• Nairobi
  • Last Updated May 20th, 2024 9:16 PM
TAHARIRI: Serikali iharakishe kandarasi mpya

TAHARIRI: Serikali iharakishe kandarasi mpya

KITENGO CHA UHARIRI

MOJAWAPO ya nguzo Nne Kuu za Utawala wa Rais Uhuru Kenyatta ni ustawishaji viwanda nchini.

Viwanda ni njia ya haraka na rahisi ya kuunda nafasi za ajira kwa vijana na watu wa eneo vinakopatikana. Aidha, viwanda huwapa soko wakulima, wavuvi na watu wote wanaohusika na uzalishaji wa malighafi.

Mojawapo ya viwanda chini ya mpango huo ni kile cha samaki cha Liwatoni Kaunti ya Mombasa. Imetangazwa kwamba sasa serikali imefuta kandarasi ya ujenzi, kwa madai kuwa kampuni ya Daniel’s Outlets Ltd ilikiuka masharti ya ujenzi.

Serikali inadai kwamba kampuni iliyopewa kandarasi ilijihusisha na ufisadi na ulaghai. Kwamba kipengee cha 15.2 (f) cha Tume ya Maadili na Kupambana na Ufisadi (EACC) kinairuhusu serikali kusitisha kandarasi iwapo mwanakandarasi atatoa au kuahidi kutoa hongo, zawadi au kiinua mgongo kwa mtu yeyote, moja kwa moja au kupitia mtu mwingine ili apatiwe tenda.

Kama EACC ilitoa ushauri baada ya uchunguzi wa kutosha, hiyo ni hatua nzuri katika kukabiliana na ufisadi nchini.

Lakini kusimamishwa kwa mwanakandarasi kusiwe sababu kwa serikali kukata matumaini ya maelfu ya wakazi wa Pwani wanaotegemea uvuvi.

Kiwanda hicho ambacho Rais Kenyatta ametambua kama mradi muhimu wa kuimarisha uchumi wa baharini, kilinuiwa kubadilisha Liwatoni kuwa bandari kamili ya uvuvi. Kilitarajiwa kuwa na vyumba vya barafu vya kuhifadhi samaki. Kupitia shughuli hizo, serikali ilitarajiwa kuongeza thamani ya samaki kabla ya kuuzwa nje ya nchi.

Kufutwa kwa kandarasi hiyo kutahujumu mipango ya Rais Kenyatta na nafasi ya kuimarisha uvuvi kwenye bahari. Kiwanda hicho kilitarajiwa kuwa tegemeo kubwa kwa watu wa Pwani ambao wamekuwa wakilia kila siku kutokana na kuuawa kwa viwanda vyao siku za nyuma.

Ingawa Pwani hukuza kwa wingi korosho, nazi, mihogo kati ya mazao mengine, kiwanda pekee kilichojengwa upya majuzi ni kile cha sukari za Kwale Interional Sugar Company (Kiscol).

Wakenya wanaunga mkono juhudi za kukabili ufisadi katika sekta zote. Kama mtu alijipatia kandarasi kwa njia isiyostahili, ni lazima sheria ichukue mkondo wake. Lakini katika kufanya hivyo, wananchi wasiwe nyasi kwenye vita vya ndovu.

Serikali iharakishe kutangaza upya kandarasi hiyo, ili juhudi za Rais kutimiza ajenda Kuu Nne zisivurugwe.

You can share this post!

Kibagare Slums yajiweka pazuri kuwania ubabe wa Nairobi...

Afrika ikiungana na China zitaweza kujitegemea kwa tiba za...