• Nairobi
  • Last Updated May 4th, 2024 3:57 PM
SHINA LA UHAI: ‘Wageni’ hatari wanaohangaisha wakazi hasa vijijini

SHINA LA UHAI: ‘Wageni’ hatari wanaohangaisha wakazi hasa vijijini

Na LEONARD ONYANGO

MIAKA saba tangu Abdirashid Bashir kuumwa na nyoka aina ya koboko (black mamba), hajawahi kupona licha ya kutumia Sh40, 000 katika matibabu.

Bashir ambaye ni mkazi wa wa kijiji cha Bula Skuli, eneobunge la Galole, Kaunti ya Tana River, anasema kuwa tangu wakati huo amekuwa akisumbuliwa na tatizo la kuishiwa na nguvu upande mmoja wa mwili.

“Wakati mwingine ninapokuwa kazini, huu mguu unakwama na kufa ganzi ghafla na inabidi niketi chini kwa muda,” anaeleza.

Bw Abdirashid Bashir akionyesha kovu alilobaki nalo baada ya kuumwa na nyoka katika kijiji cha Bula Skul eneobunge la Galole. Picha/ Stephen Oduor

Nyoka aina ya koboko ana aina mbili za sumu zinazozalishwa katika mwili wake. Aina moja ya sumu huitwa neuro – hii huathiri mfumo wa mishipa (nerve).

Aina ya pili inafahamika kama cardio-toxin ambayo huathiri mfumo wa moyo. Sumu hizi zinaweza kuua binadamu chini ya dakika 20.

Bashir, hata hivyo, anashukuru Mungu kwa kunusuru maisha yake.

Alikuwa amelala chumbani kwenye godoro sakafuni katika nyumba yake aina ya ‘manyatta’ ambapo alitembelewa na ‘mgeni’ wake aliyeingia bila kubisha na kutafuta joto miguuni mwake.

“Nilipojigeuza nilimfinya yule nyoka naye akageuka kwa hamaki na kuniuma, nilishtuka na kupiga kelele lakini hakuna aliyenisikia,” anaeleza.

Alipoendelea kupiga kelele watu waliokuwa karibu walifika na kumfanyia huduma ya kwanza kwanza na kisha kumkimbiza hospitalini kabla ya kulemewa na sumu.

“Nilipelekwa katika Hospitali ya Rufaa ya Hola ambapo wahudumu wa afya walinipa usaidizi,” anasema.

Alipopata afueni alituma jamaa zake kwenda kuripoti kwa polisi kuhusu masaibu yaliyompata na baadaye wakaenda katika afisi za Shirika la Huduma kwa Wanyamapori (KWS) kuanza mchakato wa kulipwa fidia.

Miaka saba baadaye, Bashir bado anasubiri fidia.

Serikali ilisitisha kulipa fidia kwa waathiriwa wa kuumwa na nyoka mnamo 2018.

Hiyo ilikuwa baada ya kubaini kuwa idadi yao ilikuwa juu sana hivyo ikawa vigumu kuwafidia wote.

Wizara ya Afya inakadiria kuwa watu 15,000 huumwa na nyoka kila mwaka nchini Kenya.

Hiyo inamaanisha kuwa mtu mmoja anaumwa na nyoka kila saa humu nchini.

Bashir, kwa mfano, alikuwa ameahidiwa fidia ya Sh30,000 ambayo amekuwa akisubiri tangu 2014.

Hiyo inamaanisha kuwa serikali inafaa kutenga angalau Sh450 milioni kwa mwaka za kufidia waathiriwa wa nyoka pekee.

Bw Mohammed Berhe (aliyevalia barakoa) akielezea changamoto zake baada ya kuumwa na nyoka kijijini Kipini, eneobunge la Tana Delta. Picha/ Stephen Oduor

Katika Kijiji cha Kipini, eneobunge la Tana Delta, Mohammed Berhe, anasema kuwa amewahi kudhuriwa na nyoka mara mbili.

“Mimi nimeponea kifo mara mbili; ya kwanza niliumwa na koboko. Mwaka mmoja baadaye, nilishambuliwa na chatu nikiwa shambani. Chatu huyo alinitemea mate usoni na kunipofua jicho moja,” anaelezea.

Kijijini Kipini kumetokea zaidi ya vifo 10 vinavyohusiana na kuumwa na nyoka.

Kijiji cha Kipini, eneobunge la Tana Delta ambapo wakazi wengi wameathirika na kuumwa na nyoka. Picha/ Stephen Oduor

Kulingana na kiongozi wa watu wanaoishi na ulemavu katika Kaunti ya Tana River Mohammed Babwoya, zaidi ya watu 50 wamepata ulemavu uliosababishwa na sumu ya nyoka katika eneo hilo.

Naye Jane Koome alipoteza binti yake mwaka jana baada ya kuumwa na nyoka ndani ya nyumba yao katika eneo la Kalolone, Igembe, Kaunti ya Meru.Bi Koome anasema kuwa bintiye alienda chumbani kulala baada ya kucheza nje mchana bila kujua kwamba kulikuwa na nyoka ndani.

Alikutana na nyoka aina ya swila (cobra) ambaye alimuuma mkononi.

“Tulitumia bodaboda kumkimbiza katika kituo cha afya cha Kangeta lakini alifariki mara tu baada ya kufika hospitalini,” anasimulia.

Kuna aina 140 za nyoka nchini Kenya. Lakini ni aina 29 ambazo zina sumu.

Kati yazo ni aina tisa pekee zinazosababisha majereha mabaya na hata kifo.

Shirika la Afya Duniani (WHO) limeorodhesha kuumwa na nyoka miongoni mwa maradhi yaliyotelekezwa.

Hii ni kwa sababu tatizo la kuumwa na nyoka limekithiri zaidi katika maeneo ya vijijini na waathiriwa ni watu wa mapato ya chini.

Kenya inakabiliwa na uhaba wa dawa za kutibu waathiriwa wa sumu ya nyoka.

Baadhi ya dawa zinazoagizwa kutoka ughaibuni hukosa kufanya kazi humu nchini.Hii ni kwa sababu sumu ya nyoka aina ya swila wa nchini India ni tofauti na sumu ya swila wa hapa nyumbani.

Taasisi ya Kutafiti Sumu za Nyoka nchini (KSRIC) imekuwa ikifanya utafiti ili kupata dawa iliyo na makali ya kutibu sumu za nyoka wa Kenya.

Mkuu wa KSRIC Dkt George Oluoch, anasema kuwa taasisi hiyo inafanyia utafiti zaidi ya aina 50 za nyoka katika juhudi za kupata dawa.

Bei ya dawa ya sumu ya nyoka inauzwa humu nchini kwa kati ya Sh4,000 na Sh25,000 kwa kutegemea aina ya nyoka na kiasi cha dawa kinachohitajika katika matibabu.

Bw Berhe anasema kuwa alipoteza mjukuu wake baada ya kushindwa kupata matibabu.Licha ya kuwepo kwa changamoto hizo, Dkt Oluoch anasema kuwa mwathiriwa anafaa kukimbizwa hospitalini mara moja baada ya kuumwa na nyoka.

Anasema kuwa waathiriwa huuawa na sumu ya nyoka kutokana na imani potovu kwamba hospitali hazina uwezo wa kutibu majeraha.

Kulingana naye, ukosefu wa takwimu halisi kuhusiana na idadi ya waathiriwa kumesababisha tatizo hilo kutopewa kipaumbele na wakuu serikalini.

Baadhi ya nyoka hatari, Dkt Oluoch anasema wanafanana na nyoka wasio na sumu, hivyo mtu akiumwa anaendelea na shughuli zake za kawaida akidhani kwamba hatodhurika lakini analemewa baadaye.

Waziri wa Utalii Najib Balala anasema kuwa serikali imeanza mchakato wa kubadili sera yake ili kuhakikisha kuwa waathiriwa wanafidiwa.

Kaunti zilizo na visa vingi vya watu kuumwa na nyoka nchini Kenya kwa mujibu wa taasisi ya KSRIC, ni Baringo, Kitui, Samburu, Turkana, Taita Taveta, Kilifi na Kwale. Kaunti nyingine ni Kajiado, Laikipia, Meru, Makueni, Isiolo, Mandera na Wajir.

Kupunguza mikasa ya kuumwa na nyoka

Dkt Oluoch anasema kuwa kufyeka nyasi karibu na nyumba ni njia mojawapo ya kupunguza visa vya kuumwa na nyoka.

“Epuka kuweka maji katika mitungi au vifaa vya wazi karibu na nyumba. Kwa kawaida nyoka huja majumbani kutafuta maji ya kunywa. Kulala ndani ya chandarua cha mbu pia ni njia mojawapo ya kuzuia nyoka kwani atakosa mwanya wa kuingilia ukiwa kitandani,” anasema Dkt Oluoch.

Anasema kuwa mtu anapoumwa na nyoka ni sharti avue vitu kama vile pete na bangili kwenye mkono ulioumwa na kisha apelekwe hospitalini mara moja.

Takwimu

15,000 – idadi ya watu wanaoumwa na nyoka kila mwaka nchini Kenya.

Mtu mmoja (1) huumwa nyoka kwa saa humu nchini

1 kati ya 147 ya wanaomwa na nyoka nchini hufariki.

Kaunti zilizo na visa vingi vya kuumwa na nyoka

  • Baringo
  • Kitui
  • Samburu
  • Turkana
  • Taita Taveta
  • Kilifi
  • Kwale
  • Kajiado
  • Laikipia
  • Meru
  • Makueni
  • Isiolo
  • Mandera
  • Wajir

140 – kuna aina 140 za nyoka nchini Kenya

29 – aina za nyoka wenye sumu

9 – nyoka wenye sumu hatari ambao wamekuwa wakiuma na kuua watu nchini.

Nyoka hatari

Swila (cobra) – wanatofautiana kwa rangi na wanapatikana na wanapatikana kote nchini.

Kifutu (Puff Adder) – wanapatikana kwa wingi katika maeneo ya Magharibi

Kipiribao (Viper) – wanatofautiana kwa rangi kutoka eneo moja hadi jingine. Wanapatikana Magharibi na Bonde la Ufa.

Sh5,000Sh25,000 – gharama ya kutibu sumu ya nyoka

Watu walio hatarini zaidi kuuawa na nyoka

Watoto – sumu inasafiri kwa haraka kutokana na mwili mdogo

Wanawake – kutokana na shughuli wanazofanya kama vile kuteka kuni misituni, kuchuma mboga vichakani.

Sumu ya nyoka husababisha:

  • Matatizo ya kupumua
  • Kuvuja kwa damu hadi kifo
  • Matatizo ya figo
  • Kuharibu viungo vya mwili

Dalili za mtu aliyeumwa na nyoka

  • Kutapika
  • Unyonge
  • Maumivu ya tumbo
  • uchovu

Duniani

Milioni 5.4 Idadi ya watu wanaoumwa na nyoka kila mwaka

81,000138,000 – Idadi ya watu wanaouawa na nyoka kila mwaka

400,000 – idadi ya watu wanaoachwa na ulemavu baada ya kuumwa na nyoka.

You can share this post!

Machifu waeleza hofu kuhusu njaa

Serikali haijaruhusu uagizaji wa chakula chochote cha GMO...