• Nairobi
  • Last Updated May 4th, 2024 6:09 PM
SHINA LA UHAI: Kukabili athari za tabianchi: Denmark mfano mzuri kwa Kenya

SHINA LA UHAI: Kukabili athari za tabianchi: Denmark mfano mzuri kwa Kenya

Na PAULINE ONGAJI

HUKU ulimwengu ukiendelea kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi, Denmark, taifa la idadi ya watu milioni 5.7 pekee, limechukua hatua, kuweka mifumo na kupitisha sheria za kulinda mazingira.

Hii imelifanya taifa hili kuwa mfano mzuri sio tu kwa taifa linalostawi kama Kenya, bali hata kwa mataifa yenye uwezo mkuu wa kiuchumi duniani, inapowadia katika mbinu kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi.

Kwa hivyo ni yapi ambayo Kenya, mojawapo ya mataifa yanayokumbwa na changamoto za kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi, inaweza ikajifunza?

Hewa safi

Hewa safi kutokana na uchukuzi

Shirika la Afya Duniani linakadiria kwamba uchafuzi wa hewa husababisha vifo milioni saba vya mapema kila mwaka, na takriban asilimia 80 ya watu wanaoishi mijini wamo hatarini.

Aidha uchukuzi ndio chanzo kikuu cha uchafuzi wa hewa mijini. Kwa upande mwingine, taifa la Denmark linaongoza katika kutoa suluhu za usafiri salama kimazingira, huku matumizi ya baiskeli katika maeneo ya mijini yakihimizwa, ili kupunguza misongamano ya magari na uchafuzi wa hewa.

Baiskeli nje ya jengo la Folketing jijini Copenhagen, Denmark. Picha/ Pauline Ongaji

Denmark inatambulika kwa kuwa na desturi thabiti ya uendeshaji baiskeli, ambapo zaidi ya asilimia 50 ya watu wanaoishi katika jiji kuu la Copenhagen, husafiri kila siku kwa baiskeli.

Hewa safi kutoka viwandani

Kulingana na WHO, viwanda vya uzalishaji bidhaa, uchimbaji madini na usafishaji mafuta, vile vile mitambo ya kuzalisha umeme, vimeonekana kuchangia pakubwa uchafuzi wa hewa.

Taifa hili limevumbua teknolojia mbalimbali za kukabiliana na moshi na ekzosi kutoka mitambo ya nguvu za umeme na viwanda vya kuchoma uchafu.

Nishati kutoka kwenye uchafu

Nchini Denmark, viwanda vya kuchoma uchafu huzalisha joto zaidi ya umeme. Joto hili husambazwa kupitia mfumo maalum kwa zaidi ya asilimia 12 ya majumba ya makazi nchini humo.

MAJI

Ubora na usafishaji maji

Kwa kusafisha maji, tangu mwaka wa 1980 taifa la Denmark limeweza kupunguza matumizi ya maji kwa asilimia 40.Suluhu za kusafisha maji nchini humo ni pamoja na mifumo ya UV disinfection systems (mbinu inayohusisha kusafisha maji kwa kuangamiza seli na chembechembe za DNA za bakteria kwa kutumia nishati ya sumaku umeme, na hivyo kuzuia zisizaane), teknolojia ya elektrolisisi, teknolojia ya utando ya kusafisha maji na kuondoa chumvi toka kwenye maji ya bahari, teknolojia za usafishaji maji ya mvua na suluhu zingine za kawaida za kuimarisha ubora wa mazingira ya maji.

Usambazaji maji

Usambazaji maji nchini humo umegatuliwa huku usimamizi wa maji ukiwa katika sehemu zote nchini.

Aidha, maji ya ardhini ndio chanzo cha kipekee cha maji ya kunywa nchini humo. Kutokana na hayo, mfumo sahili wa kutibu maji ndio unaohitajika na maji ya mfereji hayatibiwi kwa kutumia klorini, kwani wana mfumo ambapo bakteria na uchafu mwingine vinapunguzwa.

Kutibu maji ya kunywa

Maji yote ya mfereji hutoka ardhini ambapo huhitaji kutibiwa kwa usahili tu kabla ya kusambazwa hadi kwa wateja kupitia mabomba yaliyozibwa. Hii hupunguza gharama na kuondoa haja ya matumizi ya klorini na kemikali zingine, huku ikipuguza hatari ya kuwepo bakteria.

Maji yanayopotelea mjini

Kulingana na Shirika la Umoja wa Mataifa, matumizi ya maji duniani kote yataongezeka kwa asilimia 30 kufikia mwaka wa 2020. Ili kutosheleza mahitaji haya, kuna haja ya kuzingatia usambazaji maji thabiti.

Maji yanayopotelea mijini (Non-Revenue Water (NRW) ni changamoto kuu ulimwenguni kote huku kati ya asilimia 25 na 50 ya maji yanayosambazwa duniani kote, yakipotea au kutolipishwa kutokana na uunganishaji haramu wa maji, mifumo dhaifu ya kulipisha maji, vipimamaji dhaifu, maji kuvuja, miundo misingi mibovu na usimamizi dhaifu wa kasi ya maji. Kwa upande mwingine, huduma za usambazaji maji nchini humo zimeweza kupunguza uharibifu wa maji kwa asilimia nane (8%) pekee.

Majitaka

Duniani kote, nusu ya majitaka yanayozalishwa hukusanywa, na chini ya asilimia 20 ya maji haya hutibiwa na kurejeshwa katika mazingira asili. Nchini Denmark, asilimia 95 ya majitaka yote hutibiwa.

Kutibu majitaka

Duniani, inakadiriwa kwamba chini ya asilimia 20 ya majitaka kutoka manyumbani na viwandani, hukusanywa na kutibiwa.

Isitoshe, ni takriban kati ya asilimia 50 na 60 ya mifumo ya kupitisha majitaka yanayotimiza vigezo hivi. Hii ni kutokana na uwezo duni au miundo msingi isiyo thabiti.

Lakini, taifa hili lina muundo thabiti wa kupunguza athari kutokana na majitaka na kuhakikisha kwamba maji haya yanasafishwa kwa ubora wa hali ya juu.

Matumizi thabiti na uhifadhi wa maji

Kufikia mwaka wa 2030, zaidi ya nusu ya idadi ya watu ulimwenguni wataishi katika maeneo yanayokumbwa na uhaba wa maji.

Ili kuhakikisha matumizi thabiti na uhifadhi wa maji, taifa hili limebuni mbinu kadha wa kadha, ikiwa ni pamoja na kupunguza maji yanayovuja kupitia mabomba, kubuni vipimamaji vya lazima, vile vile ushuru wa kutumia maji na kutoa majitaka.

Pia, kuna kampeni za kuhamasisha umma kuhusu uhifadhi wa maji na kuhimiza matumizi ya vifaa vinavyookoa maji.

Kutokana na haya, tangu mwaka wa 1980 taifa hili limepunguza matumizi ya maji kwa takriban asilimia 40, na matumizi ya maji manyumbani yamepunguzwa na kufikia lita 104 kwa siku.

TAKA

Huku idadi ya watu ulimwenguni kote ikiendelea kuongezeka na matumizi ya bidhaa mbalimbali yanaendelea kuwa juu, kumekuwa na ongezeko la taka.

Kukabiliana na taka hatari Nchini Denmark, kuna sheria kali zinazoshurutisha mashirika na raia kutupa taka hatari kwa njia inayofaa na hivyo kudumisha usafi wa mazingira, huku usafishaji salama wa taka likiwa jukumu la viwanda maalum.

Kuharibu taka na kusafisha

Kila mwaka, sekta ya taka nchini Denmark hukusanya na kusafisha tani milioni 15 za taka. Viwanda vya kubadilisha taka na kuwa nishati nchini humo, hubadilisha taka na kuzalisha joto na nguvu za umeme.

Viwanda vya kuchoma taka nchini humo ndio safi na thabiti zaidi ulimwenguni, na sababu mojawapo kwamba kiwango cha taka kinachotupwa kwenye majaa ya taka nchini humo, ni chini ya asilimia tano.

VYANZO SALAMA VYA UZALISHAJI NISHATI

Tangu 1980, taifa hili limeweza kutenganisha ukuaji wa kiuchumi na matumizi ya jumla ya nishati.

Kwa mfano utajiri wa nchi kwa jumla (GDP) umekua kwa asilimia 100, ilhali matumizi ya nishati yameongezeka kwa asilimia 6 pekee, na matumizi ya maji yamepungua kwa asilimia 40.

Nishati kutoka ardhini

Mwaka wa 2015, chini ya asilimia 0.5 ya joto linalozalishwa nchini humo, lilitokana na nishati kutoka ardhini.

Nishati ya upepo

Mwaka wa 2019, nishati ya upepo nchini humo ilitoa zaidi ya asilimia 47.2 ya nguvu za umeme zilizotumika nchini humo.

Mifumo ya nishati ya kisasa kiteknolojia

Kama mataifa mengi, wakati mmoja Denmark pia ilitegemea mafuta kutoka mataifa mengine na aina nyingine ya fueli za visukuku (fossil fuels).

Hii leo, zaidi ya asilimia 30 ya nishati inayohitajika nchini humo, hutokana na vyanzo au mifumo asili (renewables). Takriban asilimia 70 ya nguvu za umeme zinazotumika nchini humo hutokana na nishati asili.

Vipima umeme vya kisasa kiteknolojia

Vipima umeme vya kisasa kiteknolojia vinaweza kunakili matumizi ya nishati kwa vipindi fulani na kuwasilisha ujumbe kwa mashirika husika, kwa minajili ya ukaguzi na kulipisha.

Hii hupunguza matumizi ya nguvu za umeme wakati wa matumizi mengi, na kuimarisha utegemezi endapo kutakuwa na upungufu au hitilafu.

Majengo ya kisasa kiteknolojia

Nchini humo, asilimia kubwa ya majengo yana vifaa maalum vya kutambua mwangaza, ubora wa hewa na kupunguza matumizi ya nishati.

Aidha, yamejengwa kwa kutumia teknolojia ya kisasa kiasi cha kwamba yana uwezo wa kustahimili na kudhibiti athari zinazotokana na mabadiliko ya tabianchi.

Hii imepunguza gharama zinazotokana na ukarabati na ujenzi mpya wa majengo hasa baada ya majanga asili, kama vile mafuriko.

[email protected]

You can share this post!

Muuzaji bidhaa za hospitali apewa muda kulipa deni la...

Malumbano makali kati ya mawakili na DPP kuhusu kesi ya...