• Nairobi
  • Last Updated May 2nd, 2024 8:55 PM
Nafuu kuu watalii wakifurika Mombasa

Nafuu kuu watalii wakifurika Mombasa

Na WINNIE ATIENO

MATUMAINI ya sekta ya utalii kufufuliwa tena Mombasa yameongezeka baada ya idadi ya wateja wanaokodi vyumba hotelini kupanda sana tangu serikali ilipolegeza kanuni za kupambana na maambukizi ya virusi vya corona.

Imebainika kuwa vyumba katika hoteli za ufuoni zimejaa kwa asilimia 60, kinyume na hali ilivyokuwa awali ambapo hoteli zilikuwa tupu zikiathirika kibiashara.

Hali hii imepigwa jeki na hatua ya mashirika mbalimbali kuanza kurejelea mikutano na makongamano hotelini.

Mojawapo ya hafla kubwa ambayo imevutia idadi kubwa ya wageni ni michezo ya muungano wa spoti za serikali za kaunti.

Wasimamizi wa hoteli wamesema michezo hiyo pekee ya watumishi wa kaunti imevutia zaidi ya watu 10,000.

Michezo hiyo inayohusisha kaunti 38 ilikuwa imeahairishwa mwaka uliopita wakati Rais Uhuru Kenyatta alipiga marufuku spoti nchini kufuatia ongezeko la maambukizi ya virusi vya corona.

Kanuni kali za kudhibiti msambao wa ugonjwa huo pia ziliwafanya waandalizi kushindwa kuwaleta pamoja wanamichezo wote.

Hoteli kama vile Pride Inn Paradise, Whitesands, English Point Marina, Bamburi na Serena pia zimethibitisha kupata biashara baada ya serikali na sekta ya kibinafsi kupeleka mikutano yao katika maeneo hayo.

“Tunafurahi na kuishukuru serikali kwa kuondoa kafyu ambayo imefanikisha michezo hii kufanyika hapa Mombasa ambapo vile vile itainua uchumi wetu. Pia tunashukuru serikali za kaunti kwa kuchagua Mombasa kwa michezo hii,” alisema Bw Aharub Khatri, Spika wa Bunge la Mombasa.

Kauli hiyo iliungwa mkono na Kaimu Katibu wa Kaunti ya Mombasa, Bw Joab Tumbo.

Bw Habel Mwakio aliye katika sekta ya vyumba vya kukodisha alisema biashara imeimarika tangu kafyu ilipoondolewa pamoja na kanuni nyinginezo kama vile za kusafiri usiku.

“Vyumba vya kukodi maeneo ya Nyali, Shanzu na Mtwapa vimejaa. Wageni wamefurika Mombasa na kuipiga jeki sekta ya utalii,” alisema Bw Mwakio.

Afisa Mkuu wa Muungano wa Wawekezaji wa Utalii, tawi la Pwani, Dkt Sam Ikwaye alisema wengi wao hawakutarajia utalii kufufuka haraka jinsi hii.

You can share this post!

Vinyago wa Uhuru

TAHARIRI: Mutyambai atoe namba kwa umma

T L