• Nairobi
  • Last Updated May 4th, 2024 7:12 PM
SHINA LA UHAI: Ugonjwa wa kupasuka mdomo una suluhu

SHINA LA UHAI: Ugonjwa wa kupasuka mdomo una suluhu

NA WANGU KANURI

MIAKA minne iliyopita, Sarah Naomi alijifungua mtoto wa kike ambaye alimletea furaha kuu.

Naomi ambaye alijifungua kwa kufanyiwa upasuaji, anaeleza kuwa baada ya kujifungua, madaktari walimweleza kuwa mtoto wake alizaliwa na tatizo.

Hakuweza kumuona mtoto wake kwa muda huku akiwa mwenye hofu na kujiuliza maswali mengi kuhusu kilichomtendekea mwanawe.

Hata hivyo, madaktari walimhakikishia kuwa mtoto huyo atakuwa sawa iwapo atapokea matibabu huku wakimfahamisha kuwa mwanawe alikuwa akiugua ugonjwa wa kupasuka mdomo almaarufu cleft lip and palate.

“Sikuwa najua chochote kuhusu ugonjwa huo,” anasema.

Mtoto huyo alipelekwa kwa chumba cha watoto wachanga ambapo alimsubiri mumewe akiwa wodi kuweza kumuelezea kilichojiri.

“Alipofika hospitalini, nilimweleza aende kwenye chumba alichokuwa mtoto wetu na kunipigia mtoto picha ili niweze kujua alikuwa mgonjwa wapi,” anaeleza.

Kwa fikra zake, Naomi alitumaini kuwa mtoto huyo angepokea matibabu mara moja, lakini madaktari wakamshauri kuwa na subra ya kama miezi mitatu kabla hajafanyiwa upasuaji ili kurekebisha sura ya mdomo wake.

Kisa chake Naomi ni sawa na cha Nathan Abbot mzaliwa wa Uingereza ambaye pia alizaliwa na ugonjwa wa kupasuka mdomo.

Alipozaliwa, mama yake Abbot alihisi mpweke sana haswa alipomuona mwanawe huku akiugua ugonjwa wa msongo wa mawazo, unaoathiri baada ya wanawake baada ya kujifungua.

Licha ya kufanyiwa upasuaji na kupata afueni, Abbot anasimulia kuwa hapo awali alinyanyaswa sana na wanafunzi wenzake kwa utofauti wake wa sura.

“Wanafunzi hao walinibandika majina ya dhihaka na kutotaka kushirikiana na mimi pale shuleni. Unyanyasaji ule uliniathiri sana kimawazo mpaka wakati mmoja nikakataa kuenda shuleni na kuwarai wazazi wangu kuniruhusu nipate mafunzo yale nyumbani,” anasimulia.

Abbot, 25, anaeleza kuwa zaidi ya kuzaliwa kwenye nchi iliyoendelea kiteknolojia na kiuchumi, ameanzisha wakfu nchini Kenya ambao kwa ushirikiano na hospitali ya watoto ya Getrude hutoa huduma bila malipo kwa watoto wanaozaliwa na hali hii.

“Ninaelewa fika wanachopitia wagonjwa wa kupasuka mdomo na kupitia usaidizi wangu ninawapa moyo wazazi wa watoto ya kwamba watoto wao watapata afueni,” anasema Abbot.

Ugonjwa wa kupasuka mdomo huathiri mtoto mmoja kati ya 700 na haubagui jinsia, rangi wala nchi anayotoka mtoto.

Ugonjwa huu hutokana na kasoro kwenye shingo au kichwa huku jeni na mazingira anamozaliwa mtoto yakichangia ongezeko lake.

Kwa mujibu wa Daktari Tom Osundwa, mtaalamu wa ugonjwa huu na ambaye hufanya upasuaji kwa wagonjwa wa kupasuka mdomo, mama mjamzito ambaye hali vyakula vyenye madini ya kuongeza damu (iron), folic acid na vitamini B ambavyo husaidia mwili kupata nguvu, huenda akaathiri mtoto.

“Ugonjwa wa kupasuka mdomo hujitokeza aidha kwenye sura au juu – sehemu ya ndani ya mdomo,” anaeleza daktari.

Hata hivyo, wazazi ambao mtoto au watoto wao hupata hali hii na huenda wakashika mimba tena hushauriwa kumeza dawa za kumsaidia mtoto kukua vizuri akiwa tumboni.

Nchini Kenya, wagonjwa 30,000 hawajapokea matibabu ya ugonjwa huu huku watu wengi wakidhani kuwa mtoto anayeugua ameupata ugonjwa huo kutokana na uchawi.

Ukosefu wa maarifa kuhusu ugonjwa huu wa kupasuka mdomo huchangia katika uenezaji wa dhana potovu, asema Dkt Osundwa.

“Nilipozuru kitongoji kimoja katika Kaunti ya Pokot Magharibi pamoja na wanamishonari, tuliweza kumuokoa mtoto ambaye alikuwa awachwe msituni aliwe na fisi,” Dkt Osundwa anasimulia.

“Mama ya mtoto huyo alikuwa amepewa onyo kali na viongozi wa jamii aliyokuwa akiishi huku akielezwa asirudi kitongojini akiwa na mtoto huyo ambaye alionekana kama mjaa laana.”

Licha ya wagonjwa kupata nafuu na sura zao kuwa kama za watoto wengine, wanastahili kufanyiwa upasuaji mara mbili.

Upasuaji wa kwanza huwa kwa sura ya mdomo na hufanywa mtoto akiwa na miezi mitatu huku ule wa ndani ya mdomo ukifanywa wakati mtoto yupo na umri wa kati ya mwaka mwaka mmoja hadi mwaka moja na nusu.

Hali kadhalika, Dkt Osundwa anawashauri wazazi kutochelewa kuwapeleka watoto wao hospitalini huku akisema kuwa kuchelea huathiri uwezo wao wa kutamka silabi na maneno.

Wazazi ambao watoto wao huugua ugonjwa huu hupitia unyanyapaa huku wakionelea ni heri kuwaficha nyumbani.

Watoto hao huishia kudhoofika kutokana na utapia mlo kwani hawawezi kula au kuzungumza vizuri.

Vile vile, gharama ya juu ya kupokea matibabu ikiwa changamoto kwao.

Inakadiriwa kuwa zaidi ya Sh250,000 huhitajika ili mtoto kufanyiwa upasuaji huu huku familia za watu maskini zikitatizika kuchanga pesa hizo.

“Changamoto nyingine za mgonjwa wa kupasuka mdomo ni pamoja na kutatizika akila, kupata maambukizi ya sikio na mapafu mara kwa mara, kukosa kutamka silabi zingine inavyofaa na kushindwa kusikia,” anaongezea Dkt Osundwa.

Kulingana na Kituo cha Kudhibiti na Kuzuia Magonjwa (CDC) kina mama wajawazito ambao wanavuta sigara, wale wanaougua ugonjwa wa kisukari pamoja na wale ambao hutumia dawa za kutibu kifafa kama vile topiramate au ya valproic acid katika miezi ya kwanza tatu wapo kwenye hatari ya kujifungua watoto wenye ugonjwa huu.

Mwezi Novemba, zaidi ya watoto 50 waliokuwa wakiugua ugonjwa wa kupasuka mdomo walifanyiwa upasuaji bila malipo katika hospitali ya rufaa ya Kaunti ya Kakamega.

You can share this post!

MAKALA MAALUM: Kwa nini tuktuk ni kipenzi cha wengi Mombasa

Museveni aondoa masharti makali ya kudhibiti tishio la Ebola

T L