• Nairobi
  • Last Updated May 18th, 2024 1:46 PM
Machifu waeleza hofu kuhusu njaa

Machifu waeleza hofu kuhusu njaa

Na MAUREEN ONGALA

MACHIFU katika eneo la Ganze, Kaunti ya Kilifi wametoa tahadhari kuhusu uhaba wa chakula ambao umeanza kuathiri jamii.

Machifu hao wameomba wadau kujitolea kufadhili misaada ya vyakula, huku ikihofiwa huenda wakazi wakaanza kufa njaa kama hakuna hatua zitachukuliwa haraka.

Chifu wa eneo la Vyambani, Bw Juma Tsori alisema inakadiriwa asilimia 90 katika eneo hilo wanatatizwa na njaa.

“Tunahitaji usaidizi wa dharura kutoka kwa serikali na wahisani ili tuepushie watu wetu maafa kwa kukosa chakula,” akasema katika kijiji cha Dzunguluka.

Bw Tsori alisema uhaba wa chakula umesababishwa na jinsi kulikuwa na upungufu wa mvua ambao ulikosesha wakazi mavuno, kando na changamoto za kifedha zilizotokana na janga la corona.

“Tulipoteza pesa kwa kujaribu kupanda mahindi mara kwa mara ilhali mvua haikutosha katika misimu yote,” akasema.

Katika lokesheni ndogo ya Msanda, Chifu Msaidizi Moses Chitole alisema inahofiwa hali hii itasababisha mizozo ya kinyumbani na kuathiri elimu kwa vile itakuwa vigumu watoto kuenda shuleni wakiwa na njaa.

Naibu Kamishna wa Kaunti anayesimamia eneo la Ganze, Bw George Chege aliungama kuwa wakazi wengi eneo hilo wanahitaji msaada wa chakula na maji.

“Watu wanateseka sana. Imefika kiwango ambapo wanapoitwa kuhudhuria mikutano, wanakuja na matarajio ya kupewa chakula cha msaada,” akasema Bw Chege.

Kulingana naye, ni wakazi wachache tu ambao wanafaidika na mpango wa serikali unaosambaza pesa za msaada.

Mmoja wa wakazi, Bi Beatrice Mwanje alisema huwa wanalazimika kuwapikia watoto wao mara moja pekee kwa siku, hasa usiku.

“Huwa inatulazimu kupika ugali nyepesi ndipo pakiti ya unga itoshe kutumiwa zaidi ya mara moja,” akaeleza.

Mbunge wa Ganze, Bw Teddy Mwambire alitoa wito kwa Wizara ya Fedha iharakishe kutoa pesa za kununua chakula cha msaada la sivyo wananchi wataangamia.

Eneo la Goshi halijapokea mvua kwa karibu miaka mitatu sasa.

Maeneo mengine kama vile Mrima wa Ndege yamekuwa na kiangazi tangu Juni 2020.

“Serikali kuu na ya kaunti zinafaa kushirikiana kutafuta suluhisho sawa na jinsi zilivyofanya mwaka wa 2016 wakati eneo hili lilipokumbwa na ukame,” akasema Bw Mwambire.

Kulingana na mbunge huyo, kuna uwezekano hali inayoshuhudiwa kwa sasa itadumu hadi Machi mwaka ujao kwa hivyo ni muhimu wadau wachukue hatua za dharura.

You can share this post!

Ni uchaguzi wa masonko 2022

SHINA LA UHAI: ‘Wageni’ hatari wanaohangaisha wakazi...