• Nairobi
  • Last Updated May 17th, 2024 2:07 PM
TAHARIRI: Mutyambai atoe namba kwa umma

TAHARIRI: Mutyambai atoe namba kwa umma

KITENGO CHA UHARIRI

INSPEKTA Jenerali wa Polisi Hillary Mutyambai ameonya maafisa wa polisi wenye mazoea ya kushinikiza watu kununua mafuta ya gari kabla ya kuenda katika maeneo ya mikasa au uhalifu.

Inspekta Jenerali alisema kwamba polisi wanaotaka kununuliwa mafuta au kupewa fedha wanakiuka sheria na watakaopatikana na hatia wataadhibiwa vikali.

Bw Mutyambai aliyekuwa akizungumza kupitia ukumbi wa #EngageTheIG kwenye mtandao wa Twitter, alitoa onyo hilo baada ya Wakenya kulalamika kwamba kumekuwa na ongezeko la visa vya maafisa wa polisi kuomba mafuta au hongo wanaporipoti visa vya uhalifu.

Onyo la Mutyambia ni habari njema ambazo zitapokelewa na watu wengi kwa furaha.

Hii ni kwa sababu inatarajiwa kwamba maafisa wa polisi sawa na kauli mbiu yao, wanafaa kuwa watumishi kwa wote kwa maana kwamba wanafaa kuhudumia raia wote bila ubaguzi.

Hata hivyo, kumekuwepo visa vingi ambapo wahalifu huvamia watu iwe mchana au usiku kisha polisi waitwapo huhitaji kuhongwa ndipo waende katika maeneo ya tukio.

Tabia hii imewahi kusababisha vifo vya watu au pengine mali ya thamani kubwa kuibwa.

Matukio kama haya yamefanya raia kukosa imani kabisa na vikosi vya polisi.Kumekuwepo hali ambapo polisi huitisha hongo ya hadi Sh50,000 kusaka wezi au wahalifu wengine.

Mtu wakati mwingine hushawishika kutoa hela hizi kwa tumaini kwamba atafaulu kurejeshewa mali aliyoipoteza.

Hata hivyo, hela hizi huishia kuzama na hivyo kuwa pigo zaidi kwa waathiriwa wa uhalifu au wizi.

Wakati mwingine polisi huitwa na raia kunapotokea ajali na baadhi yao hulimatia kufika katika eneo la tukio. Visa kama hivi huchangia kupotea kwa maisha ya watu kutokana tu na mapuuza ya maafisa wa polisi.

Ni muhimu hata hivyo kusisitiza kwamba si maafisa wote wa polisi huwa watepetevu kazini. Maafisa wengi ni wachapakazi wa kupigiwa mfano.

Kwa wale maafisa walio na mazoea ya kuitisha hongo, Inspekta Jenerali ametoa ushauri mzuri ila lipo pengo katika nasaha yake kwa umma.

Mutyambai alifaa kupiga hatua na kuambia umma ni wapi raia wanaweza kuripoti visa ambapo wataitishwa ‘mafuta’ na polisi.

Iwapo kweli Inspekta ana nia ya dhati ya kukabili ufisadi katika idara ya polisi, basi aambie umma pa kuripoti malalamishi dhidi ya polisi watovu wa maadili.

You can share this post!

Nafuu kuu watalii wakifurika Mombasa

Wavuvi Faza wapinga marufuku dhidi ya mitego ya samaki...

T L