• Nairobi
  • Last Updated May 17th, 2024 2:07 PM
SIKU YA KISWAHILI DUNIANI: Tutambue mchango wa watangulizi wetu

SIKU YA KISWAHILI DUNIANI: Tutambue mchango wa watangulizi wetu

NA ENOCK NYARIKI

ULIMWENGU unaposherehekea siku ya Kiswahili, ni muhimu kuukumbuka mchango wa watu binafsi katika kuikuza na kuikarabati lugha ya Kiswahili hususan nchini Kenya na kuwapa mkono wa tahania.

Nimetaja kuhusu kuikuza na kuikarabati lugha ya Kiswahili ili kurahisisha mjadala huu kwa kuwa mambo haya mawili ni mamoja jinsi zilivyo pande mbili za sarafu moja.

Waama, watu tuliowataja wasingejituma katika kutekeleza jukumu hili mahususi, Kiswahili kisingekuwa kilipo leo hii katika taifa hili. Sitakosea kusema kwamba Kenya imepiga hatua kubwa katika kuhimiza matumizi ya lugha ya Kiswahili kuliko taifa jingine lolote barani Afrika na hata ulimwengu kwa jumla.

Maadamu safu ya ‘Ndivyo Sivyo’ kila Alhamisi katika gazeti hili inahusu kuhimiza matumizi sanifu ya Kiswahili. Nitawaangazia baadhi ya mabingwa ambao wamechangia katika kuhimiza matumizi sanifu ya lugha hii bila kuvifumbia macho vyombo mbalimbali walivyovitumia katika kutekeleza jukumu hilo.

Kipo kipindi cha ‘‘Maswali kwa Wanafunzi’’ ambacho kiliongozwa na Bili Omalla, (Mungu airehemu roho yake) ambacho kilikuwa na mchango muhimu sana si tu katika kuwatia wanafunzi hamasa ya kukipenda Kiswahili bali pia katika kuikarabati lugha hii katika kiwango muhimu.

Kunaye mtangazaji mkongwe wa idhaa ya Kiswahili ya KBC, Bwana Leonard Mambo Mbotela, ambaye juhudi zake katika kuhimiza matumizi sanifu ya lugha ya Kiswahili haziwezi kumithilishwa na mtangazaji mwingine wa enzi zake.

‘Ongea Lugha Sanifu ya Kiswahili’ – kipindi alichokianzisha gwiji huyu – kilichochea kuanzishwa kwa safu hii ya ‘Ndivyo Sivyo’ katika gazeti la Taifa Leo.

Hongera enyi nyote ‘mliojitwika magogo mazito’ kukifikisha Kiswahili kilipo leo hii!

  • Tags

You can share this post!

USHAURI NASAHA: Zipo taaluma tele za Kiswahili katika soko...

VYAMA: CHAKIMO kilivyo mhimili thabiti katika ukuzaji...

T L