• Nairobi
  • Last Updated May 21st, 2024 6:55 AM
TAHARIRI: Koome aonyeshe hapokei maagizo

TAHARIRI: Koome aonyeshe hapokei maagizo

KITENGO CHA UHARIRI

KUTEULIWA rasmi kwa Jaji Martha Karambu Koome kuwa Jaji Mkuu mpya kunaweka historia nchini.

Tangu Kenya ipate uhuru miaka 57 iliyopita, Jaji Koome anakuwa mwanamke wa kwanza kushikilia wadhifa huo wa Jaji Mkuu.

Kuteuliwa kwake na Rais Uhuru Kenyatta baada ya kuidhinishwa na Bunge, kunatoa mwelekeo mpya kwa wanawake katika eneo la Afrika Mashariki. Ameteuliwa miezi miwili tu baada ya Bi Samia Suluhu Hassan kuapishwa kuwa Rais wa kwanza mwanamke Tanzania na katika nchi tatu za Afrika Mashariki.

Jaji Koome anaangaliwa na wanawake wote, wakiwemo wasichana kuwa kielelezo kwao. Wanamtarajia aonyeshe kwamba wanawake wanaweza kuongoza na kufanya maamuzi muhimu. Wanamtarajia aikuze heshima ya mwanamke kwa kuongoza mfumo wa sheria ambao hautaegemea upande wowote.

Ana bahati kwamba Katiba inatoa masharti makali ya kumwondoa Jaji Mkuu. Kwa maana hiyo, ana nafasi kubwa ya kuongoza kwa miaka yote minane akiwa Jaji Mkuu na akitaka astaafu wakati huo akiwa na miaka 69 au awe Jaji wa Mahakama ya Juu kwa mwaka mmoja hadi afikishe miaka 70.

Maamuzi atakayofanya, yafaa yawe yanayotokana na uelewa wake wa sheria na haki. Hafai kuonekana kuwa anayehudumu kuwafurahisha watu fulani, kwa sababu hawana uwezo wala mamlaka ya kumwondoa.

Wakati wa mahojiano ya kumsaka Jaji Mkuu, suala la jinsi wananchi wanavyoichukulia idara ya mahakama lilijitokeza. Karibu kila mmoja wa watu kumi waliohojiwa, alitakiwa aeleze angefanya nini kubadili sifa mbaya ya idara hiyo muhimu.

Jaji Koome alikumbushwa wakati huo kuhusu tukio ambapo aliitwa usiku wa Sikukuu, ili kubadilisha uamuzi wa jaji George Odunga. Alijitetea kwamba aliagizwa kufanya hivyo, na akatoa uamuzi kwa manufaa ya umma.

Jambo hilo huenda likawatia wasiwasi Wakenya kwamba Jaji Koome anaweza kuwa mtu wa kupokea maagizo ‘kutoka juu.’

Mtihani wake wa kwanza sasa utakuwa jinsi atakavyoshughulikia rufaa kuhusiana na Mswada wa marekebisho ya Katiba (BBI).

Aelewe kuwa mtangulizi wake, Jaji David Maraga aliweka viwango vya juu vya utendakazi. Wakenya watampima kutumia viwango hivyo.

You can share this post!

Matumaini ya mwafaka kati ya Israeli na Palestina yafifia

KAMAU: BBI: Kimya cha makanisa kwa hakika chatamausha