princes kabla ya kampeni za muhula huu kuanza ili kuepuka hali ambapo angeagana na PSG bila ada yoyote baada ya mkataba wake wa sasa kutamatika rasmi mwishoni mwa msimu wa 2022-23.

“Nilitaka PSG waniuze ili wapate pesa nzuri za kutafuta mrithi wangu pale kambini. Msimamo wangu ulikuwa wazi na wa kweli. Nilitaka kuondoka,” akatanguliza.

“Sikufurahia madai ya PSG kwamba niliwapa taarifa za kutaka kukatiza uhusiano nao mwishoni mwa Agosti. Niliwasilisha ombi langu kwao mapema Julai.”

“Niliwapa habari hizo mapema sana ili wawe na muda wa kutosha kujipanga. Matamanio yangu yalikuwa ni kuondoka PSG kwa uzuri kwa sababu naamini bado tungehitajiana katika siku za usoni,” akaongeza Mbappe.

Nyota huyo aliyesaidia Ufaransa kunyakua ubingwa wa Kombe la Dunia mnamo 2018 nchini Urusi, anajivunia kufungia PSG jumla ya mabao 136 kutokana na mechi 182 tangu ajiunge nao kutoka AS Monaco mnamo Agosti 2017.

“Naheshimu maamuzi ya PSG kutonitia mnadani. Hiki ni kikosi ambacho kimekuwa na mchango mkubwa katika makuzi yangu kitaaluma. Nimefurahia sana kipindi cha miaka minne ambapo nimekuwa hapa, na bado naona fahari tele.”

“Niliwaambia PSG kwamba nilikuwa tayari kusalia kambini mwao na kuwachezea kwa kujitolea iwapo hawakuwa radhi kuniachilia kutafuta hifadhi mpya kwingineko,” akaongeza.

Kusalia kwa Mbappe kambini mwa PSG kunafanya kikosi hicho kujivunia maarifa ya mafowadi mahiri zaidi duniani wakiwemo Neymar Jr na Lionel Messi aliyejiunga nao mnamo Agosti 2021 baada ya kuagana ghafla na Barcelona ya Ligi Kuu ya Uhispania (La Liga).

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

You can share this post!

SHINA LA UHAI: H. pylori: Bakteria hatari wanaotesa...

Watford waajiri kocha Claudio Ranieri kujaza pengo la Xisco...