• Nairobi
  • Last Updated April 27th, 2024 11:15 AM
Simulizi ya Gachagua alivyopoteza ndugu zake kupitia pombe

Simulizi ya Gachagua alivyopoteza ndugu zake kupitia pombe

NA MWANGI MUIRURI

NAIBU Rais Rigathi Gachagua Jumapili, Machi 17, 2024, alisimulia jinsi alivyopoteza ndugu zake kwa sababu ya pombe.

Kupoteza ndugu zake, Bw Gachagua alisema ni mojawapo ya sababu zinazomshinikiza kupambana na pombe haramu na hatari nchini.

“Nilipoteza ndugu zangu kwa sababu ya pombe na matumizi ya dawa za kulevya. Hii ndio maana unaona nikiendeleza vita dhidi ya pombe,” akasema Bw Gachagua

Bw Gachagua alisimulia hayo kwenye Inooro TV huku akieleza kwamba walikuwa tisa katika familia yao, kaka wanne na dada watano ila baadhi yao walizamia pombe.

“Ndugu yangu Dkt Wachira Gachagua alifariki kutokana na pombe. Alikuwa akifanya kazi kama daktari nchini Afrika Kusini. Nilienda kuchukua mwili wake mnamo 2012 na kumzika. Mwaka 2014 kaka yangu Nderitu Gachagua alifariki kutokana na Saratani ya kongosho,” Bw Gachagua alisema.

Aliongeza kuwa ndugu yake mwingine Bw Reriani Gachagua alikuwa mlevi ambaye hakuwahi kumsikiza.

“Nilijaribu juu chini ila ikashindikana. Nilijaribu hata kuishi naye nyumbani kwangu. Nilipochaguliwa kuwa naibu rais 2022 nilifurahi sana nikampa pesa ili aende kusherehekea. Aliingia kwenye pombe. Akaaga.”

Bw Gachagua alisema pombe imemfanya abaki pweke katika boma la babake lililozingirwa na makaburi.

Alisema pia alijitosa katika ulevi hadi mkewe-Pastor Dorcas Rigathi–alipofanikiwa kumshauri na akaamua kuacha pombe.

“Ikiwa ningempuuza, kuna uwezekano kwamba ningekuwa nimekufa na singekuwa Naibu Rais wa sasa.”

Ni katika hali hizo ambapo Naibu Rais alisema anapinga uamuzi wa hivi majuzi wa mahakama katika kaunti ya Kiambu ya kusema kuwa pombe ya kitamaduni ya Muratina si haramu.

“Bila kujali uamuzi wa mahakama ulioidhinisha utayarishaji wa pombe ya Muratina kama pombe ya kitamaduni, lazima tuunde sheria za kimsingi. Wazee ambao mahakama iliwapa mamlaka ya kusimamia uundaji wa pombe hiyo ya kitamaduni hawawezi kuaminiwa. Jinsi walivyo sasa, baadhi yao hawawezi kuaminiwa kuunda Muratina kwa hafla za kitamaduni,” alisema.

“Baadhi ya wazee hao hawana uvumilivu kama huo na pombe. Wanataka Muratina papo hapo,” akaongeza Bw Gachagua.

Alisema atakutana na wazee hao na kuwaleta pamoja ili waweze kuangalia namna ya kusonga mbele.

Kwa upande mwingine, alisema kuwa hatalegeza kamba kwani ataendelea na vita yake dhidi ya pombe hata kama wengi serikalini wanajaribu kumzima.

  • Tags

You can share this post!

Tutakusaidia kupata mke, Maribe amwambia Itumbi

Putin ajigamba kwa ‘jeuri’ baada ya ushindi mkubwa...

T L